UKISIKIA mtego ndio huu uliofanywa na mabilionea wa Simba na Yanga. Ndio, Yanga imesajili majembe ya maana kwa gharama kubwa ili kuimarisha kikosi. Bilionea Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ kupitia uongozi wa klabu hiyo, amemsajili Clatous Chama kutoka Simba, amemvuta Prince Dube kutoka Azam kwa gharama kubwa. Amemleta Chadrak Boka kutoka DR Congo. Amembakisha Stephane Aziz KI aliyemaliza mkataba. Bado kuna Aziz Andambwile, Jean Baleke na Abubakar Khomeiny. Juzi kati ikamtambulisha Duke Abuya kutoka Singida BS.
Turudi upande wa pili, yaani kule Msimbazi nako hakujapoa. Bilionea Mohammed ‘Mo’ Dewji baada ya kuona misimu mitatu mfululizo timu ikihenyeka kusaka ubingwa bila mafanikio, fasta amejitosa kujenga Simba mpya. Mwenyewe amesimamia usajili. Mo Dewji ameshusha nyota wapya 13. Joshua Mutale kutoka Zambia. Debora Mavambo na Valentin Nouma kutoka DR Congo. Kuna Steven Mukwala kutoka Uganda. Pia kuna Jean Charles Ahoua, Chamou Karaboue na Augustine Okajepha.
Kuna nyota wa kizawa, Omary Omary, Kelvin Kijili, Valentino Mashaka, Abdulrazak Hamza, Yusuf Kagoma, huku ikielezwa Awesu Awesu badio kutangazwa tu kwa sasa, lakini naye pia ni mnyama kutoka KMC.
Mo Dewji alienda mbali zaidi kwa kuamua kushusha benchi nzima la ufundi kutoka Afrika Kusini kwa kumleta Fadlu Davids kama kocha mkuu na wasaidizi DarianWilken, Wayne Sandilands, Riedoh Berdien na Mueez Kajee wanaungana na mzawa, Seleman Matola aliyekuwapo kwa misimu kadhaa klabuni hapo.
Hatua ya mabilionea hao wa Simba na Yanga kuamua kujitosa wenyewe kuimarisha vikosi hivyo kwa msimu ujao wa mashindano umeonekana ni kama mtego kwa makocha, Fadlu na Miguel Gamondi aliyeiwezesha Yanga msimu uliopita kutetea mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho kwa mara tatu mfululizo.
GSM na Mo ni kama wamewachonganisha makocha wa timu hizo na hasa baada ya kuelezwa kila mmoja wamewapa malengo yenye kufanana kwa Fadlu na Gamondi kwa ajili ya msimu ujao wa 2024-2025.
Fadlu aliyejichimbia na kikosi cha Simba kambini jijini Ismailia, Misri kujiandaa na msimu huo ndio kwanza amechukua mikoba iliyoachwa na Abdelhak Benchikha aliyeachana na timu hiyo Aprili mwaka huu, lakini kwa Gamondi yeye yupo na timu kambini maeneo ya Kigamboni pale Avic Town, jijini Dar es Salaam.
Katika misimu mitatu iliyopita ambayo Yanga imetawala kwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA mfululizo, imekuwa ikiweka kambi Avic Town, wakati watani zao wa jadi wakienda nje ya nchi.
Ni kama Yanga wameshtukia kwamba pale Avic Town ndiyo sehemu sahihi kwao zaidi kujiandaa na msimu mpya kwani kumewapa matunda mazuri ikiwemo kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2022-2023 kwa mara ya kwanza sambamba na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2023-2024.
Taarifa ikufikie kwamba, baada ya kumalizika kwa msimu uliopita 2023-2024 na Yanga kuendelea kutawala tena soka la Bongo huku Simba ikiporomoka, mabosi wa timu hizo wamekuja na mikakati mingine msimu ujao.
Kuondoka kwa Benchikha, Simba iliwalazimu kumpa kibaryua cha muda kocha mzawa, Juma Mgunda, ili kumalizia msimu akisaidiana na Matola, timu ikamaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara na kukata tiketi ya Kombe la Shirikisho ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki michuano hiyo moja kwa moja tangu 2018.
Ujio wa Fadlu na namna kikosi hicho kilivyosukwa upya, matumaini ya viongozi wa Simba akiwemo Mo Dewji ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi na rais wa heshima wa klabu hiyo ni kupindua utawala wa Yanga.
