BIMA YA AFYA KWA KILA MTANZANIA UHAKIKA WA MATIBABU; RAIS SAMIA

Na. Majid Abdulkarim, KATAVI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wakazi wa Katavi na Watanzania wote kwa ujumla kila mmoja kuwa na bima ya afya ambayo itamsaidia kupata matibabu yeye na familia yake ili kuepusha usumbufu wakati wa kupatiwa Huduma za matibabu kipindi mtu atakapo ugua.

Rais Samia, ametoa rai hiyo leo Julai 14, 2024 wakati akizungumza na watumishi wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Moa wa Katavi na wananchi wa mkoa wa Katavi mara baada ya kukagua utoaji huduma za afya na kuangalia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika hospitali hiyo.

“Niwaombe sana watakapokuja mfuko wa bima ya afya kila mwananchi anunue bima yake na familia yake maana yake unakata bima yako mara moja kwa mwaka unatibiwa mwaka mzima, mtusaidie kununua bima ya afya ili tuweze kujenga na kutoa huduma za afya katika hospitali kama hii na hata hospitali za Taifa, kanda, mikoa, wilaya na kata”. Amesisitiza Dkt. Samia

Amesema watanzania wakate bima ya afya ili kila mtanzania afya yake iweze kuimarika kwa kujiimarisha na uhakika wa matibabu wakati atakapo kuwa ameugua.

Serikali imedhamilia kupeleka huduma bora za afya karibu na wananchi kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika hospitali zote nchini kwa kuhakikisha vifaa tiba vya kisasa, dawa na vitendanishi pamoja na miundombinu inakuwa vizuri kwa wananchi kupata Huduma bora katika maeneo yao.

“Hii ni hospitali ya Rufaa ya Mkoa lakini ndani ya mkoa tumefanya kazi kubwa ya kuwekeza idadi kubwa ya vituo vya afya, hospitali za wilaya na vituo vya kata na kule chini kwenye zahanati”. Ameeleza Rais Samia.

Aidha, Rais Samia ameeleza masikitiko yake baada ya kutembelea wodi ya wakinamama ambapo alikuta idadi ya waliojifungua wengi wao ni mabinti wa umri wa miaka 14 hadi 19.

Kutokana na hali hiyo amewaomba wazazi kuwapa muda wa kusoma watoto wao badala ya kuwaozesha na kuzaa katika umri mdogo ambapo inachangia kujifungua watoto ambao umri wao bado hauja timia (njiti).

Hata hivyo amewataka Waganga wa Kuu wa Mikoa na watumishi wote wa afya nchini kutoa huduma bora kwa wananchi kama walivyoapa katika viapo vyao vya taaluma.

Related Posts