UKIMUONA nje ya kazi unaweza kumdharau, lakini ukija kazini kwake utapata stori ya namna anavyosifika kwa uchezaji uwanjani.
Noela Uwandameno (22), ambaye ni mchezaji wa Vijana Queens na mwanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere anasimulia namna alivyoingia kwenye mpira wa kikapu na anavyojigawa pia kwenye masomo.
“Ni miaka saba sasa tangu nianze kucheza mpira wa kikapu lakini nilianza kama mas-hara tu mimi kabla ya kucheza hivyo nilikuwa mchezaji wa volleyball na siku hiyo nilienda Ukonga kwa ajili ya kufanya mazoezi,” anasema Noela.
“Lakini sikuwakuta wenzangu nikawaona watu wanacheza kikapu ikabidi na mimi niunge sikuwa naujua lakini kwa sababu ni mchezaji wa volleyball na wengi wanajua kukimbia vizuri nikaambiwa najua nifanye mazoezi ndipo hapo nilipoanzia.
“Mwaka 2014 Ukonga wakanitaka nichezee timu yao wakati huo nimemaliza darasa la saba. Nikacheza hadi 2022 nikaacha na kujiunga na Vijana Queens ambayo nachezea hadi sasa.”
Anasema kutokana na kuupenda mchezo huo ilibidi aweke mzani sawa yaani kuhakikisha anatokea chuo na kazini ili acheze vizuri.
Noela anachukua kozi ya rasilimali watu na utawala akiwa mwaka wa pili chuoni.
Anasema aliamua kuchagua elimu na kutupilia mbali pesa kwa sababu elimu itampa manufaa ya baadaye tofauti na kipaji.
“Nilijiunga na Vijana na nikawaambia pesa ya mshahara msinipatie, nisaidieni ufadhili wa masomo kuanzia mwanzo hadi namaliza, hivyo nalipiwa kila kitu na kwa wakati.
“Kwanini nimechagua elimu kwanza kiwango changu kinaweza kushuka muda wowote na siwezi kucheza siku zote lakini elimu inaweza kunisaidia kupata ajira na kupiga pesa zaidi,” anasema.
Noela anasema amebeba tuzo mbalimbali kwenye mashindano tofauti, lakini anayoyakumbuka zaidi ni yale ya Taifa. “Kiukweli labda nikazihesabu (tuzo) moja moja, lakini ninavyokumbuka nina zaidi ya tuzo 10 za mchezaji bora wa mwaka (MVP) na nimekuwa nikichukua mfululizo,” anasema mchezaji huyo ambaye ni kiraka, akiwa na uwezo wa kucheza popote.
“Huku MVP anapewa kiasi cha Sh600,000 ukipiga hesabu nina jumla ya milioni sita ambayo pesa hizo zimenisaidia vitu vingi.”
Mchezaji huyo anasema anapenda kuvaa mitindo mbalimbali ya nywele na mavazi ambayo humuweka nadhifu na kuonekana vizuri.
“Wengi wananiambia kuwa ni mwanamitindo mzuri na nikiitumia fursa hiyo inaweza kunisaidia kupata matangazo mbalimbali ya urembo na kuwa mtu mkubwa baadaye,” anasema.
Noela pia ni mfuatiliaji wa soka na kwa sasa anakoshwa na staa mpya wa Yanga, Clatous Chama aliyetua hivi karibuni kikosini hapo akitokea Simba.
Anasema alikuwa anampenda sana mchezaji huyo wakati akiitumikia Simba ambayo yeye ni shabiki lialia. Kutokana na mapenzi aliyo nayo kwa Chama, anasema mashabiki wa kikapu pia wanapenda kumuita Chama kutokana na aina yake ya uchezaji akichezesha timu, kukaba, kushambulia na kufunga.
“Nafasi ninayocheza kwenye kikapu inaweza kufanana na Chama ingawa ni michezo tofauti. Siyo mara ya kwanza watu kuniita hivyo wakinifananisha na Chama,” anasema Noela
Mchezaji huyo anasema mchezo wa kikapu umemlipa kwa kiasi japo si kikubwa, lakini anachojivunia ni umaarufu ambao umemfanya ajulikane na kutambulika sehemu mbalimbali.
“Chuo kuna watu hawanijui, lakini kupitia kikapu wananiona kwenye TV kupitia mashindano mbalimbali na wanawaambia hadi wazazi wangu mwanao tumemuona,” anasema.
Nje na kujulikana, Noela anasema mafanikio mengine ni kununua baadhi ya vitu kama simu, TV na friji ambavyo akiviangalia ndani anajivunia kipaji chake.
Mjini ukiwa na kipaji umetoboa ni wewe mwenyewe tu utakavyojiweka. Ndivyo anavyoweza kusema binti huyo ambaye nje ya kucheza kikapu ni mtaalamu wa netibali na hapa anaeleza anavyopiga pesa upande huo. “Kuna ndondo za netibali ambazo nazo nikisikia kuna bonanza sehemu fulani nachangamkia fursa na hapo inategemea mnacheza siku ngapi. Kama mbili au wiki unalipwa kulingana na kiwango cha aliyeandaa, lakini ni pesa nyingi.
“Mabonanza mengine unakuta kwa wiki Sh300,000 au mengine 800,000. kKwa hiyo unaweza kujikuta yamechanganya umetoka sehemu laki nane unapiga tena sehemu nyingine,” anasema.
Noela anawataja wachezaji watatu bora anaopenda namna wanavyocheza akianza na Tukusubila Mwalusamba kutoka Tausi Royal ambaye anasema akiwa uwanjani ni mchezaji kiongozi na anajua namna ya kuendana na kila mchezaji. “Ukiachana na huyo kuna Jesca Lenga anaichezea DB Tronkanti anayecheza nafasi moja na mimi na natamani siku moja nije kucheza naye. Anajua sana, kwa nje yupo Natalia wa Kenya,” anasema.