Lakini maboresho ya kikosi cha Yanga yaliyofanywa na uongozi chini ya rais Hersi Said akipewa nguvu na mfadhili wa klabu hiyo, Gharib Mohamed Said (GSM) ni wazi unaleta uchonganishi kwa makocha wa timu hizo.
Malengo yaliyowekwa endapo yasipofikiwa kuna hatari ya makocha hao kuweka rehani vibarua vyao, kwani imekuwa kawaida kushuhudia hilo likitokea.
Msimu uliopita tulishuhudia Simba ikibadilisha benchi la ufundi mara mbili, hiyo yote ni kutaka kuweka mambo sawa baada ya kuonekana kuna tatizo.
Kocha Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ licha ya kuipa timu hiyo, Ngao ya Jamii kwa kuifunga Yanga kwa penalti 3-1 mwanzoni mwa msimu pale jijini Tanga, lakini safari yake iliishia pale alipopokea kichapo cha mabao 5-1 kutoka kwa Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Novemba 5 mwaka jana.
Benchikha naye safari yake ilihitimishwa na Yanga baada ya kufungwa mabao 2-1 katika Ligi Kuu Bara, kumbuka kocha huyo raia wa Algeria alitambulishwa kikosini hapo Novemba 2023, akaondoka Aprili 2024. Alidumu kwa takribani miezi mitano akiwapa Kombe la Muungano aliloshinda kule Zanzibar.
Hapa ndiyo kwenye uchonganishi wenyewe kwani mabosi wa timu hizo kila mmoja anataka kuona msimu ujao mataji yanaingia kabatini kwao.
Yanga wana kazi kubwa ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA), wakati Simba wenyewe wanapaswa kulitetea taji lao la Ngao ya Jamii.
Msimu uliopita, Yanga ililipoteza taji la Ngao ya Jamii lililokwenda kwa Simba, safari hii wamepania kulirudisha.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe amesema cha kwanza walichopanga msimu ujao ni kuanza kurudisha taji la Ngao ya Jamii kutoka kwa Simba.
“Msimu uliopita tulitetea mataji yetu ya Ligi Kuu na Kombe la FA, lakini tulishindwa kufanya hivyo Ngao ya Jamii. Msimu ujao malengo ni kubeba mataji yote hayo ikiwemo kulirudisha Ngao ya Jamii.
“Hayo yanawezekana kwa sababu ukiangalia namna kikosi kilivyoboreshwa na malengo ya klabu yalivyo, hakuna kinachoshindikana kabisa,” alisema.
Wakati Yanga hesabu zikiwa hivyo, Simba nao wanataka kutetea taji la Ngao ya Jamii.
“Baada ya mateso ya misimu mitatu sasa Wanasimba tunakwenda kufurahi msimu ujao kwa kubeba mataji ambayo tuliyapoteza. Tutaanza na Ngao ya Jamii kutetea taji letu, kisha hayo mengine yatafuata ambayo yapo kwa mtani.
“Usajili tulioufanya ni wa kimkakati zaidi, ukiangalia vijana walioingia wana uchu wa mafanikio hivyo wapinzani wajiandae,” alisema Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally.
Majibu ya nani zaidi kati ya wawili hao tutayapata Agosti 8, mwaka huu pale timu hizo zitakapovaana katika mchezo wa Ngao ya Jamii hatua ya nusu fainali.
Ngao ya Jamii itahusisha timu zilizomaliza nafasi nne za juu katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita ambazo ni Yanga, Azam, Simba na Coastal Union.
Mabingwa Yanga watacheza dhidi ya Simba iliyoshika nafasi ya tatu, kisha Azam iliyokuwa ya pili itapambana na Coastal iliyomaliza wa nne.
Washindi wa mechi hizo za nusu fainali watakutana fainali, huku waliopoteza wakiwania nafasi ya tatu na nne.
Ni wazi katika malengo ya kuanza kubeba mataji waliyowekewa makocha wa Simba na Yanga, hapo tutashuhudia mmoja lazima apoteze na kuweka rehani kibarua chake kama huko mbele ya safari mambo yakizidi kwenda vibaya.
Simba kwa kumaliza nafasi ya tatu kwenye ligi msimu uliopita, watashiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao ambapo katika droo ya michuano hiyo iliyochezeshwa, watamsubiri mshindi wa hatua ya awali kati ya Uhamiaji ya Zanzibar na bingwa wa Kombe la FA kutoka Libya ambaye bado hajapatikana.
