Dar es Salaam. Licha ya juhudi zinazofanyika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa kila sekta, imebainika kuwapo mwamko mdogo wa wanahabari wa Afrika Mashariki kuripoti matumizi bora ya nishati ya umeme jua.
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti kuhusu uchapishaji habari zinazohusu nishati ya umeme jua katika sekta ya kilimo, ni habari 63 pekee ziliripotiwa mwaka jana katika mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda.
Ripoti hiyo ilihusisha vyombo sita vya habari kutoka mataifa hayo, yaani magazeti ya Mwananchi, Daily Nation na New Vision; na mashirika ya utangazaji ya Taifa ya KBC (Kenya), TBC (Tanzania) na UBC (Uganda).
Miongoni mwa sababu zinazotajwa katika utafiti huo ni kukosekana mvuto wa soko la aina hiyo ya habari, na ombwe la uelewa kuhusu namna ya kuripoti habari hizo kwa wahariri na waandishi wa habari.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi, Julai 11, 2024 na Mhadhiri wa Shule Kuu ya Habari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Darius Mukiza, alipowasilisha ripoti ya utafiti huo uliofanyika mwaka 2023 chini ya Kituo cha Umahiri katika Vyombo vya Habari (ACME).
Ingawa si kwa kiwango cha kuridhisha, Uganda imeonekana kuongoza kwa kuripoti habari 30.
Kenya ilifuata kwa kuripoti habari 23 huku Tanzania ikiwa na habari 10 pekee.
Ripoti imebainisha kwa upande wa magazeti habari ziliwekwa kuanzia ukurasa wa tano na kuendelea.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA-TAN), Salome Kitomari amesema vyombo vya habari vinaangalia zaidi habari zinazovipa faida kibiashara.
“Ukweli sisi wanahabari ili tuweke habari katika kurasa za mbele tunazingatia vitu vingi na hasa ni biashara, kwa hiyo hizi habari za nishati ya umeme jua zimeonekana kama si kipeumbele katika soko,” amesema.
Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Joseph Damas amesema kuna umuhimu wa kufanya tathmini ya mahitaji ya jamii kuhusu habari hizo.
Tathmini hiyo kwa mujibu wa Damas, itaviwezesha vyombo vya habari kujua ni kwa kiasi gani aina hiyo ya habari ina soko.
“Sisi (Mwananchi) hatuandiki habari kama hatujui tunaandika kwa ajili ya nini na kwa nani, kila tunachokiandika tunakuwa na matarajio, kwa hiyo kuna umuhimu wa kujua kwa kiwango gani habari hizi zinahitajika na jamii,” amesema.
Awali, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema maarifa kwa waandishi wa habari na wahariri kuhusu uandishi wa habari hizo ndiyo changamoto.
Amesema kuna umuhimu wa kuwapo uwezeshaji wa rasilimali zitakazowezesha waandishi kuibua habari hizo na zikafanywa kwa ukubwa.
Ofisa Mipango wa ACME, Brian Ssenabulya amesema uzinduzi wa ripoti hiyo utafuatiwa na semina kwa wanahabari kuhakikisha wanajengewa uwezo juu ya kuripoti habari za nishati ya umeme jua.
Amesema taasisi hiyo itafanya kila namna kuhakikisha inawawezesha wanahabari kifedha ili wakaripoti aina habari hizo.