Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeunga mkono hatua ya wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo kuandamana kwenda ofisi ndogo za chama hicho, kikisema walikwenda mahali sahihi kwani hakiwezi kujitenga na changamoto za wananchi.
Chanzo cha kauli hiyo ni maandamano yaliyofanywa na wafanyabiashara zaidi ya 800 Julai 11, 2024 wakishinikiza uongozi wa Shirika la Masoko Kariakoo kurudisha majina yao katika orodha ya watakaorejea sokoni humo baada ya kukarabatiwa.
Kauli hiyo pia ni jibu kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ambaye katika kikao na wafanyabiashara walioandamana Julai 12, mwaka huu, aliwakosoa kwa kwenda ofisi za CCM.
“Mlichofanya wafanyabiashara jana (Julai 11) kwenda ofisi za CCM ni sawa na mgonjwa wa malaria kwenda kwa mtu asiyetibu malaria. Ofisi ya mkuu wa mkoa ipo, mlipaswa kuja hapa kwa kuwa ndiyo tunaolisimamia na siyo huko mlikokwenda,” alisema Chalamila Julai 12.
Wafanyabiashara hao Julai 11, waliandamana kwenda ofisi ndogo za CCM Dar es Salaam kupeleka malalamiko yao ya kuondolewa kwenye orodha hiyo.
Orodha ya wafanyabiashara hao ilitangazwa Julai 10 na Shirika la Masoko Kariakoo, likiorodhesha watu 891 kati 1,662 kurudi sokoni humo, huku wengine wakishindwa kujua hatima yao.
Soko hilo liliungua Julai, 2022 na Serikali ilitoa Sh28 bilioni kwa ajili ya ukarabati.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla katika mkutano wa hadhara alioufanya Mbezi kwa Yusuph, jijini hapa amesema:
“Juzi niliwaona wafanyabiashara wa Kariakoo wakiandamana kwenda ofisi ya CCM kwa sababu wanaamini hiki ndicho chama chenye Serikali.”
Maandamano ya wafanyabiashara hao kwenda CCM, Makalla amesema yametokana na kufahamu ukweli kwamba chama hicho hakiwezi kujitenga na kero za wananchi.
“Na mimi nilimshauri Mkuu wa Mkoa (Chalamila) walienda mahali sahihi, walienda kwenye ofisi wakijua ni ya CCM itakayotatua changamoto zao,” amesema.
Kutokana na mazingira hayo, Makalla alielekeza wafanyabiashara wote 1,662 waliopaswa kurejeshwa katika soko hilo wahakikiwe na kurejeshwa.
Umuhimu wa kutekelezwa hilo ni kile alichoeleza, soko lilipoungua wafanyabiashara hao waliahidiwa watarejeshwa pale ukarabati utakapokamilika.
“Kila aliyeondoka pale apate haki yake ya kurudi sokoni, wapewe wahakikiwe, hatutaki kughushi lakini vibanda vigawiwe kwa kila aliyekuwa muathirika wa moto na ndiyo wapewe kipaumbele,” amesema.
Ameueleza uongozi wa soko hilo kuhakikisha CCM haisikii kile alichokiita minong’ono na maandamano ya waliokuwa wafanyabiashara wa Kariakoo.
Amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha wanatenga muda wa kuwatembelea wafanyabiashara masokoni ili kutatua changamoto zao.