Wasio na makazi wanavyolala Dar

Dar es Salaam. “Sikuwahi kufikiria kukosa makazi na kulala nje, lakini imenibidi kutokana na hali iliyonikuta, hadi leo nawalaani mgambo, ndiyo chanzo cha kuharibika maisha yangu na kuanza kulala hapa nilipo.”

Hiyo ni kauli ya Rashida Omari (45), mzaliwa wa Kigoma ambaye kwa sasa analala kibarazani, kwenye ghorofa lililopo kwenye makutano ya Barabara ya Bibi Titi Mohammed na Morogoro, jijini Dar es Salaam.

Rashida ni miongoni mwa mamia ya watu wanaolala nje kwa kukosa makazi jijini humo, suala ambalo hata hivyo, halijakatisha harakati zao za kutafuta maisha, miongoni mwao wakiwemo ombaomba na wenye shughuli nyingine ndogondogo.

Baadhi ya watu hao waliozungumza na Mwananchi, walisimulia adha wanazopata kwa kulala nje, ikiwa pamoja na kukosa faragha, kuibiwa vitu na wengine wakinyanyaswa kingono.

Baridi kali usiku, fukuzafukuza za mgambo na kukoswakoswa na ajali pia ni miongoni mwa masaibu wanayokumbana nayo usiku kila mara.

Maeneo ambayo wengi wa watu hao wameonekana wakilala ni chini ya madaraja na barabara za juu, nje ya misikiti na maduka.

Mwananchi limezunguka maeneo mbalimbali yanayotumiwa na wakazi hao kwa malazi kupata mikasa mbalimbali inayowakabili, kadhalika sababu zilizowafikisha katika hali hiyo.

Akizungumza na Mwananchi katika eneo analolala baada ya mihangaiko ya mchana, Rashida anasema alitoka kwao Kigoma kwa lengo la kutafuta maisha kwa kufanya biashara. Anasema lengo lake awali lilifanikiwa na alipanga chumba eneo la Ilala Mchikichini.

Akiwa huko, alikuwa anauza bidhaa ndogondogo na vinywaji  vilivyosaidia kumuingizia kipato cha siku, hadi mgambo walipobadilisha mwelekeo wa maisha yake.

Baada ya kuongeza mtaji, anasema alifungua biashara nyingine ya kuuza mitumba, huku eneo la kwanza akamweka kijana aliyemtoa kijijini kwao, ili aendeleze biashara hiyo huku yeye akisimamia biashara ya nguo.

Anasema kuna siku askari wa Jiji walifanya opereshini ya kukamata wafanyabiashara na mmoja ya waliokamatwa alikuwa kijana wake, walibeba vitu vyake na kumuumiza kijana huyo wakati wa purukushani.

“Nilipigiwa simu kuambiwa kijana wangu anapigwa na vitu vyangu vimechukuliwa, nilipofika nikakuta kijana ameumia, maamuzi ya haraka ni kumchukua na kumpeleka hospitali nikiwa nimeacha biashara yangu ya nguo bila kukabidhi mtu,” anasema Rashida.

Baada ya tukio hilo, anasema alitumia akiba kufufua biashara yake ya vinywaji na vitu vidogo huku akilipa madeni ya mikopo na alimrudisha kijana kijijini baada ya kupona.

Wakati akiendelea kujitafuta, mwenyewe alikamatwa na mgambo na alipelekwa Mahakama ya Jiji ambapo alifunguliwa kesi ya uchafuzi wa mazingira na kutakiwa kulipa faini ya Sh50,000 ambazo hakuwa nazo, hivyo alipelekwa gereza la Segerea kutumikia kifungo cha miezi mitatu.

Anasema akiwa gerezani mwenye nyumba alihitaji chumba chake, maana hakuwa amelipa kodi miezi minne, huku akiwa hajamaliza kurejesha mkopo, hivyo wadai nao wakaamua kuuza vitu vyake vya ndani, mwenye nyumba akampangisha mtu mwingine.

