Mwanza. Wananchi katika Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wameiomba Serikali kuharakisha malipo ya ujenzi wa vivuko vya Kome III na Kivuko cha Buyangu Mbalika ili vikamilike na kutoa huduma kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Julai 12, 2024 baada ya viongozi na wananchi waliotembelea maendeleo ya ujenzi wa vivuko vinavyotengenezwa na Kampuni ya Songoro Marine ya jijini Mwanza.
Mkazi wa Sengerema, Nicholaus Erasto amesema vivuko hivi ni muhimu vikamilike kwa wakati ili kuwaepusha wananchi kutumia mitimbwi ambayo siyo salama kwa usafari.
Amesema kutokana na changamoto ya usafari kwenda Mbalika wilayani Misungwi, wakazi wa kata ya Buyagu wanatumia usafiri wa mitumbwi ambao unahatarisha maisha yao, hivyo ukamilishaji wa vivuko hivi utarahisisha suala la usafiri.
Awali, akitoa maelezo ya ujenzi wa vivuko hivyo, mratibu msimamizi wa mradi huo kutoka Songoro Marine, Isakwisa Samweli amesema kucheleweshwa kwa vivuko hivi kumetokana na Serikali kudaiwa Sh11 bilioni ambazo kama zingelipwa kwa wakati, vivuko hivyo vingekuwa vimekamilika na kutoa huduma kwa wananchi.
Amesema Kampuni ya Songoro Marine kwa sasa inajenga vivuko vipya vitano na kufanya ukarabati wa vivuko vingine kwa zaidi ya Sh26 bilioni.
Baadhi ya vivuko hivyo ni Kome III kitakachotoa huduma kati ya Nyakaliro na Kome chenye thamani ya Sh8 bilioni na kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 22 kwa wakati mmoja na kivuko cha Buyagu Mbalika chenye thamani ya Sh3 bilioni kina uwezo wa kubeba abiria 100 na magari sita kwa wakati mmoja.
Kivuko cha Kome III kimefikia asilimia 75 na kivuko cha Buyagu Mbalika kimefikia asilimia 75 ambapo vyote vitakamilika na kukabidhiwa serikalini mwishoni mwa mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema Serikali itahakikisha inalipa fedha hizo kwa haraka ili ziwasaidie kukamilisha ujenzi wa vivuko hivyo.
“Nimetembelea karakana hii na kujionea hali ya ujenzi wa vivuko hivi, Serikali itahakikisha fedha zinalipwa kwa wakati ili zitekeleze ujenzi wa vivuko hivyo,” amesema Mtanda.
Mbunge wa Sengerema (CCM), Hamis Tabasamu aliyeambatana na wananchi wao kuangalia ujenzi wa vivuko hivyo, amesema kutokana na kasi ya ujenzi huo unavyoendelea, wananchi wa Sengerema na Buchosa watavitumia vivuko hivyo.
Amewataka wananchi wa Sengerema kuepuka maneno yanayokatisha tamaa kutoka kwa baadhi ya watu wakisema vivuko hivyo havipo huku vipo vinajengwa.