Aliyewahi kuwa kigogo wa  CCM Dodoma arejea CUF 

Dodoma. Kada na aliyewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Othman Dunga amekihama chama hicho na kwenda Chama cha CUF, akieleza nia yake ya kugombea ubunge wa jimbo la Kondoa Mjini katika uchaguzi wa mkuu wa mwaka 2025.

Dunga ni mwenye historia ndefu kisiasa aliyeanzia upinzani kwenye chama cha CUF, lakini miaka 18 iliyopita alikihama chama hicho na kujiunga na CCM.

Akizungumza juzi jioni wilayani Kondoa wakati wa mkutano wa kupokelewa kwenye chama cha CUF, Dunga ambaye amewahi kuwa katibu wa CCM Msaidizi wa Mkoa wa Dodoma (masuala ya siasa) na Katibu wa CCM Wilaya ya Hanang mkoani Manyara, amesema baada ya siku mbili za kuhamia CCM, aliteuliwa kuwa katibu wa wilaya wa chama hicho.

“Nimejifunza mengi sana. Nimejifunza mambo mbalimbali na udanganyifu, halafu wewe uko Kondoa unashusha bendera za CUF. Sasa wewe kama kiongozi wako amejiunga na CUF unanuna kwa nini?” amehoji Dunga ambaye mwaka 2020 alitia nia kugombea ubunge katika jimbo la Kondoa Mjini kwa tiketi ya CCM, lakini hakuteuliwa na chama hicho.

Akiwa katibu wa Wilaya ya Hanang, Dunga pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Hanang, George Bajuta na aliyekuwa Mbunge wa Hanang, Dk Mary Nagu,waliwahi kufikishwa polisi baada ya kutokea vurugu.

Vurugu zilielezwa kusababishwa na harakati za upangaji wa safu za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 zilitokea katika kikao cha kamati ya siasa.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mjini Kondoa, Dunga amesema amehama CCM kwa sababu ni chama cha wenye fedha, akidai kuwa huwezi kuwa kiongozi ndani ya chama hicho kama huna fedha na badala yake utakuwa mpiga kura daima wa kuchagua viongozi.

“Lakini mtoto wa mkulima na masikini hana nafasi ya kuwa kiongozi, kumejaa. CCM ni sawa na kaa, kuna samaki kule Pwani anaitwa kaa, wale samaki ukiwa kwenye kapu wakiwa hai wana kawaida ya kutaka kutoka katika kapu lakini kila samaki mmoja anapotaka kutoka anavutwa na wenzake na mwenzake anapanda juu, hakuna anayetoka wanavutana wao kwa wao. Ndivyo walivyo CCM,” amesema.

Amesema kamati ya siasa ya chama hicho katika Wilaya ya Kondoa imejaa wajumbe kutoka ukoo mmoja na kuwa kuna watu ambao wanakwenda kugombea ubunge Kondoa Mjini, ambao wamekuwa wakiparurana kama si wa chama kimoja.

Akimpokea, Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema chama chake kinafanya siasa za kistaarabu kwa kujenga hoja zinazowapa matumaini Watanzania.

“Tunapojenga hoja tunawapa matumaini Watanzania kuwa mabadiliko yanaweza kujitokeza sasa wapambe wa CCM wakiungwa mkono na vyombo vya dola wakashusha bendera hao hawamtakii mema Rais, wanataka yale yanayotokea Kenya yahamie Tanzania,” amesema.

Amesema wanapojenga hoja wanatoa matumaini kwa Watanzania kuwa wanaweza kuleta mabadiliko kwa njia ya amani na kuwa watakapoamini kuwa mabadiliko yanaweza kuletwa kwa njia ya amani wanakuwa na subira.

‘’Na nchi yetu asilimia karibia 80 ni vijana wa chini ya 35, wengine unaowaona ukawaamkia ukadhani kuwa ni wazee kumbe ni bakora za CCM zimewacharaza wakawa hoi bini taabani. Ukampa shikamoo kumbe hali ya maisha lakini wengi ni vijana,” amesema.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan alileta R nne za maridhiano, ustahimilivu, ujenzi mpya wananchi na hivyo ni vyema wanachama wake wakawa na nidhamu.

Katibu Mkuu wa CUF, Hamad Masoud amesema ni imani yao kuwa mambo yaliyotokea mwaka 2019 katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji, vitongoji pamoja na uchaguzi mkuu wa 2020, hayatajitokeza katika uchaguzi utakaofanyika mwaka huu na mwakani.

“Nchi bila haki hakuna amani …Tunataka uchaguzi wa haki. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo juzi tuliongeza neno moja huru lakini nasema jina lisiwashughulishe mambo ni yaleyale. Maana yake yale yaliyofanyika mwaka 2020 ndiyo yanaweza kufanyika tena. Tujipange ipigwavyo ndivyo ichezwavyo,” amesema.

Amesema  majimbo ya Kondoa Vijijini na Mjini ni ya CUF kutokana  na kuwapo kwa  wanachama wengi kwenye majimbo hayo.

Akijibu hoja za Dunga,  Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kondoa, Hija Suru amesema maneno aliyosema Dunga   ni uongo.

“Walipata hasira kwani matarajio yao hayakufikia, hayo ni maneno ya mkosaji, walete ushahidi wa maneno yao waliyoyasema,” amesema.

Suru amesema katika mkutano huo walilenga kupata watu wengi lakini kwa kufanya mkutano Ijumaa wakati ni siku ya soko ni vigumu kuwapata watu.

“Watu waliwapuuza hawakuacha shughuli zao kwa ajili yao. Ukizingatia walitangaza wilaya nzima magari ya matangazo yalipita watu walikuwa kazini kutafuta maisha,” amesema.

Related Posts