WANANCHI MKALAMA WAHIMIZWA KUJITOKEZA KWA WINGI UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ndugu Godfrey Mzava amewataka wananchi wilayani Mkalama kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba 2024.

 

Wito huo ameutoa Julai 10,2024 mara baada ya kumaliza kukagua, kuzindua na kuweka jiwe la Msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali wilayani Mkalama.

 

 

“Uchaguzi upo tayari mlangoni, tujitokeze kwa wingi kushiriki uchaguzi huu muhimu wa kuchagua viongozi wetu. Tukio la kupiga kura halitachukua muda mrefu, twendeni tukapige kura. Lakini pia tulinde amani na umoja wakati wa uchaguzi,” amesema Mzava.

 

Akizungumzia suala la mabadiliko ya tabia nchi, Ndugu Godfrey Mzava amewataka wananchi wilayani Mkalama kuacha tabia ya kukata miti hovyo, badala yake wajikite katika upandaji miti ili kuepukana na madhara yanayotokana na uharibifu wa mazingira.

 

“Tuchukue wajibu wa kulinda mazingira yetu, nimepita shule ya Mkalama One nimeona kazi nzuri, nimeona mmeanzisha mradi wa mazingira. Tukifanya hivi tutakuwa vinara katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira” , amesema Mzava.

 

Awali akizungumzia miradi iliyopitiwa na Mwenge wa Uhuru 2024, Ndugu Godfrey Mzava ameipongeza wilaya ya Mkalama kwa usimamizi mzuri katika kusimamia fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo “Tumepita tumeona kazi kubwa imefanyika wilayani Mkalama, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu anatoa fedha lengo likiwa ni kuona wananchi wanapata huduma nzuri”, ameongeza Mzava.

 

Mbio za Mwenge 2024 wilayani Mkalama zimezindua mradi mmoja na kuweka jiwe la msingi katika miradi miwili ambapo miradi yote ina thamani ya jumla ya shilingi 2,067,623,126.00 na umetembelea program 8 ambazo ni Lishe, Mazingira, Rushwa, Dawa za kulevya, VVU/UKIMWI, Malaria, Elimu kwa Mpiga Kura na Kongamano la Vijana.

 



Related Posts