ACT-Wazalendo, CCM wanavyonyosheana vidole uvunjifu amani Zanzibar

Unguja. Wakati Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akieleza kuna kauli zimeanza kutolewa kuashiria uvunjifu wa amani kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Chama cha ACT-Wazalendo kimesema hakuwezi kuwa na amani kama hakuna haki.

ACT-Wazalendo imesema licha ya viongozi wakuu kuhubiri amani, lakini matendo yanayotendeka yanaonesha hakuna nia ya dhati ya kuleta amani visiwani humo.

Julai 12, 2024 baada ya swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Kilimani, Rais Mwinyi alisema uchaguzi umekaribia na wote wanajua katika nchi kunapokuwa na uchaguzi kunakuwapo changamoto nyingi.

Dk Mwinyi amesema ni matarajio yao kwamba Mwenyezi Mungu awawezeshe waingie kwenye uchaguzi kukiwa na amani, salama na utulivu licha ya kwamba wameanza kusikia kauli kutoka kwa wenzao (hakuwataja) ambazo hazina viashiria vizuri.

“Lakini wakati tunaomba, kila mmoja wetu anapaswa kufanya jitihada, tumeshaanza kuzisikia kauli zinazokwenda kinyume cha hayo na mambo hayaharibiki siku ya uchaguzi, mambo yanaanza na kauli zinazotolewa na watu, kwa hiyo viashiria hivi vinataka dua nyingi,” alisema Dk Mwinyi.

Wakati wa mkutano wa hadhara wa ACT-Wazalendo, Jumamosi Julai 13, 2024 katika Uwanja wa Mshelishelini Tomondo, ikiwa ni mwendelezo wa mikutano ya hadhara ya viongozi wa chama hicho iliyoitwa kwa jina la ‘bandika bandua’ viongozi wa chama hicho walidai wanaohubiri amani ndio wanaochochea kuvurugika kwa amani hiyo ili kuingia madarakani, wakirejea yaliyotokea katika uchaguzi mkubwa na ndogo uliopita.

Akihutubia wanachama, wafuasi na wananchi waliohudhuria mkutano huo, Makamu mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Ismail Jussa amesema matendo yanayofanywa hayana viashiria vya kujenga amani kama inavyohubiriwa.

Jussa amesema baada ya uchaguzi wa mwaka 2020 watu 21 walipoteza maisha na wengine zaidi ya 700 kuumizwa, huku wengine wakijeruhiwa na kubaki na vilema kwa sababu watu walitaka kuingia madarakani kwa nguvu.

Hata hivyo, amesema baada ya madhila hayo yote aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho wakati huo, hayati Maalim Seif Sharif Hamad alikubali kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa masharti ya kutekelezwa mambo matatu.

Amesema mambo hayo ni pamoja na kulipwa fidia watu walioumizwa katika uchaguzi huo, mfumo wote wa Tume ya Uchaguzi ufanyiwe marekebisho na sheria za uchaguzi zibadilishwe.

Amesema maridhiano hayo yasiwe kwenye ngazi ya kitaifa bali yafike chini ngazi ya shehia.

Pasipo kufafanua zaidi akidai chama hicho kitatoa maelezo baadaye, Jussa amesema kati ya mambo hayo mpaka sasa ukikaribia uchaguzi mwingine ni jambo moja la kulipwa fidia ndilo limetekelezwa mengine bado wamekuwa wakipewa ahadi zisizotekelezwa mpaka sasa licha ya jitihada za viongozi hao kukumbushia utekelezaji wa ahadi hizo.

“Maneno yasiyokuwa na vitendo ni unafiki, kwa hiyo watu wanahubiriwa kulinda na kutunza amani lakini kwa matendo haya kweli amani inakuja vipi,” amehoji Jussa.

Amesema baada ya Othman Masoud kushika mikoba ya Maalim Seif, walisisitiza mambo hayo katika misingi 26 ya utekelezaji wake, lakini bado hakuna linalofanyika.

Jussa pia alizungumzia uchaguzi mdogo wa Pandani, Konde, na Mtambwe baada ya waliokuwa wawakilishi na wabunge kufariki dunia akidai uligubikwa na hila na dhuluma lakini baadaye haki ikapatikana walipokataa dhuluma hizo.  

Jussa amesema wanajiandaa kuing’oa CCM madarakani katika uchaguzi mkuu mwakani.

Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Taifa, Othman Masoud amesema sehemu ambayo haina haki haiwezi kuwa na amani na chama hicho kinafahamu lazima nchi ipate mageuzi makubwa ya kiuongozi ili iweze kufanikiwa kukuza uchumi wake.

“Waliopo madarakani mageuzi hawayataki kwa sababu kwao ni masilahi, sisi ACT tunasema hapana lazima nchi hii ipate mageuzi na inshaallah tutayapata,’” amesema.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema: “Leo unapokuwa na kigugumizi cha kubadilisha sekretarieti ya Tume ya Uchaguzi kwa nini, unataka tukuiteje, hakujawa na amani kwa sababu bado nchi hii haijawa na haki, lakini haya yote inabidi tuyapindue katika sanduku la kupiga kura Oktoba 2025.”

Alisema kumekuwapo tabia ya baadhi ya viongozi kutotenda haki na kutengeneza mazingira ya kuwanyima wananchi vitambulisho vya Mzanzibari.

“Ikiwa wewe unafanya hivyo ama uwe Waziri, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Diwani au Sheha unataka tukuiteje, si mwizi?” alihoji kiongozi huyo.

Amesema watu hawapo kwa ajili ya kutumikia nchi bali kwa masilahi binafsi na ndiyo maana yanatokea hayo yanayotokea (pasipo kufafanua).

Related Posts