Mvua zaleta maafa kila kona, hofu yaongezeka, shule zafungwa

Dar/mikoani. Mvua zinazonyesha sehemu tofauti nchini zimeendelea kusababisha uharibifu wa mali, miundombinu, mashamba na hata kusababisha vifo vya watu kutokana na kufurika kwa maji.

Leo Jumatano, Aprili 24, 2024, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetangaza mwendelezo wa mvua katika mikoa mbalimbali nchini na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari.

Mikoa mbalimbali jana iliripotiwa kuwa na mvua kubwa zilizosababisha madhara kwa wananchi kutokana na kuzidiwa na mafuriko, jambo ambalo limewafanya wahitaji msaada kutokana na madhara yaliyojitokeza.

Madhara yaliyoripotiwa kutokea ni pamoja na kuharibika kwa barabara na miundombinu mingine, kuharibika kwa mazao mashambani, madaraja kukatika, Mwenge kukwama na watoto wawili kupoteza maisha.

Kutokana na athari zinazojitokeza, baadhi ya shule zimechukua hatua ya kufunga shule kwa muda, ili kuwaepusha wanafunzi na mvua zinazoweza kuhatarisha maisha yao wakati wakienda au kutoka shuleni.

Baadhi ya shule katika mikoa ya Dar es Salaam na Mbeya zimefungwa kwa muda.

Shule ya awali na msingi ya Tusiime na Fountain Gate, zote za Dar es Salaam zimefungwa kwa siku mbili kuanzia leo na kesho, Aprili 29, 2024. Zitafunguliwa Jumatatu ijayo. Kesho ni sikukuu ya Muungano.

Halmashauri ya Kyela, Mkoa wa Mbeya yenyewe ilitangaza kuzifunga shule zake nne ikiwemo moja ya sekondari iitwayo Tenende. Za msingi zilizofungwa ni Matebe, Tenende na Ndola.

Hatua hiyo inatokana na mvua kubwa zinazonyesha na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara kupitika kwa shida pamoja na baadhi ya shule kuzingirwa na maji.

Mvua hizo ndizo zilizosababisha vifo vya wanafunzi saba wa Shule ya Msingi Ghati Memorial iliyopo Murieti jijini Arusha baada ya gari la shule kusombwa na maji Aprili 12, 2024.

Katika tukio hilo, msamaria mwema mmoja aliyejitolea kuwaokoa wanafunzi hao, naye alifariki dunia.

Akizungumza na Mwananchi, jana, Mmiliki wa Tusiime, Dk Albert Katagira, alisema wamefunga shule kwa muda kutokana na mvua zinazoendelea, kwani watoto wamekuwa wakichelewa kufika shuleni na majumbani.

“Tumeona hali imekuwa mbaya watoto wanafika nyumbani saa sita usiku kutokana na gari kukaa muda mrefu kwenye foleni kutokana na barabara kutopitika tukaona ni kuwatesa watoto,” alisema Dk Katagira.

Amesema watoto wamekuwa wakiamka mapema lakini wanafika shule saa tatu hadi saa nne asubuhi, hivyo hata utaratibu wa ufundishaji umekuwa ukibadilika.

Dk Katagira amesema kuchelewa kwa watoto kufika shule, kumesababisha kuchelewa kwa vipindi vya asubuhi badala ya kuanza saa mbili wanajikuta wameanza kwa kuchelewa.

Pia, amesema kutokana na kuharibika kwa miundombinu, wamehofia usalama wa watoto wanapokwenda shuleni au kutofika kabisa na sababu hizo zimewasukuma wafunge shule kwa siku mbili.

Waziri apongeza, yatoa maelekezo

Leo Jumatano, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amezungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam akizipongeza shule ambazo zimechukua hatua za kusitisha masomo na kuzisihi zingine kuchukua hatua za tahadhari.

