Majaliwa kuongoza NBC Dodoma Marathon, jezi zazinduliwa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuongoza washiriki zaidi ya 8,000 wa mbio za NBC Dodoma Marathon zitakazofanyika Julai 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, imefahamika. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Hafla ya kumtambulisha mgeni rasmi huyo imefanyika jijini Dar es Salaam jana jioni ambapo pia ilishuhudiwa muandaaji wa mbio hizo Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ikizindua jezi maalum zitazotumika kwenye msimu wa tano wa mbio hizo sambamba na kuitambulisha kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL) kama mshirika rasmi wa vinywaji na burudani kwenye tukio hilo.

Lengo kuu la mbio hizo ni kukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na  kutoa ufadhili wa elimu kwa wakunga  ili kuboresha afya ya mama wa mtoto.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi alisema uwepo wa Waziri Mkuu kama mgeni rasmi wa mbio unatarajiwa kuongeza hamasa kwa washiriki hao kutoka makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo wakimbiaji kutoka taasisi na mashirika mbalimbali, wakimbiaji wa kimataifa, vilabu mbalimbali vya wakimbiaji nchini (Jojgging clubs) na wakimbiaji mmoja mmoja, huku lengo likiwa ni kuunga mkono agenda kuu za mbio hiyo ya kuokoa maisha ya mama na mtoto.

“Pamoja na uwepo wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambae kimsingi amekuwa nasi mara kadhaa kwenye mbio hizi, tunafarijika zaidi kuona kwamba wadau mbalimbali wanaendelea kujitokeza ili kutuunga mkono kwenye mbio hizi ambapo hii leo tunaitambulisha kampuni ya Serengeti Breweries kupitia kinywaji chao cha Captain Maorgan kama mshirika mkuu wa vinywaji na burudani kabla na wakati wa tukio hilo,’’ alisema Sabi huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya taasisi mbalimbali katika kufanikisha azma ya pamoja katika kuisaidia jamii.

Aidha, Sabi aliwashukuru wadau mbalimbali yakiwemo mashirika na kampuni zilizoshiriki kufanikisha mbio hizo ikiwemo kampuni ya Bima ya Sanlam Insurance ambao ni wafadhili wakuu wa mbio hizo huku wadau wengine wakiwa ni Vodacom Tanzania, Jubilee Allianz, Serengeti Breweries, Gardaworld security, Strategis Insurance, Redcross, Precission Air, Metropolitan Life Insurance, Britam Insurance, Tembo Kabanga Nickel.

Akizungumzia ushirikiano huo mpya, Mkurugenzi wa Masoko na Ubunifu wa Serengeti Breweries Limited (SBL), Henry Esiaba alisema kampuni hiyo kupitia bidhaa yake ya Captain Morgan imejipanga kimkakati zaidi kuhakikisha washiriki wa mbio hizo wanapata wasaa wa kufurahia pamoja kabla na baada ya mbio kupitia matukio mbalimbali yaliyoandaliwa ikiwemo tafrija mbalimbali zitazohusisha uwepo wa muziki na vinywaji mbalimbali vinavyozalishwa na kampuni hiyo.

Akizungumzia ubora wa jezi hizo zenye rangi tano tofauti ikiwemo bluu, njano, nyeupe, nyekundu na nyeusi, Mkuu wa Idara ya Masoko wa NBC, David Raymond alisema tofauti ya rangi hizo ambazo zimebeba maana tofauti inalenga kutoa chaguzi tofauti kwa kuzingatia tafsiri ya rangi na mtindo (design) ya jezi husika lengo likiwa ni kuhakikisha kila mshiriki anaridhika na kufurahia aina ya jezi atakayovaa  kwenye mbio hizo.

Akizungumzia ushiriki wa mbio hizo, Raymond aliwaomba washiriki waendelee kujisajili kupitia tovuti ya www.events.nbc.co.tz na kuchangia kiasi cha TZS 35,000 kwa usajili wa washiriki mmoja mmoja au 25,000 kwa usajili wa kikundi chenye idadi ya watu wanaozidi 25.

Related Posts