Kikapu Mbeya visingizio kibao Taifa Cup

TIMU ya mchezo wa Kikapu ya Wanawake Mkoa wa Mbeya imesema kuwakosa baadhi ya nyota wake, kucheza pungufu na kuwatumia wachezaji wasio na uzoefu ndio iliwapa wakati mgumu kutofikia malengo.

Timu hiyo ambayo ndio iliwakilisha mkoa huo baada ya wanaume kushindwa kushiriki kwa madai ya ukata, iliishia nusu fainali kwa kufungwa na Mara ambao walitwaa ubingwa huo.

Kamishna wa mchezo huo mkoani humo, Linda Luzira alisema pamoja na kufika nusu fainali ikiwa ni mafanikio, lakini walikwamishwa na mambo matatu na kwamba watajipanga upya mwakani.

Alisema katika mashindano hayo ya Taifa ‘Taifa Cup’, waliwakosa wachezaji wao muhimu kutokana na muda wa michuano hiyo kuingiliana na ratiba za mitihani kwa vyuo vikuu.

“Wachezaji kutoka Must na Mzumbe hawakushiriki kwa sababu ya mitihani, tukachezesha wachezaji 10 badala ya 15, lakini baadhi yao wengi hawakuwa na uzoefu.

“Lakini pamoja na yote tunashukuru tulicheza nusu fainali tukaishia hapo, tunaenda kujipanga kwa ajili ya mwakani kuweza kufanya vizuri na kurejesha heshima yetu,” alisema Linda.

Staa huyo aliyewahi kuchezea timu ya Taifa ya mchezo wa Kikapu, aliongeza kuwa pamoja na upungufu huo, wanahitaji kuwapo kwa Ligi ya Mkoa ambayo itawapa ushindani wachezaji.

“Tunasubiri vyuo vifunguliwe tuanze kucheza Ligi ya Mkoa, makocha wawe karibu nao ili kupata uzoefu na ushindani kutuwezesha mwakani kushiriki kikamilifu,” alisema staa huyo.

Related Posts