“Tunatoa wito kama hali ya hewa ikiwa sio nzuri, wazazi wana haki ya kuwazuia watoto kwenda shule. Kwani kitu cha kwanza ni usalama wa watoto wetu, hivyo shule zina wajibu wa kufidia vipindi inapotokea hali mbaya ya hewa na wanafunzi kushindwa kufika shule,” amesema Profesa Mkenda.

Amesema tatizo hilo wanaliona zaidi katika shule binafsi ambako watoto wanasoma mbali na maeneo wanayoishi na kueleza kamishna wa elimu atatoa mwongozo ikiwemo mabadiliko kidogo ya ufundishaji au kusititisha kabisa masomo.

Waziri huyo amesema magari hanayobeba wanafunzi yachukue tahadhari kwa sababu Serikali haitaki kusikia imepoteza watoto kwa sababu tu magari yalikuwa yakiwapeleka shule.

Kuhusu shule za Serikali ambazo zimeathiriwa na mafuriko, amesema wamejipanga kuzirudisha na zile ambazo zipo katika maeneo hatarishi watatafuta maeneo mengine mbadala ya kuzinga.

Katika Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, mashamba yenye ukubwa wa hekta 528.3 yameharibiwa vibaya na mengine kufunikwa kwa tope zito kufuatia mvua kubwa zilizosababisha mafuriko kwenye kata 11 zilizopo wilayani humo.

Tathimini ya awali imebaini kuwepo kwa athari kubwa na huenda kukawa na upungufu wa  uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kwa msimu wa mwaka 2023/24.

Maeneo yaliyoathirika ni pamoja na kata Ngonga, Matema, Njisi, Talatala, Katumba, Songwe, Lusungo, Bujonde, Ipinda, Kajunjumele, Mwaya, Makwale.

Jana, Kaimu Ofisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Wilaya ya Kyela, Pantaleo Mushi amesema athari zilizojitokeza mwishoni mwa Machi na Aprili, mwaka huu kwenye zao la mpunga ni hekta 4,18.3 zimeharikiwa huku mihogo zikiwa ni hekta 74 na migomba hekta 36.

Awali, waliweka mikakati ya uzalishaji wa zao la mpunga tani 85,0500 kwa msimu wa 2023/24  lakini utashuka na kufikia tani 84.035.95  sawa na upungufu wa tani 1,465.

Kwa upande wa mihogo matarajio ilikuwa kuzalisha tani 44,000 lakini uzalishaji utashuka mpaka tani 42,372 ikiwa na upungufu wa tani 1,628.

“Kimsingi, kutakuwa na upungufu wa chakula kwani matarajio yamekwenda ndivyo sivyo na kama Serikali tunajipanga kuona msimu ujao tunaweka mikakati ya kukabiliana na janga la mafuriko,” amesema.

Mwathirika wa mafuriko hayo, Elizabeth Mwaimise alisema wamechoshwa na hali hiyo kila mwaka na kuomba Serikali iharakishe kuwatengea eneo ili wahame na watakuwa wakirejea kiangazi kwa ajili ya kilimo na sio makazi.

“Mafuriko ya mwaka huu yalikuwa ya kipekee  maji yalikuwa mengi  yalianza kuingia ndani saa 6.00 usiku  licha ya kuzingira makazi  mazao kama  mpunga, mihogo, migomba na kokoa kuharibika na mengine kumezwa na udongo,” alisema.

Naye Jesca Mwakalinga amesema licha ya kugoma kuondoka kwa miaka mingi,   sasa wamekubali kwa hiari yao na kuomba Serikali kuharakisha kutenga eneo.

“Kwa mafuriko ya mwaka huu tunaondoka kwa hiari yetu wenyewe, hali ilikuwa mbaya maji yalijaa, nyumba zote zilimezwa, mashamba, mazao yameharibika, tumepata hasara kubwa,” amesema.

Mkoani Mwanza, mvua zimeripotiwa kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara na daraja, jambo linalosababisha kero kwa watumiaji wa barabara hizo na pia kuhatarisha maisha na usalama wao.

