ZRA inavyojipanga kudhibiti rushwa Zanzibar

Unguja. Wakati Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) ikitunukiwa tuzo ya udhibiti vitendo vya rushwa, imesema hatua hiyo imeongeza morali kuendelea kupambana na vitendo hivyo ili kufikia malengo ya kukusanya zaidi ya Sh800 bilioni mwaka 2024/25.

Tuzo hiyo imetolewa na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu  Uchumi Zanzibar (Zaeca), ikiwa ni kutambua mchango wa ZRA katika kudhibiti vitendo vya rushwa na uhujumu wa uchumi kisiwani humo.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo Julai 15 2024, Kaimu Kamishna Mkuu wa ZRA, Said Ali Mohamed amesema ZRA, imejipanga kuhakikisha hakuna mianya ya rushwa katika utendaji kazi na huduma inazotoa.

“ZRA imejijengea utaratibu mzuri kuhakikisha jukumu la ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya Serikali linasimamiwa ipasavyo, huku ikitilia maanani udhibiti wa mianya yote ambayo inaweza kuvujisha mapato ya Serikali,” amesema.

Katika misingi hiyo, amesema ZRA itaendeleza weledi katika usimamizi wa mapato na kwamba, taasisi hiyo itadumisha ushirikiano na taasisi zingine ili kuhakikisha vitendo vya rushwa vinapigwa vita na kuchukiwa na kila mmoja.

Kamishna Said amesema pamoja na kutekelezwa kwa kanuni imara za kiutumishi, ZRA inayo mikakati iliyoandaliwa mahususi kwa lengo la kupambana na rushwa ili kudhibiti usimamizi wa mapato.

Amesema Mamlaka hiyo ina mkakati wa kupambana na rushwa 2022/2023 hadi 2024/2025, kanuni ya maadili ya kiutendaji kwa watendaji, na dira ya utoaji wa taarifa za masuala ya kimaadili.

Pamoja na mikakati hiyo, Kaimu Kamishna Mkuu wa ZRA amesema kwa kufahamu na kuyapa uzito masuala ya kimaadili kwa watendaji na walipakodi, muundo wa ZRA umeanzisha kitengo maalumu kinachosimamia upelelezi na maadili ya wafanyakazi.

Amesema hatua ya taasisi hiyo kuanzisha njia mbalimbali za mawasiliano kama programu ya ZRA Funguka na kituo cha mawasiliano ya walipakodi, ni miongoni mwa jitihada za kuona taasisi inajisogeza karibu zaidi na jamii ili kuweka wazi mianya ya upotevu wa mapato.

Mkurugenzi wa Zaeca, Ali Abdallah Ali amesema hatua hiyo ni kutoa motisha kwa taasisi ili kuongeza ushirikiano na kudhibiti vitendo hivyo.

Related Posts