Mamilioni ya raia wa Rwanda wameanza zoezi la kupiga kura katika uchaguzi wa rais na wabunge leo jumatatu huku kiongozi wa taifa hilo la Afrika Mashariki Paul Kagame akitarajiwa kushinda na kuendeleza utawala wake kwa miaka mingine mitano.
Paul Kagame, Kiongozi mkuu wa Rwanda tangu mwaka 1994 baada ya mauaji ya kimbari na raiswa nchi hiyo tangu 2000, anakabiliwa na wapinzani wawili tu katika uchaguzi wa raisi baada ya wakosoaji wengine kadhaa wakuu kuzuiwa kuwania.
Soma zaidi. Raia wa Rwanda wateremka vituoni kuchagua rais na wabunge
Orodha hiyo ya wagombea inajirudia kama ilivyoshuhudiwa katika uchaguzi wa mwaka 2017 wakati Kagame aliposhinda uchaguzi huo kwa kuwaacha mbali wapinzani wake kwa karibu asilimia 99 ya kura.
Frank Habineza, Kiongozi wa chama cha kijani cha (DGP), na mgombea huru Philippe Mpayimana ndio wagombea wawili pekee waliopitishwa kushindana na Kagame kati ya wanane walioomba kuwania nafasi hiyo.
Asilimia 65 ya idadi ya watu wa Rwanda walio chini ya miaka 30 wanamjua Kagame anayewania muhula wake wa nne kama kiongozi pekee ambaye wanamfahamu tangu kuzaliwa kwao.
Soma zaidi.Mapigano yaanza tena mashariki mwa Kongo kati ya jeshi na M23
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 66 anasifiwa kwa kulijenga taifa hilo upya lililokumbwa na taharuki baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 yaliyofanywa na Wahutu wenye itikadi kali ambapo waliwaua takriban watu 800,000, hasa Watutsi lakini pia Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuliwa.
Pamoja na kusifika Paul Kagame, mashirika ya kutetea haki za binadamu yanaushutumu utawala wake kwa kukandamiza vyombo vya habari na wapinzani wa kisiasa kwa kuwaweka kizuizini kiholela, mauaji na kutoweka kwa watu.
Mbali na hilo, serikali ya Kagame inakabiliwa na shutma za ku kimataifa ya kwamba inaliunga mkono kundi la waasi wa M23 katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa wanajeshi wa Rwanda wanapigana pamoja na waasi wa M23 katika eneo la mashariki lenye machafuko.
Mara hii ni uchaguzi wa rais na wabunge kwa mara ya kwanza
Katika uchaguzi huu, zaidi ya Wanyarwanda milioni tisa wamejiandikisha kupiga kura katika vituo 2,433, huku kinyang’anyiro cha urais kikifanyika sambamba na uchaguzi wa wabunge kwa mara ya kwanza.
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa mwendo wa saa 7:00 asubuhi kwa saa za Afrika ya mashariki na zoezi la kuhesabu kura litaanza mara tu zoezi hilo litakapokamilika majira ya saa tatu usiku.
“Nimekuja kupiga kura mapema ili nirudi kazini kwangu ni muhimu kupiga kura, tuna nafasi ya kuishi katika demokrasia nzuri ambayo wananchi wanaweza kuchagua viongozi wao wanafanya kazi kwa ajili yetu, wanatuwakilisha na kufanya maamuzi ili kuhakikisha maendeleo ya nchi yetu.” amesema mmoja ya raia wa Rwanda ambaye amejitokeza kupiga kura.
Mwingine aliyejitambulisha kwa majina ya Shabane Muhizi amesema “Nilipoamka asubuhi ya leo, nilihisi haja ya kuja kumpigia kura rais ambaye atakuwa kiongozi wangu. Ni jukumu la Wanyarwanda wote, kwa kuwa sasa nimepiga kura, najisikia vizuri. Kila kitu kiko sawa.”
Kagame alishinda kwa zaidi ya asilimia 93 ya kura mwaka 2003, 2010 na 2017 alipata asilimia 98.79 katika uchaguzi wa hivi karibuni, ikilinganishwa na asilimia 0.48 tu ya Habineza na asilimia 0.73 ya Mpayimana.
Soma zaidi: UN yaishtumu Uganda kuwasaidia waasi wa M23
Kabla ya uchaguzi huo, Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International liliripoti kuwa upinzani nchini Rwanda unakabiliwa na vikwazo vikali pamoja na vitisho vya kuwekwa kizuizini kiholela na kufunguliwa mashtaka.
Kukosekana kwa usawa kati ya Kagame na wapinzani wake kulidhihirika wakati wa kampeni ya wiki tatu, mabango mengi katika maeneo mengi ya nchi hiyo yalibandikwa yakinadi sera za chama cha Kagame cha RPF.
Wakati wa kampeni umati mkubwa wa watu ulijitokeza katika kampeni za Paul kagame huku wapinzani wake wakipata wakati mgumu wa kupata walau hata watu 100 wa kuhudhuria kampeni zao katika baadhi ya maeneo.