Barabara za Airport kuelekea Kisesa pamoja na daraja la Masai lililopo katika barabara ya Uhuru jijini Mwanza ziko kwenye hali mbaya hasa daraja hilo ambalo limeanza kumeguka kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha.

Daraja hilo lililopo katika makutano ya mitaa ya Uhuru na Liberty linatumiwa na daladala zinazotoka Airport, Ilemela, Bwiru na Maduka tisa kupitia Kemondo kwenda Kishiri, Kisesa, Ilalila, Busweru, Machinjioni na stendi ya Nyamhongolo.

“Daraja hilo limekuwa hatari sana kwetu sisi na kwa abiria kwa sababu tayari limelika upande mmoja ukiwa unaelekea dampo, lakini bado kuna mchanga mwingi na kadri mvua zinavyonyesha, maji yanazidi kuongezeka na linazidi kumeguka, hali hii inahatarisha maisha yetu,” amesema Daniel Lyaganda, dereva wa daladala inayofanya safari za Kisesa – Ilemela.

Msafara wa magari ya mbio za Mwenge umelazimika kusimama kwa dakika kadhaa eneo la Manjecha katika kijiji cha Michenga wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, baada ya maji kujaa barabarani kufuata mkondo wa Mto Lumemo kuzidiwa.

Msafara huo ulisimama wakati ukitokea Halmashauri ya wilaya ya Mlimba kuanzia saa 3:19 asubuhi hadi saa 3:29 asubuhi ukitokea kijiji cha Igima na maofisa wa Jeshi la Polisi na wengine wakishuka kwenye magari ili kuvuka eneo hilo.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Mkazi wa Mchombe, Tukuzeni Lusingo amesema taarifa ambazo alikuwa nazo ni kuwa Mwenge ungelala Mngeta lakini kwa namna hali ya barabara ilivyo msafara ungepata shida zaidi kutokana na kuwa na maeneo mengi korofi.

“Tuliambiwa kuwa Mwenge wa Uhuru ungekesha Mngeta Mchombe, lakini umekesha Igima pengine kwa sababu kuna unafuu wa magari kufika tofauti na Mngeta ambako barabara imechafuka kwa sababu barabara bado ni chafu,” amesema Tukuzeni.

Watoto wawili waliokuwa wakiishi Mtaa wa Mkwajuni uliopo katika Manispaa ya Morogoro walifariki dunia Aprili 23, 2024 baada ya kuzama kwenye shimo la choo lililochimbwa na jirani yao mwaka mmoja uliopita.

Watoto hao, Glory Geitan (12) na Neema Emmanuel (11) walikuwa wakiishi na bibi yao, Anastazia Mpilipili ambapo siku ya tukio hilo bibi hiyo anaeleza kwamba aliwaacha nyumbani na kuwataka wamsaidie kazi za nyumbani.

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro lilithibitisha kutokea kwa vifo hivyo ambapo taarifa za kuwataka kwenda kufanya uokoaji ziliwafikia Aprili 23, 2024 saa 4:38 usiku, walipofika walikuta wananchi wameshawatoa.

“Jeshi la Zimamoto linawashauri wananchi wote wa mkoa wa Morogoro wanaoendelea na ujenzi, wajitahidi kuweka vizuizi au kufunika kabisa mashimo ya vyoo ili watoto na mifugo wasipate madhara kama haya,” amesema.

Akisimulia mkasa huo, bibi wa watoto hao, Anastazia amesema siku hiyo alishinda na mjukuu wake Neema ambaye alikuwa anaumwa shingo, ilipofika saa 11 jioni, Glory naye alirudi kutoka shuleni, akawaacha na kwenda kufuata simu yake alikokuwa anachaji.

“Niliporudi saa 12 jioni nikakuta mlango umefungwa, nikaanza kuita kwa majina yao wakawa hawaitiki, nikarudi, mizigo niliyokuwa nayo nikaitunza jikoni, nikadhani wako kwa jirani, jua likazidi kuzama na nikawa siwaoni ikabidi nianze kupita kwa majirani nauliza,wakaniambia hawapo, nikazunguka kote nikawakosa, hata zile familia ambazo tumezoeana nikafika lakini sikuwapata.