Taarifa kutoka katika kambi ya Simba iliyopo nchini Misri, zinabainisha kwamba kikosi hicho kabla ya kuondoka jijini Dar es Salaam, kulikuwa na kikao kizito cha kupeana maagizo ya nini kinatakiwa kufanyika kuelekea msimu ujao.
Kikao hicho kilichoongozwa na Mo Dewji, kilikuwa na mambo mengi lakini kubwa zaidi Kocha wao mpya Fadlu Davids na wasaidizi wake walibebeshwa malengo ya klabu hiyo kwa msimu ujao ni kwamba tajiri wao analitaka Kombe la Shirikisho Afrika, Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Ngao ya Jamii.
Kama sio kubeba kombe hilo la Shirikisho, basi kikosi hicho kinatakiwa kwa uchache kitinge fainali ili kutuliza presha ya mashabiki.
Ikumbukwe kwamba, Simba katika misimu sita iliyopita imefanikiwa kucheza robo fainali tano za michuano ya CAF, nne Ligi ya Mabingwa na moja Kombe la Shirikisho, huku malengo ya kutinga nusu fainali yakifeli.
Sasa basi, kwa kuwa msimu ujao timu hiyo imeangukia Kombe la Shirikisho, malengo yameongezeka wakitakiwa kufika fainali kama walivyofanya Yanga msimu wa 2022-2023 na ikiwezekana kubeba kabisa ubingwa kwani mabosi wanaamini inawezekana ndiyo maana wameshusha majembe yaliyohitajika kikosini.
Gamondi yeye ameambiwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika, ahakikishe timu inacheza nusu fainali baada ya msimu uliopita kuishia robo fainali ikiwa ni hatua kubwa zaidi kwao kupiga kwa mara ya kwanza.
Yanga itaanzia ugenini hatua ya awali kwa kucheza dhidi ya Vital’O ya Burundi kisha marudiano nyumbani, endapo ikivuka hatua hiyo, itakwenda kucheza na mshindi kati ya SC Villa ya Uganda na Commercial Bank ya Ethiopia kuwania nafasi ya kutinga makundi.
Yanga katika kuimarisha kikosi chao, wameingia sokoni na kushusha majembe mapya ambayo wanaamini yanakwenda kuwapa kile wanachokitaka. Katika hilo wameenda tena Simba kuchomoa kifaa kama walivyofanya msimu uliopita walipombeba Jonas Mkude.
Safari hii Yanga imemchomoa Clatous Chama ambaye alifanya makubwa ndani ya Simba tangu msimu wa 2018-2019 hadi 2023-2024 mkataba wake ulipomalizika na kuamua kuondoka.
Hakuna asiyefahamu nini Chama amekifanya ndani ya Simba kwani akiwa na kikosi hicho ameshinda mataji matatu ya Ligi Kuu Bara na Kombe la FA mara mbili, huku pia akichangia ushiriki wa hatua ya robo fainali ya michuano ya kimataifa mara tano katika misimu sita iliyopita.
Mbali na Chama, Yanga imemsajili Prince Dube ambaye aliitumikia Azam kuanzia 2020 hadi 2024. Mwingine ni Chadrack Boka kutoka FC Lupopo ya DR Congo, Aziz Andambwile (Singida Fountain Gate), Khumeiny Aboubakar na Duke Abuya ambao wote msimu uliopita waliitumikia Ihefu ambayo hivi sasa inaitwa Singida Black Stars.
Yanga pia imepambana kuwabakisha wachezaji waliokuwa bado katika mipango ya benchi la ufundi la timu hiyo ambao ni Aboutwalib Mshery, Djigui Diarra, Kibwana Shomari, Nickson Kibabage, Bakari Mwamnyeto, Farid Mussa na Stephane Aziz Ki ambaye ishu yake iliteka hisia za wengi.
Aziz Ki mkataba wake wa miaka miwili aliosaini wakati anatua kikosini hapo mwanzoni mwa msimu wa 2022-2023, ulimalizika Juni 30, 2024, hivyo klabu mbalimbali zikatajwa kuwania saini yake ikiwemo Mamelodi Sundowns, CR Belouzidad, Wydad Casablanca, Al Ahly na Raja Casablanca, lakini akabaki kikosini hapo kwa miaka miwili mingine.
Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amezungumzia maboresho ya kikosi akisema: “Malengo ni kuunda timu ya kutikisa Afrika. Hilo nimeliona linakwenda kutimia kutokana na namna kikosi kilivyofanyiwa maboresho ya kuingiza wachezaji wapya na wale wa zamani kuboreshewa mikataba yao.”