Na Mwandishi Wetu
Tangu juni 28, 2024 Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) iliweka kambi katika viwanja vya Mwl.Julius Nyerere na kushiriki Maonesho ya 48 ya Biashabara ya Kimataifa Dar es Salaam maarufu Sabasaba yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania TanTrade kila ifikapo tarehe 28 Juni hadi 13 Juni ya kila mwaka.
Kwa kutambua fursa hii, TGDC iliweza kutoa elimu kwa wananchi na wageni mbalimbali wakiwemo viongozi waandamizi wa Serikali waliotembelea maonesho haya.
Miongoni mwa viongozi waliofika katika banda la TGDC ni Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alionesha kufurahishwa na hatua iliyofikiwa katika utafutaji wa nishati jadidifu ya jotoardhi.
Mhe.Kikwete alienda mbali zaidi na kusema banda la TGDC limemkumbusha namna alivyoenda nchini Kenya kujionea mradi wa Jotoardhi wa Olkaria wakati wa hatua za mwanzo za utafutaji nishati hiyo.
Pamoja naye, TGDC ilitembelewa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felschesmi Mramba ambaye yeye kwa upande wake alishauri kuwa ni vyema kwa kampuni kuongeza juhudi na kutumia njia rahisi zaidi za kuipata nishati ya umeme wa jotoardhi ili uingie kwenye gridi ya taifa pamoja na mambo mengine uchochee na kukuza uwekezaji na uchumi kwa ujumla.
Aidha, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mhandisi Innocent Luoga alifurahishwa na hatua zilizofikiwa na kushauri kuwa ni vyema kwa kampuni kuongeza juhudi na kutumia maonesho haya kutafuta wawekezaji zaidi ili waje kuwekeza na kuhakikisha umeme wa jotoardhi unapatikana.
Vilevile, Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt.Lucy Mboma aliipongeza TGDC alipotembelea banda lake na kupata elimu juu ya maendeleo ya upatikanaji wa nishati ya jotoardhi ambapo alielezwa kuwa kwa sasa kampuni inaendelea na miradi yake mitano ya kipaumbele hususan mradi wa Ngozi (megawati 70) ambao upo katika hatua ya uhakiki ili baadaye ufikie hatua ya uzalishaji unaotarajiwa kuanza na megawati 30.
Wageni wengine waliotembelea banda la TGDC ni pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Bw.Halfan Halfan pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo ya PURA Mhandisi Charles Sangweni ambao walionesha shauku yakuwa ipo haja TGDC na PURA kuendeleza mashirikiano katika utendaji kutokana na shughuli zao kuingiliana ambapo kwa kufanya hivyo itaongeza tija kiutendaji na kuleta matokeo kwa haraka.
Wanafunzi na wananchi pia walikuwa ni sehemu ya waliotembelea banda la TGDC ambapo wapo waliosema kuwa TGDC ni mkombozi wa mazingira baada ya kuelezwa jinsi nishati hiyo ilivyo rafiki wa mazingira na ilivyo jadidifu isiyoathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi.
TGDC ni kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inayomilikiwa na Serikali kwa 100% iliyoanzishwa mwaka 2013 na kuanza shughuli zake rasmi mwaka 2014 ikiwa na jukumu la kuendeleza rasilimali ya jotoradhi nchini ambapo kwa sasa inayo miradi mitano ya kipaumbele yenye lengo la kuzalisha megawati 200 kwa awamu ikiwemo mradi wa Ngozi (MW 70), Kiejo Mbaka (MW60), Songwe (MW5-38), Luhoi (MW5) na Natron (MW60) ambapo kwa sasa TGDC ipo katika hatua ya maandalizi uchorongaji visima vya uhakiki wa rasilimali ya Jotoardhi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Bw.Halfan Halfan (wa kwanza kulia) Akipewa Maelezo ya Hatua Iliyofikiwa Katika Utafutaji Umeme wa Jotoardhi Katika Banda la TGDC Wakati wa Maonesho ya Sabasaba. Apongeza Jitihada.
Mkurugenzi Mkuu – EWURA Dkt. James Andilile (wa pili kutoka kulia) Akipatiwa Elimu ya Jotoardhi Katika Banda la TGDC Wakati wa Maonesho ya Sabasaba.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) Bw.Halfan Halfan (wa kwanza kulia) Akipewa Maelezo ya Hatua Iliyofikiwa Katika Utafutaji Umeme wa Jotoardhi Katika Banda la TGDC Wakati wa Maonesho ya Sabasaba. Apongeza Jitihada.