WACHEZAJI wa Gofu wa Jiji la Arusha wameibuka vinara kwa kutwaa tuzo nyingi kwenye raundi ya tatu ya michuano ya Lina PG Tour kwa wa kulipwa na ridhaa.
Elisante Lembris na Nuru Mollel walishika nafasi ya kwanza na ya pili mtawalia wakiwaacha wapinzani wao zaidi ya mikwaju 15.
“Sikucheza vizuri katika raundi mbili za awali, lakini hapa Arusha gofu imenikubali kwelikweli,” alisema Lembris baada ya kumalizika kwa michuano.
wawili hao walifuatiwa na vijana wadogo Jay Nathwani, Gaurav Chadder na Aliabass Kermali wachezaji wa ridhaa
Isaac Wanyeche kutoka Dar es Salaam alikuwa chini ya kiwango kwa mikwaju 21 hadi mwisho wa mzunguko wa mashimo 54, huku, Frank Mwinuka kutoka Serengeti alimaliza wa nne na alikuwa chini ya kiwango kwa mikwaju 22 na nafasi ya tano ikienda kwa Fadhil Nkya kutoka Dar es Salaam.
Jumla ya wachezaji 12 waliingia fainali ya mashimo 36 ya mwisho baada ya mchujo uliofanyika Ijumaa.
Wengine waliopita mchujo huo ni Hassan Kadio, aliyeshinda raundi ya pili Morogoro, Salum Dilunga Ninja, Athuman Chiundu pamoja na Angel Eaton, ambaye ni mchezaji wa pekee wa kike wa gofu ya kulipwa nchini.
“Nilicheza vizuri sana siku ya kwanza kwa kupata mikwaju 78 iliyokuwa alama ya tatu kwa ubora. Lakini siku ya pili mambo hayakuwa mazuri sana baada kurudisha mikwaju 88,” alisema Eaton na kudai haikuwa kazi rahisi kupambana na ‘Mapro’ wa kiume uwanjani hapo.
Kwa upande wa gofu ya ridhaa Nathwani, Kermali, Chadder na mwanadada Madina Iddi walichukua nafasi za juu na hivyo kumpa wakati mgumu Ally Isanzu ingawa bado anaongoza kwa matokeo ya jumla ya raundi zote tatu.
“Sijawahi kupata upinzani kama huu katika raundi mbili nilizoshinda viwanja vya TPC na Morogoro Gymkhana. Kijana Jay Nathwani amenikimbiza mno hadi kupata ushindi mdogo wa fimbo moja baada ya kumalizika kwa mashimo 54 ya michuano hii,” alisema Isanzu kutoka Dar es Salaam ambaye wengi walitegemea angeshinda kirahisi mno.
Lina PG Tour ni mashindano maalumu ya kumuenzi Lina Nkya aliyekuwa mlezi wa mafanikio ya gofu ya wanawake nchini kabla ya kufariki dunia mwaka uliopita.
Mashindano haya yatachezwa katika raundi tano ili kumpata mshindi wa jumla ambaye atakata tiketi ya kucheza mashindano ya gofu ya kimataifa ya Dubai, Falme za Kiarabu mwishoni mwa mwaka.