Nonga: Huyu Guede anajua sana!

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga ambaye kwa sasa ni kocha wa viungo wa Mbeya City, Paul Nonga amemtaja Joseph Guede kuwa ni mchezaji bora kutokana na kuwa vitu vitatu muhimu kwa wachezaji wanaocheza eneo hilo la ushambuliaji.

Guede aliletwa na Yanga ameitumikia timu hiyo kwa miezi sita na baadaye kupewa mkono wa kwaheri na sasa anatarajia kuitumikia Singida BS msimu ujao baada ya kumnasa hivi karibuni akimuacha Kennedy Musonda aliyebakizwa kikosini pamoja na Clement Mzize wanaoongezewa nguvu na Prince Dube na Jean Baleke.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nonga alisema yeye ni kocha, lakini amecheza eneo la ushambuliaji ameona vitu vitatu muhimu kwa Guede ambavyo vinampa tafsiri ya kuwa mchezaji mzuri.

“Kwanza ni mshambuliaji anayeweza kujitenga eneo zuri ndani ya boksi akiwa hana mpira, ana utulivu, anaweza kukaa na mpira pia ni mzuri wa kuona lango, kwani anajua sana kufunga,” alisema Nonga.

Alisema kuna vitu vingi anaamini kutoka kwa mshjambuliaji huyo ndio maana ameamua kumzungumzia licha ya Ligi Kuu iliyoisha kulikuwa na washambuliaji wengi huku Guede akicheza mechi chache na kufunga mabao sita, akifafanua kuwa, kama kocha katika kikosi cha timu hiyo angekuwa naye ni mtu sahihi.

Akizungumzia uamuzi walioufanya Yanga kwa kuamua kuachana na mshambuliaji huyo alisema hawezi kujua sababu lakini mchezaji kwenye timu anaachwa kutokana na kushindwa kufikia mahitaji ya kocha aliyempendekeza.

“Mchezaji anasajiliwa kwa mahitaji ya mwalimu akishindwa kufanya kile mwalimu alikuwa anataka akipate kutoka kwake ni rahisi kuachwa na mchezaji anaachwa kiufundi au kwa nafasi yake tangu alipokuwa anakuja,” alisema na kuongeza;

“Siwezi kuzungumzia kwanini Yanga wamemuacha sio nafasi yangu aliyependekeza kumuacha ananafasi kubwa zaidi ya kuzungumzia lakini kwangu ni mshambuliaji bora na mzuri.”

Related Posts