Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema yeye ndiye aliyeanzisha ujenzi wa shule za sekondari za kata nchini, zikianzia wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, alikokuwa mbunge kwa mara ya kwanza kati ya mwaka 2000 hadi 2005.
Ujenzi wa shule hizo ulishika kasi katika awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete baada ya ongezeko la wanafunzi wanaongia kidato cha kwanza, huku shule zikiwa chache.
Akizungumza leo Julai 13, 2024 katika Kijiji cha Nshara, Hai mkoani Kilimanjaro, Mbowe amesema katika kipindi chake cha ubunge kwa mara ya kwanza alijenga shule 12 kabla ya mwaka 2005.
“Watu wa Hai mkumbuke historia. Wakati nakuwa Mbunge mwaka 2000 miaka 24 iliyopita, mimi ndiye mtu niliyewaza kujenga sekondari za kata katika nchi hii na mojawapo ya shule za kwanza kabisa ilikuwa Harambee.
“Kipindi kile tulijenga Harambee, tukajenga Tumo, Marumo, Losikita Lyamungo, tukajenga shule Bomang’ombe, tukajenga Hai sekondari, tukajenga Ukwasa kule Kwasadala, Kata ya masama Kusini, tukajenga shule ya Mtokashi Masama. Wakati huo Serikali ya CCM haijafikiria shule za kata, tumeshajenga shule 12 za kata jimbo la Hai kwa nguvu za wananchi,” amesema.
Amesema mwaka 2005 baada ya Serikali ya awamu ya nne kuingia iliendeleza ujenzi wa shule hizo nchi nzima.
Amewataka wananchi kutowaogopa viongozi wa Serikali, akisema ndiyo chanzo cha umasikini wa Watanzania.
“Siasa ni maisha yetu, viongozi wa kisiasa, awe Rais, waziri mkuu, awe makamu wa rais, awe mkuu wa mkoa, awe mkuu wa wilaya, awe wa kata, hao ni watumishi wetu.
“Ugomvi wangu na CCM ni kwamba mimi nimekataa woga. Ni bora nife nimesimama kuliko niishi nimepiga magoti, haki yangu nitaidai, iwe gerezani, iwe polisi iwe kaburini,” amesema.
Akizungumzia uchaguzi, Mbowe amelalamikia rafu katika uchaguzi, akisema chama hicho hakikutendewa haki katika uchaguzi wa mwaka 2020.
Amesema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 walishinda vizuri katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, lakini mwaka 2020 waliporwa ushindi wao.
“Kosa tulilotendewa watu wa Kilimanjaro, katika uchaguzi ule, katika wabunge tisa tulishinda wabunge saba, tukasomba madiwani wote katika halmashauri zote za Kilimanjaro ikiwemo halmashauri ya Wilaya ya Same.
“Katika majimbo saba ya Arusha tulisomba majimbo matano na halmsahauri zake, halmashauri ya Arumeru, Arusha Mjini, Karatu, Monduli, Longido, tuliwaachia halmahsuari moja na mbunge mmoja wa Ngorongoro,” amesema.
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Katibu wa Baraza la Wanawake wa Chadema, Catherine Ruge aliwataka wananchi wa kijiji hicho kujiandaa na uchaguzi kwa kuikataa CCM.
“Tunakwenda kwenye uchaguzi, tuendelee kukiunga mkono Chadema, tuhakikishe kwenye chaguzi serikali za mitaa tunawafukuza wenyeviti wa vijiji na vitongozi wa CCM.
Tukimaliza uchaguzi wa serikali za mitaa, tunakwenda kuwapa CCM likizo kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2025,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini wa chama hicho, Godbless Lema amewaonya vijana wanaoendesha pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda, akisema kazi hiyo imesababisha vifo na majeruhi, huku ikiwafunga kiuchumi.
“Vijana wa Kichaga mlikuwa mkimaliza darasa la saba, mkimaliza kidato cha nne na sita mlikuwa mnachukua mabegi mnakwenda mikoani, mlikuwa hamjui mtamkuta nani, leo kazi hizi zimewafunga, mmekuwa watumwa kwa ujira mdogo,” amesema.