Dar/Siha. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amewataka Watanzania kuacha kutukuza miradi ya maendeleo wanayojengewa na Serikali kwa kuwa ni wajibu wao na si hisani.
Mbowe ametoa kauli hiyo leo Julai 14, 2024 alipohutubia mkutano wa hadhara katika Kata ya Nasai wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro.
Mbowe alionekana kukerwa na kitendo cha baadhi ya wabunge akiwamo wa eneo hilo kusifia mambo yaliyofanywa na Serikali.
Amesema Rais wa nchi hana hata senti tano akieleza fedha ya nchi inapotumika haiamriwi na Rais bali Bunge ambalo hujadili mapato na matumizi kabla ya kiongozi wa nchi kupelekewa muswada wa fedha ili ausaini kuwa sheria baada ya Bunge kupitisha.
“Bunge halina fedha zake, ukiona wanapitisha matumizi na mapato ni fedha za kodi, hizi fedha za kujenga zahanati, kujenga shule, kujenga barabara, Serikali ikijenga siyo fadhila kwenu ni haki yake na wajibu ambao wamechelewa kuutekeleza,” amesema Mbowe.
Amesema mpaka sasa nchi ina miaka 63 ya Uhuru kwa nini iwe na shida ya madarasa, akihoji kwa nini Wilaya ya Siha haina kiwanda hata kimoja lakini kuna vijana wanaomaliza shule na haijulikani wanakoenda.
“Mifumo yoyote ya kiutawala duniani kwa nchi zenye watu wenye akili, kuna kitu kinaitwa Serikali kuu halafu kuna Serikali ya Mitaa, mnasikia nchi hii kuna kitu kinaitwa Tamisemi maana yake Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,” amesema Mbowe.
Amesema asili ya Serikali ya mtaa ni lazima iwe na viongozi wanaotoka eneo husika lakini Serikali kuu wanaweza kutoka sehemu yoyote.
Mbowe amesema viongozi hao wa mitaa lazima wajue historia ya maeneo husika, miiko na tamaduni.
“Kitu kinachosababisha umasikini wa nchi hii ni viongozi wa Serikali za mitaa hawachaguliwi na wananchi wanateuliwa na Rais na wanaletwa kusimamia wananchi, wanasimamia uchumi wenu, maisha yenu na pia uhuru wenu matokeo yake hufanyika maamuzi ambayo hayaendani na eneo husika,” amesema.
Amesema umefika wakati wa wakuu wa wilaya wachaguliwe na wakazi wa Siha na si kuchaguliwa na Rais.
Mbowe amesema chama chake ni miongoni mwa vyama vikuu vya upinzani vilivyosimama imara wakati wa awamu ya tano, huku vingine vikianguka.
Amesema wao kama Chadema walisema kuliko wafe wamepiga magoti ni heri wafe wamesimama jambo lililowafanya kupambana kukitetea chama na kubaki kuwa chama pekee chenye uwezo, mikakati na mpango halisi wa kuitoa CCM madarakani.
Amesema chama hicho kina misingi minne pekee ambayo ni kusimamia na kupigania haki za watu wote, kusimamia uhuru wa watu, demokrasia na msingi wa nne ni maendeleo ya watu.
Amesema ili uchumi wa watu uongezeke ni lazima uchumi wa nchi upanuke kupitia uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Ili kuleta mageuzi, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema anaamini atakuwa mbunge, akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura ili waweze kupiga kura katika uchaguzi ujao.
“Una miaka 18 nenda kajiandike, umepoteza kitambulisho nenda kabadili taarifa zako upate kitambulisho, ulikuwa unakaa Dar es Salaam umestaafu umerudi nyumbani nenda karekebishe upige kura hapa tufanye mabadiliko,” amesema Lema.
Katika hatua nyingine, Mbowe amesema wataunda kamati ya watu 100 wanaoaminika na kukubalika kwenye maeneo yote wanayopita ili kukiandaa chama hicho na uchaguzi ujao.
Kamati hiyo aliyosema ni ya ukombozi itaundwa katika kata zote nchini ili kuwaandaa wenyeviti wa vijiji na vitongoji, madiwani na wabunge.
Amesema hayo katika mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Isanja, Sanya Juu, wilayani Siha.
Amesema chama hicho kinahitaji mikakati na mbinu ya watu jeuri na siyo wezi na watu makini wanaoweza kusimamia masilahi ya wengine.
Lema amesema watahakikisha maeneo yote wanayopita wanahamasisha kamati hizo ili kushughulika na Serikali ya CCM.