Na Elizabeth Zaya, Dar es Salaam
MKUU wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, amesema wamejipanga kuwasaidia wajasiriamali katika wilaya hiyo ili wafanye biashara za viwango vya juu.
Magoti alitoa kauli hiyo jana alipotembelea maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam(DITF) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Temeke.
Alisema Kisarawe ni miongoni mwa Wilaya yenye bidhaa nyingi hivyo ni vema kutumia wajasiriamali hao ambao wamekuwa wakiendesha biashara kupitia bidhaa hizo kuwainua na kuzitangaza zaidi.
“Kisarawe ni moja ya wilaya inayotengeneza bidhaa nyingi ikiwamo wine inayoitwa Chole, tunatengeneza kwa kutumia mabibo, tuna Zabibu na Korosho ambayo inavitamini yote, kwa hiyo sisi kama viongozi wa wilaya hii, tumejipanga kuwasapoti wajasiliamali ili wafanye biashara kufikia ngazi ya juu,”alisema Magoti.
“Kama Rais Samia Suluhu Hassan alivyoagiza kwamba wajasiriamali wapate maeneo maalum ya kufanyia biashara zao, na sisi viongozi wa wilaya hii tuliona tuje kuangalia na kujifunza kutoka kwenye mikoa mbalimbali ndani na nje ya nchi wanaoshiriki kwenye maonesho haya ili tukirudi tuweke mipango mizuri ya kuwasaidia wajasiriamali wa wilaya hii”
Kuhusu maonesho ya mwaka huu, Magoti alisema kuna mabadiliko makubwa katika kila eneo kwenye maonesho hayo.
“Kadri siku zinavyokwenda maonesho yanazidi kuwa makubwa na mazuri na mataifa mengi yanazidi kushiriki, tunaamini kwamba zile changamoto ndogondogo zitazidi kupungua na uwezeshwaji wa wananchi wengi kushiriki utazidi kuongezeka,”alisema Magoti.