AISHI Manula hayupo katika kambi ya Simba pale Ismailia, Misri. Haijashangaza sana. Kiasi ilitarajiwa mambo yawe hivi. Uhusiano wa Aishi na Simba ni kama vile mwanadamu ambaye yupo ICU. Muda wowote unaweza kukata roho. Ni kama vile Aishi na Simba hawatakani.
Aishi ni miongoni mwa wachezaji wachache ambao wameondoka katika mioyo ya mashabiki na viongozi wa Simba. Baada ya kuruhusu bao tano kutoka kwa mtani, nguzo za mahusiano yao zikakatika. Kila nikirudia mabao yote matano ya Yanga sijaona kosa la Aishi. Hata hivyo, Simba hawaamini ninachokiamini.
Licha ya kwamba Aishi alikuwa nje kwa muda mrefu kabla ya pambano hilo bado sijaona bao ambalo Aishi alifanya makosa. Hapo hapo unajikumbusha kwamba ni viongozi wa Simba ndio waliolazimisha Aishi acheze kutokana na kushindwa kumuamini Ayoub Lakred katika pambano kubwa la watani. Walijua Ayoub angeyumba.
Aishi amewekwa katika kundi la Henock Inonga na Clatousa Chama. Kwamba wamekuwa wakihujumu timu kwa muda mrefu. Na hapo hapo Simba wakapanga kumtafutia Aishi kipa mpinzani wa daraja la juu kwa ajili ya kumng’oa langoni. Bahati nzuri wakampata Ayoub Lakred kutoka Morocco.
Haikuwa bahati mbaya kwa kipa wa kigeni kuja. Mabosi walipokosa kipa wa ndani wa kumng’oa Aishi wakalazimika kwenda nje ili mradi Aishi aondoke langoni. Hata Aishi mwenyewe anafahamu hilo, ndio maana naye kwa muda mrefu alikuwa na mpango wa kuondoka zake kurudi nyumbani kwake Azam
Ayoub amewatia jeuri zaidi mabosi wa Simba na mashabiki. Lakini wakati Simba wakiwa na hisia hizo dhidi ya Aishi inadaiwa kwamba Aishi mwenyewe ana hisia hisia dhidi ya Simba. Ameichoka timu. Anataka kupumzika kutoka katika shutuma za kila siku. Anataka kwenda zake nyumbani Azam akapumzike. Kichekesho ni namna pande zote zinavyolichukulia jambo lenyewe.
Simba walitaka kumpeleka Aishi Azam kwa mkopo. Kumuuza linaweza kuwa jambo gumu. Azam wanajua hali ambayo Aishi anayo. Ni jambo zuri kwao kutumia mgogoro wa Simba na Aishi kutotumia pesa nyingi kumnunua kwa sababu wanaweza kumpata kwa mkopo kisha kumpata bure mwishoni mwa msimu ujao ambapo Aishi atakuwa huru kwa sababu mkataba wake utakuwa umefika tamati.
Kwa mtazamo wangu ambaacho kilipaswa kufanyika ni pande zote mbili kukaa mezani na kuafikiana kuachana. Simba wakiwa wagumu wanaweza kujikuta wanamlipa Aishi mshahara, huku wakiwa hawana kazi naye. Bahati mbaya pia kwamba kuendelea kuwepo kwa Aishi kunaweza kuwafanya wawe na makipa wanne kama ilivyo sasa. Lakred, Ally Salim, Hussein Abel na Aishi mwenyewe.
Sawa, Aishi anaweza kuendelea kusota benchi, lakini haitakuwa na maana sana kama wataendelea kumlipa mshahara. Haina afya kwao. Kama Azam haitaonesha nia ya kumnunua kwa sasa na kisa wakaona masharti ya mkopo ni magumu basi Simba wanaweza kujikuta wamejiweka katika mazingira magumu bila ya sababu za msingi.
Kwa wenzetu, inapofikia hatua ya kutotakana kama hivi kinachotokea ni kuhitimishwa kwa mkataba wa mchezaji husika na kumuweka huru ili kila mtu ashike njia yake. Waingereza huwa wanasema ‘mutual agreement’. Hakuna kulipana. Kwa sasa Aishi akitaka kuvunja mkataba analazimika kuilipa Simba. Simba ikitaka kuvunja mkataba inalazimika kumlipa Aishi.
Kufikia hapo ni bora tu kila mtu akubali kupoteza. Mkataba unachanwa. Kila mtu anaenda njia yake. Basi. Sioni tena kama daraja la mahusiano kati ya Aishi na Simba linaweza kujengeka. Simba huwa wanaongozwa na watu wale wale kwa siku zote. Akitoka Salim Try Again basi atakuja Crescentius Magori au Kassim Dewji. Hisia zao kuhusu Aishi hazitaweza kubadilika.
Kuondoka kwa Aishi Simba kutaashiria nini? Mambo ni mengi. Kitu cha kwanza kabisa itaashiria mwisho wa manung’uniko ya Simba dhidi ya Aishi. Kwamba anawahujumu. Haikuanzia pambano ambalo walipigwa bao nyingi na mtaani. Ilianzia zamani. Hata bao aliloruhusu kutoka kwa Mapinduzi Balama lilileta zogo kubwa klabuni kiasi kwamba Aishi akaanza kukaa benchi na nafasi yake kwenda kwa Beno Kakolanya.
Lakini Simba watakuwa wamepunguza nafasi muhimu ya mchezaji wa kizawa kikosini. Kwa muda mrefu Aishi Manula, Mohammed Hussein Tshabalala na Shomari Kapombe wameisadia timu kusahau kuchukua wachezaji wa kigeni katika nafasi zao. Imewasaidia. Wamejikuta wakipambana zaidi katika nafasi za beki wa kati na mbele.
Hii ni faida ambayo watani wao wanayo kwa mabeki watatu wa kati. Dickson Job, Bakari Mwamunyeto na Ibrahim Bacca. Imesababisha wapeleke nguvu katika maeneo mengi. Kwa ninavyowatazama makipa wetu wazawa, Simba sasa imefungua mlango wa kuwa na kipa wa kigeni hata kama Ayoub akiamua kuondoka. Makipa wetu wazawa siku hizi wana viwango vidogo.
Kuondoka kwa Aishi Simba pia kutaashiria mwisho wa kushikana uchawi baina ya viongozi na wachezaji wao. Hii miaka ambayo Simba imeenda chini kuna wachezaji wameshikwa uchawi kila Simba inapofanya vibaya. Hata kwa Chama imekuwa hivyo. Kuna ambao bado wana hofu namna gani Simba itaweza kusonga bila yeye na kuna wanaosema ‘afadhali ameondoka”.
Tukiachana na hayo Aishi ana kazi ngumu aendako. Kipa namba moja wa Azam wa sasa hivi ni imara kweli kweli. Kama akienda Azam maisha yanaweza kuwa magumu kwa sababu Mohamed Mustafa ni jiwe kweli kweli. Ni sawa uende Yanga ukakumbane na Djigui Diarra. Maisha yanakuwa magumu. Sioni kama kuna ulazima wa Aishi kumpiga benchi Mustafa. Ni kipa haswa.
Vyovyote ilivyo Aishi anahitajika kucheza. Nafasi yake kwa Taifa Stars ni muhimu kuelekea katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026 na Afcon 2025. Hatuna makipa wa uhakika kukaa pale langoni kiasi kwamba wakati mwingine makocha wa Stars wanalazimika kuchagua makipa wa pili katika kikosi chao. Makipa wanaosugua benchi katika timu zao.