“Nilipotoka gerezani niliamua kuwa ombaomba kwenye misikiti na kulala kwangu ikawa barabarani (pembeni) maana sikuwa na mahali pa kwenda,” anasema.

Ukiacha simulizi ya Rashida, hapo anapolala pia yupo Neema (alijitaja kwa jina moja) anayetokea Manyoni, Singida, ambaye alikuwa muuza mbogamboga mtaani na kuachana na biashara hiyo baada ya kuzidiwa ujanja na washindani.

“Nina sehemu ya kuishi Kigamboni, lakini nalala mjini, kwani kule ni mbali, siwezi kurudi kila siku. Sina uwezo wa kulipa nauli ya kunipeleka nyumbani, ninachopata ni kidogo, bora kuwatumia wajukuu kwa simu,” anasema Neema.

Anasema wanaouza mboga wakitumia baiskeli walibeba wateja wake wote, kwani ilimbidi yeye awe anawahi kuamka ili kufika mitaani, lakini wakati mwingine alishindwa kutokana na umri wake (hakutaka kuutaja), hivyo alijikuta akilaza mboga na kuharibika.

Hivyo aliamua kuacha biashara hiyo na kuingia mtaani kuomba nje ya misikiti na kwenye migahawa mikubwa.

Anasema pindi anapokutwa na askari wa jiji inabidi aondoke au kujikausha kama sio muombaji, na kuwa mara nyingi huwa wanakamatwa.

Anasema wanapokamatwa hushtakiwa kwa kosa la uzururaji na uzembe na wakikosa wadhamini hutupwa gerezani kwa miezi miwili hadi sita.

“Nina wajukuu naishi nao, nikipelekwa gerezani nikirudi nakuta na wao wameingia barabarani kuomba,” anasema.

Kama ilivyo kwa Rashida na Neema, wengi wa watu hao wasio na makazi hupata chakula kwa mamalishe au kwa kuomba kwenye misikiti mikubwa na migahawa.

Kuhusu Neema amesema wanaingia msikitini saa 11 alfajiri jirani na wanapolala, pia wakati mwingine wanatumia vyoo vya umma, ambako wanatozwa Sh500 kuoga na kubadilisha nguo zao.

Kila mmoja wa watu hao wanaolala nje, ana namna yake ya kupata kipato. Neema anasema anapopita kuomba kwa siku anaweza kupata Sh5,000 hadi Sh 10,000, huwa anawatumia wajukuu zake kwa ajili ya chakula na kwenda shule.

“Nikipata pesa nyingi kidogo narudi nyumbani kwangu, nikikosa kabisa au nikipata Sh4,000 nawarushia kwenye simu (wajukuu) watoe ili wale na mimi nabaki na kiasi kidogo kitakacho nisaidia,” anasema.

Anasema pesa wanazopata wakati mwingine wanagawana na polisi jamii wanaopita kwenye maduka mjini kuangalia hali ya usalama.

Wakati wakiwa kwenye maongezi na mwandishi wa gazeti hili, walitokea vijana waliovaa fulana zilizoandikwa Polisi Jamii mgongoni na kuwaamsha wanawake wote waliolala na kuwadai ‘ushuru’.

“Wewe mwanamke haya, muda huu fanya mpango… wewe fanya haraka bibi kama kawaida,” vijana hao wanasema.

Mwandishi alishuhudia wanawake hao wakitoa Sh500 kila mmoja na kuweka chini, huku mmoja wa vijana hao akiinana na kuokota ili isionekane kama wanakusanya pesa kutoka kwa watu hao wasio na makazi.

Mwandishi alipowauliza wanawake hao kwa nini wanatoa fedha, walisema wamekuwa wakiwanyanyasa kila siku na wakigoma wanamwaga maji kwenye maeneo wanayolala.

“Wanakuja kila siku kudai pesa, ukiuliza wanazipeleka wapi, wanasema wanatulinda, sasa tunajiuliza wanalinda nini wakati huwa tunaibiwa na vijana hapa, hadi kuna siku mlinzi wa eneo hili aliamua kutusaidia kuwakimbiza hao vibaka,” anasema Rashida.

