Samia azindua makao makuu ya Jeshi la Polisi Katavi

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amezindua jengo jipya la Makao Makuu ya Jeshi la Polisi mkoani Katavi lililogharimu Sh1.4 bilioni, huku akiagiza litunzwe ili lidumu.

Samia amefungua jengo hilo leo, Jumapili ya Julai 14, 2024 ikiwa ni siku ya pili ya mwendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani humo aliyoianza Julai 12 na atahitimisha Julai 15.

Jengo hilo lililopo katika eneo lenye mita za mraba 1,438 likiwa na ghorofa tatu.

Samia amesema kuwa na jengo ni hatua ya kwanza na utendaji kazi ni hatua ya pili, ambayo inapaswa kuzingatiwa huku ikienda sambamba na utunzaji ili liendelee kuwa zuri miaka yote.

Amesema jengo hilo ni moja ya hatua ya kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi kwa askari ikiwa ni pendekezo la Tume ya Haki Jinai.

“Lakini ninachokitaka, jengo hili lisomane na taasisi nyingine za Jeshi la Polisi zilizopo mkoani humu, nafikiri kazi hii IGP utaenda kuitekeleza,” amesema Samia.

Amesema mbali na ujenzi wa jengo hilo pia ipo kazi ya kuboresha vituo vya polisi nchini ambayo imeanza maeneo mbalimbali, ikiwa ni utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai  na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Rais Samia pia alitumia nafasi hiyo kuwaasa wananchi kutunza amani ya nchi kwani kadri mkoa huo unavyozidi kufunguliwa, kutakuwa na mchanganyiko wa watu kutoka ndani na nje ya nchi.

Awali, akitoa maelezo kabla ya kuzinduliwa kwa jengo hilo, Mkaguzi wa Polisi ambaye pia ni mkadiriaji wa majengo, Aisha Tuwa amesema jengo hilo lina ofisi 33 vyumba viwili vya silaha na kumbi mbili za mikutano. Sakafu ya kwanza ina vyumba 11 vinavyojumuisha ofisi za mapokezi, ofisi ya usalama barabarani na ofisi ya kikosi cha kutuliza ghasia.

“Sakafu ya pili ina vyumba 10 ikijumuisha ofisi za kamanda wa polisi mkoa wa Katavi na ukumbi wa mikutano huku sakafu ya tatu ikiwa na vyumba sita, ikijumuisha ofisi za kamanda wa upelelezi na ukumbi mkubwa wa mikutano huku sakafu ya nne ikiwa na Ofisi sita ikiwemo ofisi za Tehama na inteligensia za mkoa,” amesema Tuwa.

Akitoa maelezo juu ya ulinzi wa jengo hilo, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi na Mhandisi wa mawasiliano, Mussa Kudaba amesema jengo hilo lina kamera 15 kwa ajili ya kurahisisha ulinzi wa jengo ndani ya saa 24, huku askari watakuwa wakiangalia mwenendo ndani ya jengo.

“Jengo hilo litasaidia kutoa huduma bora kwa jamii, kwani kamera hizo zinachukua picha, video na sauti, hii itasaidia ufuatiliaji wa utoaji huduma kwa raia kutoka kwa askari wao, pindi kunapokuwa na malalamiko tutatumia ushahidi wa picha hizi,” amesema Kudaba.

Related Posts