Mwanza. Gladness Mujinja, aliyeishi na Sospeter Makene kama mume na mke kwa miaka 17, amepoteza haki ya mgawanyo wa mali walizochuma kwa miaka 17 baada ya Mahakama kutamka ndoa yao ilikuwa batili, kwani aliishi kama kimada.
Hayo yamo katika hukumu ya Mahakama ya Rufani Tanzania katika rufaa iliyokatwa na Makene dhidi ya Gladness, akipinga mahakama za chini kumpa mgawanyo wa mali, licha ya kutamka kuwa ndoa ilikuwa batili kisheria.
Hukumu hiyo imetolewa Ijumaa ya Julai 12, 2024 na Mahakama ya Rufani iliyoketi Mwanza mbele ya jopo la majaji watatu ambayo ilibatilisha amri za Mahakama za chini juu ya mgawanyo wa mali na haki za kuishi na watoto wao watano waliowazaa.
Hukumu ya majaji— Lugano Mwandambo, Lilian Mashaka na Gerson Mdemu, imekubaliana na Mahakama za chini katika uamuzi kuwa wawili hao hawakuwa na ndoa halali, licha ya kuishi pamoja kwa miaka 17.
Katika maelezo ya rufaa, licha ya Mahakama kutamka ndoa ni batili, bado ilienda mbali na kutumia busara kugawa mali.
Maelezo yaliyotokana na mwenendo wa shauri hilo katika Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Gladness na Makene waliishi pamoja kwa miaka 17 kati ya mwaka 1991 hadi mwaka 2014.
Januari 7, 1996 walijaribu kufunga ndoa ya kikristo ambayo ingefanya itambuliwe na Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, lakini ilishindikana kanisani.
Ilibainika Gladness alikuwa na ndoa ya kimila na mwanamume mwingine aliyejitokeza kupinga ndoa hiyo isifungwe katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bunda mkoani Mara.
Wawili hao waliendelea na maisha kama kawaida hadi mwaka 2013, Gladness alipofungua maombi ya talaka katika Mahakama ya Wilaya ya Bunda, akidai kufanyiwa ukatili.
Kutokana na hilo, alifukuzwa kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi, akaiomba Mahakama itoe talaka na kumpa nafuu nyingine, ikiwamo mgawanyo wa mali wazochuma pamoja na impe haki ya kuishi na watoto.
Katika majibu, Makene hakupinga kuishi pamoja lakini hakukubaliana kwamba kuishi kwao kulifanya uwepo wa ndoa kutokana na Gladness kuwa na ndoa na mwanamume mwingine. Alieleza hakuna mali walizochuma pamoja na kwamba Gladness hastahili kupewa haki ya kutunza watoto ambao alimtelekezea.
Ndoa ilivyovunjwa, mgawanyo wa mali
Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Mahakama iliona ushahidi wa Gladness ulithibitisha kuwapo ndoa ya kimila kati yake na mwanamume mwingine, kabla ya kuamua kuishi na Makene kwa miaka 17.
Mahakama ikatamka ni kweli wawili hao waliishi pamoja, lakini ikasema ndoa ilikuwa batili, kwani uhusiano wake na Makene ulikuwa wa mtu na kimada, haukuwa ndoa kwa mujibu wa sheria.
Mahakama iligawa mali walizochuma, Gladness akapewa ng’ombe watano na kiwanja kilichopo eneo la Nyasaka, lakini ikampa Makene haki ya kuishi na watoto kutokana na Gladness kuwatelekeza.
Makene hakuridhika na uamuzi huo, akakata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza. Rufaa ilisikilizwa na Jaji Lameck Mlacha aliyetoa hukumu Septemba 21, 2016 akisema hapakuwa na ndoa halali.
Mahakama ya Rufani ilisema Jaji Mlacha aliona Gladness hakuwa na uwezo wa kuolewa na mwanamume mwingine kutokana na kuwa na ndoa ambayo haikuwa imevunjwa.
“Mahakama ya kwanza ya rufaa iliona kwa vile kulikuwa hakuna ndoa halali, hivyo talaka isingeweza kutolewa wala mgawanyo wa mali ambayo ilikuwa inadaiwa walikuwa wamechuma pamoja,” imeeleza hukumu ya Mahakama ya Rufani.
Hata hivyo, Mahakama Kuu ilichukua njia ileile ya Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana kuhusu mgawanyo wa mali ikiegemea busara kwa kuwa sheria iko kimya.
Ikafanya mabadiliko kidogo katika mgawanyo wa mali na matunzo ya watoto, Makene akapewa haki ya kuishi na mtoto mmoja na ikampa Gladness nyumba iliyopo Bunda, kiwanja kilichopo Kiseke na ng’ombe watano.
Mahakama Kuu pia ikaamuru Gladness apate asilimia 40 ya mgawo wa mauzo ya kiwanja kilichopo Nyasaka, kikiwa na mashine ya kusaga na asilimia 40 ya fedha zilizopo Benki za NBC na CRDB.
Mabishano Mahakama ya Rufani
Makene hakuridhishwa na hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, akakata rufaa Mahakama ya Rufani Tanzania akiwa na hoja mbili, ikiwamo mahakama za chini kukosea kuegemea shahada ya bodi ya usuluhishi.
Alidai Mahakama ilikosea kisheria kusikiliza ombi la talaka bila kuainisha ni hoja gani zinatakiwa kufanyiwa uamuzi na Mahakama iliyolisikiliza. Gladness aliridhishwa na hukumu ya Mahakama Kuu, hivyo hakukata rufaa.
Wakili Constantine Mutalemwa aliyemwakilisha Makene alijenga hoja kuwa Mahakama haikuwa sahihi kusikiliza ombi la talaka kwa kuwa haikuwa limeambatanishwa na cheti kutoka Bodi ya Usuluhishi inayotambulika kisheria.
Akadai cheti hicho hakikutolewa kortini kama kielelezo, hivyo akaiomba Mahakama ya Rufani itumie mamlaka yake kubatilisha mwenendo wa shauri hilo kwa kuwa ulikuwa batili, ingawa hakunukuu msimamo wowote wa sheria.
Wakili Julius Mushobozi, aliyemtetea Gladness alipinga hoja hizo na kueleza mjibu maombi alitimiza takwa la kifungu namba 101 cha Sheria ya Ndoa, hivyo hakuwa na haja ya kuwasilisha tena cheti hicho kama kielelezo kortini.
Katika hukumu, majaji waliona mwenendo wa kesi haukuwa na tatizo, kwani Mahakama ya Wilaya Nyamagana ilisikiliza na kutamka kuwa hapakuwa na ndoa halali baina ya wawili hao, msimamo ambao ulichukuliwa pia na Mahakama Kuu.
Katika hukumu, Mahakama ya Rufani ilisema baada ya Mahakama ya Wilaya ya Nyamagana kutamka hapakuwa na ndoa halali, ilipaswa iishie hapo na kuyatupa maombi ya talaka na haikupaswa kujielekeza kugawa mali.
Majaji walisema Jaji Mlacha ambaye ndiye ilikuwa ngazi ya kwanza ya rufaa, alifahamu uwapo wa kifungu cha sheria kinachosema hakuna amri ya mgawanyo wa mali inayoweza kutolewa pasipokuwa na talaka au ndoa halali.
“Hata hivyo, licha ya kubaini kuwa sheria haina kifungu kinachosimamia mgawanyo wa mali kutokana na kuvunjika kwa mahusiano ya masuria (kimada) kama ilivyo katika shauri hili, bado ilitoa amri ya mgawanyo wa mali,” inaeleza hukumu.
“Mahakama (Kuu) iliendelea kutoa amri ya mgawanyo wa mali na haki ya kuishi na watoto ikiegemea busara kuhalalisha kwenda na njia hiyo.
“Mamlaka ya Mahakama kutoa haki imepewa kupitia Ibara ya 107A na 107B ya Katiba,” wanaeleza majaji katika hukumu.
Akinukuu Ibara hiyo, inasema “Katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, Mahakama zote zitakuwa huru na kuzingatia tu masharti ya Katiba na sheria za nchi,” hivyo wakasema sheria inataka kuvunjwa kwa ndoa halali tu.
“Baada ya Mahakama kutamka kuwa kulikuwa hakuna ndoa ya mume na mke, ilitakiwa kuishia hapo na kuyatupa maombi ya talaka. Kwa vile haikufanya hivyo, ngazi ya kwanza ya rufaa (Mahakama Kuu) ilipaswa irekebishe kosa hilo,” inaeleza hukumu.
Kutokana na uchambuzi huo, majaji walisema wanatumia mamlaka waliyopewa kupitia kifungu 4(2) cha mamlaka ya rufaa kurekebisha uharamu wa kisheria uliofanywa na Mahakama zote mbili.
Hivyo, Mahakama ya Rufani imeamuru kubatilishwa kwa amri ya mgawanyo wa mali uliofanywa na Mahakama hizo na amri ya nani anastahili kuishi na watoto kwa vile zilikuwa amri batili, ila matamko yao kuwa ndoa ilikuwa batili yanasimama kama ilivyokuwa.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp 0765864917