‘Makazi’ Ubungo darajani

Upitapo eneo la Ubungo usiku, huwezi kukosa watu waliolala chini ya barabara za juu, kama vile ni makazi rasmi.

Mmoja wa wanaolala pembezoni mwa Daraja la Kijazi, ni Hamis Mohamed, anasema hali ngumu ya maisha ndiyo ilimfikisha hapo.

“Hapa tunalala kuanzia saa moja usiku. Kila mtu anakuja kwa wakati wake, lakini kuanzia saa sita tunakuwa wengi zaidi.

Anasema ukitaka kulala hapa lazima uwe na shuka maana mbu ni wengi, hasa wakati wa joto.

“Ila tumeshazoea, ndiyo maisha yetu. Tunaamka kuanzia saa mbili asubuhi na kuendelea, kila mtu anakwenda katika shughuli zake, hapa tupo mchanganyiko, kuna wengine wametoka mkoani wamekuja kutafuta maisha,” anasema.

Mohamed amesema wameshazoea mazingira hayo na wanaishi vizuri katika eneo hilo, ingawa kuna wakati wanakabiliana na changamoto za kupekuliwa na vibaka wanaopita katika eneo hilo.

Anasema baadhi ya wanaolala hapo wanafanya shughuli mbalimbali, ikiwemo kuuza maji na kukusanya chupa za plastiki.

Kwa mujibu wa Mohamed, katika eneo hilo wana eneo maalumu la kutundika mashuka wanayojifunika usiku, akisema ni nadra kuibiwa kutokana na mazingira na uaminifu waliojiwekea.

Alipoulizwa mahali wanapooga na kutunza mizigo yao, Mohamed anasema, “kuoga inategemea na mizunguko ya siku hiyo, mtu ukipata choo cha kulipia unaoga huko huko.

Simulizi nyingine inatolewa na Omary Ally, anayelala pembezoni mwa barabara ya mabasi yaendayo haraka eneo la Manzese Tip Top, anayesema changamoto za maisha ndizo zilizosababisha kufikia hatua hiyo, akisema bado wanaendelea kujitafuta ili kupata fedha za kupanga chumba.

“Nikiamka alfajiri nafanya shughuli mbalimbali za kupata fedha, ikiwemo kuokota chupa au shughuli nyingine, huwa sichagui kazi. Malengo yangu kupanga chumba, lakini uwezo mdogo, ndiyo maana umenikuta hapa,” anasema.

Ally anasema changamoto wanayokutana nayo ni pamoja na walevi wanaopita na kuwakanyaga na kukosakoswa na magari na pikipiki.

 “Kuna siku wakati nimelala pikipiki iliniangukia, nilichubuka kidogo sehemu za miguu, tukio lingine basi la mwendokasi liliacha njia, bahati nzuri lilikuwa mbali na eneo nilipolala, kuumwa mbavu na nimonia kutokana na baridi kali ni kawaida,” anasema Ally.

“Mvua ikinyesha tunapata wakati mgumu, tunakimbilia chini ya daraja au katika kituo cha mwendokasi kujificha,” alisema.

Mmoja wa walinzi katika maduka yaliyopo Manzese anasema hali wanazopitia watu hao ni ngumu, kwani kulala nje kunahitaji ujasiri wa hali ya juu.

“Tunawapa misaada kutokana na sadaka za watu, wakati mwingine kukiwa na misaada tunawaita na kuwapatia, lakini watoto wa mtaani wakijua tumetoa sadaka wanawavamia na kuwapora,” anasema.

Anasema hawezi kuwafukuza kwa kulala kwao nje ya msikiti, kwani kila mmoja na changamoto yake na akifukuzwa eneo hilo anaweza kukutana na matatizo makubwa hadi aliyemfukuza akajilaumu baadaye.

Naye dereva wa bajaji katika eneo la Manzese, John Martin alisema ingawa maisha ni magumu, watu wanaolala maeneo hayo wanahatarisha maisha kwa kukaa kwenye hifadhi ya barabara yanakopita magari ya kila aina.

