Dar es Salaam. Masoko mapya tisa ya bidhaa za Tanzania yamepatikana kupitia maonyesho ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), wakati biashara ya zaidi ya Sh3.75 bilioni ikifanyika ndani ya siku 16.
Miongoni mwa nchi zilizoonyesha nia ya kununua bidhaa hizo ni Afrika Kusini, Uturuki, Saudi Arabia na Malawi.
Kufuatia hilo Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Alli Mwinyi ameitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), kuendelea kufanya utafiti wa masoko yanayopatikana ndani ya bara la Afrika na kutoa taarifa kwa wafanyabiashara.
Hayo yameelezwa leo Julai 13, 2024 katika hafla ya kufunga maonyesho ya Sabasaba yaliyofanyika leo jijini hapa ambayo yalianza rasmi Juni 28 mwaka huu.
Dk Mwinyi amesema matokeo yaliyopatikana kupitia maonyesho haya yameonyesha namna fursa ya kukuza bishara ilivyotumiwa vizuri na kampuni za ndani , huku akieleza kuwa matokeo zaidi yataonekana kupitia kushamiri kwa biashara, kukuza ajira na mapato ya nchi.
“Hivyo ninaziagiza wizara zote zenye majukumu ya kusimamia biashara nchini washirikiane kutatua changamoto zote zinazojitokeza,” amesema Dk Mwinyi.
Dk Mwinyi amesema kama nchi inayo fursa ya zaidi ya soko katika Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA), soko la Afrika ya Mashariki (EA) na soko la nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc).
Pia amesema bara la Afrika lina jumuiya tisa huku likiwa na nchi 54 ambazo fursa mbalimbali zinaweza kupatikana.
“Niiagize TanTrade, fanyeni utafiti wa kina wa masoko hayo na biashara za Tanzania zinazoweza kwenda kwenye masoko hayo huku na nyie wazalishaji na wadau zalisheni bidhaa zenye uhitaji katika soko la ndani na nje,” amesema Dk Mwinyi.
Amesema miongoni mwa bidhaa zenye soko ndani na nje ya nchi ni samaki, dagaa, mwani, sukari, mafuta ya kula huku akitaka uzalishaji ufanyike kwa utosehelevu na hata ziada.
Kwa upanden wake, Mkurugenzi wa Tantrade, Latifa Khamis amesema utafiti wa upande wa mauzo ya papo kwa papo yalikadiriwa kuwa ya Sh3.65 bilioni kwa wafanyabiashara wadogo, wakubwa na kati.
“Pia maonyesho haya yametupatia soko la bidhaa ikiwemo tani 20,000 za mihogo na tani 28,000 za viazi, pia kumekuwapo mkataba wa makubaliano ya kubadilishana wataalamu na wanafunzi,” amesema Latifa.
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema anaamini washiriki wa maonyesho hayo wamejifunza na sasa watakuwa na uwezo wa kushiriki maonyesho sehemu yoyote duniani.
“Kupitia maonyesho haya wafanyabiashara wamefundishwa kuwa katika kila wanachokifanya, lazima wawe wanalipa kodi kwa sababu nchi haiwezi kuendelea bila ulipwaji kodi,” amesema Dk Jafo.