Kampuni ya Kilombero Sugar na
Kampuni tanzu za Illovo Sugar Africa, zimeungana kupitia Kampeni yao ya
Kilimanjaro Expeditions kukabidhi taulo za kike 2400 katika shule ya
Sekondari Mieresini kabla ya kuelekea kwenye kilele cha mlima
Kilimanjaro.
Kampeni
hiyo itahusisha wapanda mlima 17 kutoka nchi 8 tofauti zilizopo chini ya
ABF Sugar Group ambapo wafanyakazi hao wamechaguliwa kupanda Mlima
Kilimanjaro, kilele kirefu zaidi barani Afrika. Msafara huo ni wa
kuheshimu urithi wa Mandela na una lengo mahsusi la kuchangisha fedha na
uhamasishaji kwa ajili ya kushughulikia hedhi salama na kuhakikisha
wasichana wanaenda shule katika mazingira mazuri katika nchi zote ambazo
ABF Sugar Group wanatoa huduma.
Akizungumza
katika hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika katika shule ya
Sekondari Mieresini, Marangu Mkoani Kilimanjaro, Meneja Mawasiliano na
Mahusiano na Wadau wa Kilombero Sugar, Bw. Victor Byemelwa, alifafanua
kuwa msafara huo unalenga kukusanya fedha kwa ajili ya mpango wa
kukabiliana na hedhi salama katika jamii ya watanzania na jamii
nyinginezo ambapo huduma zao zinapatikana ili kupaza sauti katika
kukabiliana na tatizo hili.
Lengo ni kuonesha utofauti na
ushirikishwaji wa wapanda mlima kutoka sehemu mbalimbali katika kundi
hili na kuonyesha uzuri wa Tanzania kuwa nchi mwenyeji wa kundi hili na
kusisitiza Mlima Kilimanjaro kuwa kivutio cha utalii kwa dhamiri.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa kampuni ya Kilombero
Sugar, Bw. Fimbo Butallah, alisema kuwa “Kilombero Sugar, pamoja na
kampuni tanzu nyingine za ABF Sugar, leo tunakabidhi taulo za kike 2400
kwa shule ya hii ikiwa ni sehemu ya dhamira yetu ya kibiashara katika
kustawisha shule na jamii ambazo tunatoa huduma.
Bw. Butallah
aliongeza kuwa anafurahishwa na takriban asilimia 60 ya wanafunzi wa
shule hii ni wasichana, huku akisisitiza lengo la kuwaweka wasichana
shuleni kwa kupambana na hedhi salama. Alisisitiza mipango ya kuendelea
kushughulikia ajenda hii kwa kuchangia shule zingine katika mikoa
tofauti katika miezi inayofuata. Akihutubia hadhara hiyo, Mkuu wa Wilaya
ya Moshi, na mgeni rasmi wa hafla hiyo Mhe. Zephania Stephen Sumaye,
alibainisha kuwa Serikali ipo tayari na inaunga mkono kila wakati kwa
wadau wote wanaounga mkono ajenda za Serikali, ikiwemo sekta ya elimu.
Alisema, ‘Leo, natoa shukrani zangu za dhati kwa Kampuni ya Kilombero
Sugar kwa kushirikiana na jamii kwa namna ya kipekee.’
Akipokea
msaada huo wa taulo za kike 2400 Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari
Mieresini Bw. Prosper August Mosha alitoa shukurani za jumla za shule
hiyo kwa msaada huo huku akisisitiza kuwa umekuja wakati mwafaka na
kutimiza malengo yaliyokusudiwa. Shule inakaribisha mipango kama hii
kutoka kwa wadau wengine ili kuhakikisha tunaendelea kuweka mazingira
mazuri ya kusomea.