Mapigano makali na mashambulizi ya mabomu yameripotiwa katika mji wa Gaza na maeneo mengine ya ardhi ya Wapalestina leo Ijumaa huku wapatanishi wakiendelea na juhudi za kusitisha vita vinavyoendelea. Shirika la ulinzi wa raia katika eneo linaloendeshwa na Hamas huko Gaza limesema kwamba takriban miili 40 imepatikana katika juhudi za awali kutafuta raia katika wilaya ya Tal al-Hawa na al-Sinaa.
Soma pia: UN yaonya kuhusu IDF kuwataka raia kuondoka Ukanda wa Gaza
Katika mazungumzo yanayoendelea kati ya Israel na Hamas na upatanishi kutoka Qatar, Misrina Marekani, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya vuguvugu la Kiislamu la Palestina, Hossam Badran amesema Hamas inapendekeza kuundwa kwa serikali huru ya watu wasioegemea upande wowote iongoze Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel baada ya vita.
Kulingana na afisa mmoja kwenye mazungumzo hayo ambaye hakutaka jina lake litajwe, serikali hiyo itasimamia masuala ya Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi katika awamu ya awali baada ya vita, kuandaa njia ya kabla ya uchaguzi mkuu.
Kauli hii inajiri baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuitaka Israel ibaki na udhibiti wa ukanda wa Philadelphi, eneo la Gaza kwenye mpaka na Misri. Hatua ambayo inakinzana na msimamo wa Hamas ambao wanasema Israel lazima iondoke katika eneo lote la Gaza.
Miili zaidi yapatikana
Shirika la ulinzi wa raia katika eneo linaloendeshwa na Hamas huko Gaza limesema kwamba takriban miili nyingine 40 imepatikana katika wilaya ya Tal al-Hawa na al-Sinaa baada ya wanajeshi wa Israel kumaliza mashambulizi yake.
Soma pia: Miili 60 yapatikana baada ya operesheni ya Israel
Aidha shirika hilo na wakaazi wamedokeza kuwa wanajeshi wa Israel wameondoka baada ya siku kadhaa za mapigano na wanamgambo wa Hamas hata hivyo jeshi la Israel halikuthibitishwa kuondoka kwao.
Tariq Ghanem, ni mkazi wa kitongoji cha Rimal katika Jiji la Gaza anasema, “Hali yetu ni ngumu kweli, watu wanakufa mitaani na kuna maiti zimekaa mitaani siku 4-5 au hata wiki hakuna wa kuziondoa, hakuna ulinzi wa raia, na iko wapi sheria ya kimataifa ya haki za binaadam? Shirika la Msalaba Mwekundu liko wapi ili kuokoa maisha ya waliojeruhiwa mitaani?“
Wanajeshi wa Israel na vifaru, baada ya kuvamia Shujaiya, wameingia katika wilaya nyingine za Mji wa Gaza, pamoja na makao makuu ya shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wapalestina UNRWA kupambana na wapiganaji wa Hamas na kundi la Islamic Jihad.
Siku ya Jumatano jeshi la Israel lilidondosha maelfu ya vipeperushi vikiwataka wakaazi wote wa Jiji la Gaza kukimbia “eneo hatari la mapigano” eneo ambalo Umoja wa Mataifa unasema hadi watu 350,000 walikuwa wakiishi.