Pamba Jiji yaenda chimbo la wiki tatu

KIKOSI cha Pamba Jiji kitaondoka keshokutwa (Jumapili) jijini hapa kwenda mjini Morogoro kuweka kambi ya takribani wiki tatu kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Bara chini ya Kocha Mkuu, Goran Kopunovic na msaidizi wake, Salvatory Edward.

Wachezaji wa timu hiyo wapya na wale wa zamani wameshaingia kambini tangu Jumatatu kwenye maskani yao eneo la Rwanima jijini hapa, wakianza mazoezi mepesi huku wakisubiria wengine, huku msafara wa kwanza ukiondoka na wachezaji 18 Jumapili kwenda Morogoro.

Klabu hiyo inaendelea na zoezi la usajili wa wachezaji wapya huku ikiwa tayari imewaongezea mikataba wachezaji wa zamani saba na kutambulisha wapya ambao ni Frank Ng’amba, Yona Amos, Samson Madeleke, Justin Bilal, Ibrahim Abraham, Beny Nakibinge, Erick Okutu na Salehe Masoud.

Afisa Habari wa Pamba Jiji, Martin Sawema aliliambia Mwanaspoti kikosi chao kitaweka kambi katika eneo la Highlands mjini Morogoro kwa takribani siku 14 hadi 21, huku kikosi chao cha msimu huu kikitarajiwa kuundwa na wachezaji 25.

“Kambi yetu itakuwa Morogoro katika Uwanja wa Highlands Sabato tutaondoka Mwanza Jumapili tukianza na wachezaji 18 ambao wapo watakuwa tayari kufikia hiyo siku lakini kikosi chetu cha msimu huu kitaundwa na wachezaji 25.”

“Tutakaa wiki kuanzia mbili hadi tatu na kurejea jijini Mwanza mwanzoni mwa mwezi Agosti kujiandaa na tamasha la Pamba Day tulilopanga lifanyike Agosti 10, mwaka huu,” alisema Sawema. Kiungo wa timu hiyo, Salim Kipemba ambaye ameongezewa mkataba na amesharipoti kambini, alisema mazoezi mepesi yanakwenda vizuri na benchi la ufundi liko vizuri kwani limewapokea vizuri huku wakitarajia kuanza mazoezi rasmi wiki ijayo.

“Tumeanza mazoezi lakini rasmi ni wiki ijayo kwa sababu wiki hii ndiyo watu wameanza kuingia. Tumejiandaa kwa ligi, timu inasajili lakini sisi tuliobakizwa ni kupambana kupata namba kwani kila mtu anataka kupambana aonekane ili apate nafasi kwenye kikosi,” alisema Kipemba.

Related Posts