BAADA ya AS Vita kupindua meza dakika za jioni katika dili la winga Mkongomani Elie Mpanzu na Simba, wekundu hao wa Msimbazi wameendelea kumganda staa huyo hadi kieleweke.
Awali Simba na Mpanzu walikubaliana kusaini mkataba wa miaka miwili lakini baadae vigogo wanaommiliki Mpanzu akiwemo moja ya matajiri wapya wa AS Vita, aliingilia kati dili hilo na kumzuia winga huyo kusaini.
Hata hiivyo, Mpanzu aliendelea kuwasiliana na Simba ambaye hakuwa na shida nao ila aliwataka wamalizane na bosi huyo wa Vita aliyehitaji zaidi ya dola 250,000 ili amuachie ajiunge na Msimbazi.
Simba kwa nyakati mbili tofauti ilituma wajumbe DR Congo, akiwemo Salim Abdallah ‘Try Again’ kulainisha dili hilo lakini bado hakijaelewaka huku Mpanzu akilazimisha kuja Tanzania.
Wakati Simba ikiendelea kusubiri kigogo huyo wa Vita kumruhusu Mpanzu kujiunga Msimbazi, Wekundu hao wameshtukia jambo na fasta imemvutia waya winga Willy Onana kurejea nchini ili akajiunge na kambi.
Awali Simba ilimkaushia Onana ikipanga kuachana naye jambo lililopelekea abaki kwao Cameroon bila kujiunga na wenzake kambini, lakini ugumu wa dili la Mpanzu umewafanya vigogo wa Simba kufikiria kumpa nafasi nyingine nyota huyo aliyesajiliwa msimu uliopita akitoka kuwa MVP wa Ligi Kuu ya Rwanda.
Unavyosoma hapa, Onana yupo safarini kuja nchini ili kupewa maelekezo mapya na viongozi wa Simba na baada ya hapo atapaa hadi Ismailia ilipo kambi ya timu hiyo.
Wakati Onana akirejeshwa kikosini hali imekuwa tofauti kwa Aubin Kramo ambaye licha ya kupona majeraha yake aliyoyapata mwanzoni mwa msimu uliopita siku chache baada ya kusajiliwa na Simba, hatakuwa sehemu ya kikosi hicho kwa msimu ujao.
Akizungumza na Kituo cha Azam TV, Mjumbe wa bodi ya Wakurugenzi ya Simba Cresentius Magoli ambaye anahusika zaidi na usajili unaiondelea alisema ni ngumu kumbakisha Kramo kikosini lakini bado mazungumzo yanaendelea.
“Kramo ni mchezaji ambaye ameumia kipindi cha ‘pre-season’ akiwa ni mchezaji wa Simba, hajacheza mwaka mzima kutokana na majeraha hofu tunaweza kumrejesha kwenye timu na asifikie matarajio na tukampoteza mazima, hivyo tunatazama njia sahihi ya kufanya aidha tumtoe kwa mkopo au tumalizane,” alisema Magoli.
Mwanaspoti lilimtafuta Kramo, aliyethibitisha kuondoka Simba licha ya kuwa hakusema ni kwa mkopo au mazima, lakini gazeti hili limethibitisha amevunjiwa mkataba na vigogo hao wa Msimbazi.
“Ndio, tulikuwa na vikao vingi na tumefika mwafaka. Sitacheza Simba msimu ujao na hapa najiandaa kuondoka Tanzania. Siwezi kuongea mengi lakini niseme tu nawapenda mashabiki wa Simba na Mungu akipenda tutakutana tena,” alisema Kramo.
Aidha Mwanaspoti limenasa taarifa kutoka ndani ya Simba, kwamba klabu hiyo imemalizana na winga Jonathan Alukwu (21) kutoka Sporting Lagos ya Nigeria, ambapo anaweza akatua nchini muda wowote kuanzia sasa.
Alukwu mwenye uwezo wa kucheza winga ya kushoto na kulia, anakuja Tanzania kukamilisha baadhi ya vitu kama mambo ya viza na kupiga picha kwa ajili ya utambulisho.
Chanzo cha taarifa hiyo kutoka ndani ya Simba, kinasema Alukwu amesaini mkataba wa miaka miwili, hivyo akitua Tanzania, atashughulikiwa mambo ya viza, kisha atasafirishwa kwenda kujiunga na wenzake, waliopo Misri ambako timu hiyo imepiga kambi kujiandaa na msimu mpya.
“Alishatoka kijijini kwao, kwenda mjini kwa ajili ya kuja Tanzania, hivyo anaweza akaingia leo jioni (jana) Jumapili ama kesho (leo) Jumatatu,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Ni mchezaji kijana, Simba inaandaa timu itakayokaa na wachezaji kwa muda mrefu, hivyo akipokelewa, zitafanyika taratibu zinazotakiwa kisha atakwenda kujiunga na wenzake.”
Chanzo hicho kilisema kocha mpya wa timu hiyo, Fadlu Davids anajua ujio wa mchezaji huyo, kwani kila hatua wanawasiliana naye.
“Usajili uliofanywa kwa ujumla kocha anaufahamu na baadhi ya wachezaji alikuwa anawafuatilia CV zao za walipotoka.”
Kocha Fadlu Davids alifanya mahojiano na mtandao wa Simba, alizungumzia mazoezi ya mwanzo anayoyafanya ni kwa ajili ya kuwajenga wachezaji kiakili na fiziki.
“Nilianza kuwajenga kiakili, lengo nahitaji kila mmoja, awaze majukumu yaliopo mbele yake, pia mazoezi ya uwanjani ni ya fiziki zaidi, kisha nitawapa programu za mazoezi mengine,”alisema.