“Nikakumbuka kwamba wakati naondoka wajukuu zangu niliwaacha na mtoto wa jirani, ikabidi niende nikamuulize kama amewaona, akaniambia yeye amewaacha wanapanga kwenda kuogelea kwenye shimo ambalo liko jirani na nyumbani,” alisimulia mwanamke huyo.

Wakati mvua zikiendelea kunyesha maeneo mbalimbali, baadhi ya wananchi wamehofia kupata magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu baada ya nyumba zao kuzingirwa na maji na kusababisha baadhi ya vyoo kufurika.

Kila kipindi cha mvua imekuwa ni kawaida kwa maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam hasa mabondeni maji kuzingira makazi ya watu na kusababisha adha kwa wananchi wanaoishi maeneo hayo.

Pamoja na Serikali kutoa tahadhari na kuwataka wananchi hao kuhama, wamekuwa wakikaidi kwa madai ya hali ngumu ya maisha na kutokuwa na sehemu za kwenda.

Mkazi wa Mtaa wa Msisiri B Kata ya Mwananyamala, Gati Wambura amesema amezaliwa katika eneo hilo miaka 38 iliyopita ambapo hali hiyo haikuwepo.

“Ndani ya miaka hii mitano hii kero ndio imezidi kwa sababu ya watu waliouziwa maeneo kujaza vifusi, haya maji yamekuwa ni kero tunahofia magonjwa ya mlipuko kwani vyoo vingi vimejaa na kufurika,”amesema Wambura.

Wilayani Malinyi, Mkoa wa Morogoro, bei mafuta ya petrol imepanda kutoka Sh3100 hadi Sh5500 kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha ambazo zimeharibu kwa kiasi kikubwa barabara,  hivyo kufanya malori ya mafuta kushindwa kufika kwenye vituo vya mafuta wilivyopo wilayani humo.

Mmoja wa madereva wa bodaboda katika kijiji cha Kiswaga kata ya Sofi wilayani humo,  Constantine Gabriel amesema bei ya petrol ilianza kupanda wiki iliyopita baada ya barabara kuu ya Ifakara kwenda Malinyi kukatika na kusababisha magari ya mafuta na magari mengine kushindwa kufika Malinyi.

Gabriel amesema kwa sasa usafiri unaotumika ni bodaboda abiria wamekuwa wakitoka Malinyi hadi Mtimbira ambalo magari yanakoishia wamekuwa wakiwatoza abiria kiasi cha Sh35,000 hadi Sh40,000 kwa abiria mmoja.

“Hatutozi gharama hizo kwa kuwakomoa wananchi bali gharama za mafuta zimepanda na pia pikipiki zimekuwa zikiharibika kutokana na barabara yenyewe kuwa na mashino makubwa na kuna wakati dereva na abiria wanaanguka kwenye utelezi,” amesema Gabriel.

Agatha John, mkazi wa Kiswaga kata ya Sofi amesema msimu wa mvua wamekuwa wakiwafikisha hospitali kina mama wajawazito waliopata uchungu kwa kutumia bodaboda tena kwa gharama kubwa tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Amesema kabla ya mvua hizo wamekuwa wakilipa bodaboda Sh10,000 kutoka Sofi hadi hospitali ya wilaya lakini kwa sasa gharama hizo zimepanda hadi kufikia Sh25,000.

Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Sebastian Waryuba amesema pamoja na maeneo mengi katika wilaya hiyo kuathirika, kata ya Usangule ni miongoni mwa kata ambazo zimeharibika, maeneo mengi hayafikiki na usafiri wa gari zaidi ya bodaboda na kutembea kwa miguu.

Mkuu huyo wa wilaya amesema pamoja na mvua hizo kuharibu maeneo mengi, bado maeneo kama hospitali, benki, masoko na maeneo mengine huduma zinapatikana japokuwa kwa kusuasua.

Related Posts