Dar es Salaam. Serikali imekuja na mfumo ambao utawezesha ufuatiliaji wa moja kwa moja wa mazao yanayonunuliwa na Wakala wa Hifadhi wa chakula wa Taifa (NFRA), huku ukitajwa kuondoa kilio cha wakulima kudai kuibiwa.
Mfumo huo wa kidijitali utamuwezesha mkulima kupata risiti ya mzigo wake kupitia simu ya mkononi, juu ya uzito wa mzigo husika papo hapo na kupewa risiti ya karatasi baada ya kupima bidhaa husika.
Hayo yameelezwa leo Jumapili, Julai 14, 2024 na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe mkoani Katavi wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizindua vihenga, ghala ya kuhifadhi chakula pamoja na mfumo huo wa kidijitali.
Bashe amesema wameamua kuja na mfumo huo, baada ya kupata kilio kutoka kwa wakulima kuwa vituo vya kununua mazao hasa maeneo ya vijijini wanahisi kuibiwa.
Jambo hilo liliwafanya kubadili mfumo katika vituo vyote 72 vilivyopo kwa gharama ya Sh14 bilioni.
Amesema mfumo umeenda sambamba na ufungaji mizani za kidijitali katika vituo vya vijijini, ambapo mkulima akiweka mzigo kupima anaona uzito wa mazao yake na atapokea ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu yake na kupewa risiti kutoka kwenye mzani.
“Uwepo wa mifumo hii pia utawezesha Mkurugenzi Mkuu ambaye atakuwa Makao makuu Dodoma kuona vituo vya nchi nzima, kujua vimenunua kiasi gani na atapata taarifa ya mwisho ya kiwango kilichonunuliwa kwa siku na kujua kiwango ambacho kitakuwepo siku ya kesho wanapoanza kununua katika maghala yote nchi nzima,” amesema Bashe.
Baada ya kutolewa kwa maelezo hayo, Rais Samia amesema wakati nchi ikiwa na lengo la kufikia uhifadhi wa chakula tani milioni 3 mwaka 2030, kama Serikali imeamua kuipandisha NFRA ili ifanye kazi vizuri kwa kuwa na mfumo mzuri wa ununuaji wa bidhaa za wakulima.
“Kilio cha wakulima kudhulumiwa uzito wa mazao yao sasa hakipo, kwani umewekwa mfumo mzuri utakaowawezesha kupima mazao yao wanaridhika na hauingiliwi na mkono wa mtu,” amesema Samia.
Amesema kupitia maboresho hayo mkulima anachokiweka kwenye mzani ndiyo kitakachoonekana.
“Pia tumekusudia kuipandisha NFRA kiutendaji, mifumo na teknolojia, tunatarajia kutoa bondi ya NFRA ambayo tunatarajia tutapata fedha nyingi huko, ili wakala iweze kununua mazao kwa wakulima kila msimu unapoingia kuliko tunavyofanya sasa, kila msimu ukiingia tuanze kuangalia tuna ngapi, benki gani inaweza kutupa wapi tunadaiwa.”
“Bond hii ikiwekwa wananchi wakinunua ‘share’ itafanya wananchi kupata fedha nyingi tutakaponunua chakula,” amesema Samia.
Amesema ili kukamilisha mipango hiyo, kila mtu anatakiwa afanye kazi sehemu alipo, anayenunua kwa mkulima anunue kwa haki, anayeongeza thamani ya mazao afanye vizuri.
Katika hatua nyingine, Samia amesema Serikali imekusudia kukuza sekta ya kilimo kutoka kile kilichozoeleka cha kulima na kula, kwenda cha biashara na sasa mazao kama mahindi, mpunga, mbaazi yaliyokuwa ya chakula yamekuwa ya biashara.
Mazao hayo ndiyo pia yanayofanya vizuri katika kujenga uchumi wa nchi, tofauti na yale yaliyozoeleka ya korosho, pamba na kahawa.
“Tumedhamiria kukuza kilimo na tumefanikiwa kuongeza bajeti ya kilimo kutoka Sh460 bilioni huko nyuma na mwaka huu iliyopitishwa na Bunge ni Sh1.25 trilioni, fedha hizi zinakwenda kwenye maeneo kadhaa ikiwemo skimu za umwagiliaji maji na kukuza skimu za ugani, mbolea kwa kutoa ruzuku ili kukuza uzalishaji ndani ya nchi,” amesema Samia.
Amesema fedha hizo pia zinakwenda kwenye uhifadhi wa chakula jambo ambalo limefanyika kwa uzinduzi wa vihenge na maghala.
Kuhusu Katavi kuwa kanda inayojitegemea katika ununuzi wa nafaka na uhifadhi wa chakula, amesema alitoa pendekezo hilo kutokana na urahisi walionao kwani wanaweza pia kununua kutoka mikoa jirani, kuhifadhi na kusafirisha kwa kutumia reli kwenda nje.
“Hivyo niwaombe sasa tujielekeze kwenye kuongeza tija uzalishaji, ili mkulima anufaike na Taifa linufaike. Sasa kwa sababu tumeamua Katavi iwe kanda inayojitegemea lazima muangalie namna ya kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula, hivyo niwaagize wahusika kuangalia namna ya kuongezeka maeneo mengine,” amesema Rais Samia.
Katika upande wa kuongeza uzalishaji, amesema mkoa huo una skimu 26 za umwagiliaji huku akibainisha kuwa sita nyingine zitaongezwa, ambapo uwepo wake utawezesha wakulima kulima mara mbili kwa mwaka.