“Hawa, chupa za maji na mikono ndiyo mito yao wakati wa kulala, hawaumii, wameshazoea ingawa wanahatarisha maisha yao,” anasema.

“Polisi huwa wanafanya doria za mara kwa mara za kuwakamata, lakini zinakuwa kama nguvu za soda kwa sababu baada ya siku tatu wanarejea tena kwa kishindo,” anasema.

Mmoja wa waendesha bodaboda wa maeneo ya darajani, Martin Joseph anasema siku za nyuma watu hao walikuwa wakilala katika Daraja la Kijazi, lakini wamepigwa marufuku wamekimbilia Manzese.

“Wengine wameishi Dar muda mrefu, lakini kuna wageni waliokuja kutafuta maisha na hawajafanikiwa, wamejikuta wanadondokea kulala nje. Hizi ni shida, hakuna anayependa kulala nje kama vile.”

Alipoulizwa kuhusu ustawi wa wananchi hao, Ofisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Dar es Salaam, Nyamara Elisha alimtaka mwandishi amtafute Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kwa kuwa suala hilo ni la kiusalama.

Chalamila alipotafutwa alisema atafutwe wakati mwingine, lakini wakuu wa wilaya za Ubungo na Ilala, Hassan Bomboko na Edward Mpogolo wamezungumzia tatizo hilo na mikakati iliyopo.

Bomboko alisema mara kwa mara wamekuwa wanafanya jitihada za kuwaondoa wakazi hao, lakini wamekuwa wanakaidi na kurejea.

“Ingawa wanarejea lakini programu ya kuwaondoa ni endelevu, kama tunavyowaondoa watoto kutoka mikoani, walioacha shule na kukimbilia Dar es Salaaam na kuweka makazi kwenye Daraja la Kijazi.

“Tunaendelea kutoa elimu ya kuhakikisha wanatafuta makazi kwa ajili ya usalama wao na wa watu wengine, maana baadhi yao wanakuwa vibaka,” alisema Bomboko.

Kwa upande wake, Mpogolo alisema Wilaya ya Ilala imekithiri kwa tatizo hilo kutokana na jiografia yake ya kuwa wilaya yenye biashara nyingi, majengo mengi na ofisi nyingi.

“Watu hawa wengi ni ombaomba ambao mbali ya kulala kwenye madaraja, hulala hadi misikitini na makanisani.

“Pia kuna wachache waliokuja kutafuta kazi, wanaofanya vibarua vya kutwa lakini hawana uwezo wa kupanga vyumba,” anasema Mpogolo.

Katika kulishughulikia hilo, anasema wamekuwa na kampeni za kuwarudisha walipotoka kwa kushirikiana na wilaya nyingine na mikoa wanakotoka, japo huwa wanarudi.

Pia anasema wamekuwa wakiwakusanya na kuwapa elimu ya ujasiriamali na namna ya kujitegemea badala ya kutegemea maisha ya kuomba.

“Hakuna mtu aliyezaliwa mtaani, hawa wote wanatoka kwenye majumba yetu, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuona namna gani wanawasaidia, ikiwemo kuwapa elimu, kuwa hata huko mjini wanapokwenda kutafuta maisha wawe na uhakika pia na sehemu za kuishi,” anasema Mpogolo.

Kuhusu usalama wao, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro anasema tatizo hilo ni kubwa.

“Tumefanya jitahada za kuwaondoa karibu mara nne, lakini wamekuwa wakirejea kulala katika eneo hilo.

“Wao wenyewe unaona wanaogopa hali ya hatari, kwa nini hawalali vichochoroni? Kwa nini wanalala sehemu wanayoona hawawezi kupigwa? Anahangaika lakini analala.

“Tumefanya jitihada za kuwaondoa karibu mara nne lakini wamekuwa wakirejea kulala katika eneo hilo. Tulishawatoa wakarudi, tangu enzi za Matonya (Paulo Anthony Mawezi- aliyekuwa ombaomba maarufu).

“Tulishawatoa wakarudi, zaidi ya mara nne,” anasema.

Imeandikwa na Bakari Kiango, Devotha Kihwelo na Nasra Abdallah.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts