Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imewahukumu kifungo cha maisha jela washtakiwa watano baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kusafirisha dawa za kulevya aina za heroini gramu 5,309.57 na kokeni zenye uzito wa gramu 894.28.
Hukumu imetolewa Julai 11, 2024 na Jaji Awamu Mbagwa, aliyesikiliza kesi hiyo ya jinai namba 58/2023.
Waliohukumiwa ni Muharami Abdallah, maarufu Chonji, Abdul Chumbi, Rehan Umande, Tanaka Mwakasafule na Maliki Maunda.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Jaji Mbagwa aliwahukumu kifungo cha maisha jela washtakiwa wote watano akieleza upande wa mashitaka umethibitisha makosa hayo bila kuacha shaka yoyote.
Washtakiwa walidaiwa kusafirisha dawa za kulevya kinyume cha kifungu cha 16 (1) (b) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012.
Katika shitaka la kwanza, walidaiwa Oktoba 21, 2014 eneo la Magomeni Makanya, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, walisafirisha dawa za kulevya aina ya heroini ambazo iwapo zingeuzwa zingekusanya Sh265.47 milioni.
Shtaka la pili, walidaiwa siku hiyohiyo na katika eneo hilo, walisafirisha dawa za kulevya aina ya kokeni za Sh62.59 milioni.
Katika kesi hiyo upande wa mashitaka uliwakilishwa na mawakili watano wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Saraji Iboru, huku washtakiwa wakitetewa na mawakili wanane wakiongozwa na Juma Nassoro.
Upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi 10 na vielelezo 12, ikiwamo mizani tatu za kupimia, bastola aina ya Browing iliyokuwa na risasi nane, ripoti ya mkemia, simu, cheti cha kukamata na ripoti ya kitaalamu ya taarifa ya uchunguzi na uthibitisho wa picha mjongeo (video).
Ilidaiwa mahakamani na shahidi wa kwanza wa mashitaka ACP Salmini Shelimo kuwa Oktoba 20, 2014 alikuwa akifanya kazi Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya (ADU), alipata taarifa kuhusu biashara ya dawa hizo iliyopangwa kufanyika.
Alidai alitoa taarifa kwa bosi wake ambaye alimtaka kufuatilia zaidi, baadaye alipata taarifa za uthibitisho kuwa watuhumiwa walikuwa wakipakia dawa za kulevya eneo la Magomeni Makanya.
Shahidi wa tano alidai kuwapanga wasaidizi wake kwa ajili ya doria ya mara kwa mara ya kupambana na dawa za kulevya ambayo ilikuwa imepangwa kufanyika Wilaya ya Kinondoni. Walichukua vifaa muhimu na kwenda kufanya operesheni Kinondoni Manyanya.
Ilielezwa wakiwa eneo hilo usiku walipata taarifa washtakiwa wameanza ufungaji Magomeni Makanya.
Alidai alienda na wenzake na walipogonga hawakufunguliwa mlango.
Shahidi alidai wakati wanasubiri kuingia ndani ya jengo hilo mshtakiwa wa kwanza (Chonji), alisogeza pazia lililokuwa mlangoni kuona anayegonga, alipoona ni maofisa wa polisi alipiga kelele kuwaambia wenzake watu wa Serikali wako nje.
Ilidaiwa wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo kuwa, watu waliokuwa ndani ya nyumba walianza kutoroka kwa kuruka ukuta, hivyo kuwalazimu maofisa wa polisi kuvunja mlango wa mbele na kuingia ndani ya nyumba kwa nguvu.
Ilidaiwa mshtakiwa wa kwanza alikutwa akiwa amesimama kwenye korido, akiwa ameshikilia bastola iliyokuwa na risasi nane kwenye magazine. Alikamatwa pamoja na wenzake wanne.
Mahakama ilielezwa koridoni kulikuwa na unga ulioshukiwa kuwa dawa za kulevya na baada ya kuwakamata walienda kuwaita mashahidi wa kujitegemea kabla ya kuanza upekuzi.
Kwa mujibu wa shahidi wa 10 ambaye ni ofisa wa polisi alidai mahakamani nyumba ambayo washtakiwa walikamatwa ilikuwa na vyumba viwili, choo na korido ambako walikuta pakiti 15 kwenye kabati.
Shahidi wa tano alidai mshtakiwa wa kwanza, aliyekuwa na funguo, ndiye aliyefungua kabati zilimokutwa pakiti zilizokuwa na unga ambao ulishukiwa kuwa ni dawa za kulevya.
Baada ya hapo, msako uliendelea hadi chumba cha pili ambako walichukua chombo kimoja cha kupikia (sufuria) ambacho kilikuwa na pakiti nane za unga unaodhaniwa kuwa dawa za kulevya, huku pakiti nyingine zikiwa zimepakiwa kwenye mfuko mweusi wa nailoni.
Vitu vilivyotajwa vilikamatwa na kupelekwa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya, kisha kupelekwa kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kwa uchunguzi, ilikobainika kuwa ni dawa za kulevya.
Ilidaiwa wakati wa kupekua na kukamata, shahidi wa nane alirekodi matukio muhimu ikiwemo la upekuzi kwa kutumia kamera ya ofisi aina ya Sony.
Kimsingi, washtakiwa wote watano walipinga mashitaka dhidi yao, wakikana kukamatwa kwenye nyumba inayodaiwa kuwa Magomeni Makanya wakiwa na dawa za kulevya, kupinga kusaini cheti cha kukamata na kupelekwa ofisi za ADU Kurasini, kushuhudia ufungashaji wa dawa hizo.
Chonji alidai siku ya tukio alikamatwa eneo la Magomeni Kondoa alikokuwa na duka la M-Pesa na kupelekwa kwa nguvu hadi kwenye nyumba hiyo ila alikiri kukutwa na fedha za sarafu tofauti Sh900,000, Euro 50, Dola 24,001 za Marekani na bastola.
Alidai fedha hizo zilikuwa ni mapato ya mauzo ya Luku na Mpesa na kuwa alikuwa na Dola kwa sababu alikuwa na mpango wa kufungua duka la kubadili fedha za kigeni na alitakiwa kuweka Sh50 milioni Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kupata kibali.
Mshtakiwa wa pili alidai mahakamani kuwa siku ya tukio alipigiwa simu na rafiki yake aliyemweleza yu mgonjwa mahututi na kuwa akiwa njiani kwenda kumuona alizuiwa na watu na kuingizwa ndani ya nyumba kwa nguvu, ambapo aliwakuta mshtakiwa wa kwanza na wa tatu.
Mshtakiwa wa tatu, aliieleza Mahakama aliajiriwa na Chonji kama mlinzi katika jengo la ghorofa moja ambalo liko karibu na eneo la tukio hilo na akiwa kazini alipanda ghorofani kukagua matangi ya maji, na aliporudi alikamatwa na polisi na kuingizwa ndani.
Mshtakiwa wa nne alidai alikamatwa eneo la maegesho na kisha kuburuzwa ndani ya nyumba hiyo ambako alimkuta mshtakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu.
Alidai alifika eneo hilo kuegesha gari lake na alikuwa akimtafuta mlinzi ili amkabidhi funguo za gari.
Mshtakiwa wa tano alidai alikamatwa Oktoba 20, 2014, alipokutwa akicheza kamari na baada ya kukamatwa polisi walidai Sh300,000 ili kumwachia lakini alikataa na akaendelea kuwekwa rumande hadi Oktoba 24, 2014 alipofikishwa mahakamani na kushtakiwa na wengine wanne.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clara Charwe aliieleza mahakama mashitaka yalithibitishwa pasipo kuacha shaka, na kuwa upande wa mashtaka ulimleta shahidi wa nne, ambaye alithibitisha kuchunguza unga uliokuwa kwenye pakiti na kubaini zilikuwa dawa za kulevya.
Kuhusu malalamiko ya msako kufanyika kinyume cha sheria kwa msingi kwamba hakukuwa na hati ya upekuzi, alidai upekuzi ulikuwa wa dharura kwa sababu ya mazingira chini ya uangalizi yapo chini ya kifungu cha 42(1) na si cha 38(3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Aliieleza Mahakama ingawa washtakiwa hawakuwa na jukumu la kuthibitisha kutokuwa na hatia, walipaswa kuthibitisha hawakuwa eneo la tukio.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Mbagwa alieleza masuala mawili ya kuamuliwa katika kesi hiyo ni iwapo washtakiwa walikutwa na pakiti 24 za unga unaodhaniwa kuwa dawa za kulevya na pili ni pakiti hizo zilithibitishwa ni dawa za kulevya.
Jaji alieleza shahidi wa nane alieleza alikuwa akipiga picha na kulinda eneo hilo wakati wa upekuzi na kuwa kilitolewa mahakamani kipande cha video kikionyesha mshtakiwa wa kwanza hadi wa nne wakiwa eneo hilo, na jinsi msako ulivyofanyika.
Alieleza shahidi wa tano alitoa cheti cha ukamataji ambacho washtakiwa wote watano waliambatanisha saini zao na alama za dole gumba mbele ya majina yao licha ya washtakiwa kukana kukamatwa kwenye nyumba hiyo na saini hizo.
“Baada ya kuzingatia ushahidi wa pande zote mbili ninakataa utetezi wa washtakiwa, wote watano walipatikana na kukamatwa katika nyumba ya Magomeni Makanya na walipatikana na pakiti 24 za unga unaoshukiwa kuwa dawa za kulevya, mtaalamu alithibitisha mahakamani zilikuwa ni dawa za kulevya” alieleza Jaji.
Hivyo upande wa mashitaka umethibitisha kesi bila kuacha shaka, washtakiwa wote wana hatia na amewatia hatiani na kuwahukumu kifungo cha maisha jela kama sheria inavyoelekeza.
Ameagiza kuharibiwa pakiti zote zilizokutwa na dawa za kulevya kwa mujibu wa kifungu cha 46 cha Sheria ya Dawa za Kulevya na Kuzia usafirishaji haramu wa dawa za kulevya na mali zilizokamatwa na kutolewa kama vielelezo kuendelea kuwa chini ya ulinzi hadi itakapoelekezwa vinginevyo.