Hizi hapa mbinu tatu uombaji sahihi wa vyuo vikuu

Dodoma. Wakati Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), ikitangaza kufunguliwa kwa dirisha la udahili kwa waombaji wa shahada ya kwanza kwa mwaka 2024/25, waombaji wametakiwa kuzingatia mambo matatu makubwa, ikiwemo mahitaji ya soko la ajira.

Mambo mengine wanayotakiwa kuzingatia ni ubora wa vyuo na ufadhili wa masomo utakayoyasoma, ikiwemo kutoka vyuo vya nje ya nchi.

Akitangaza kufunguliwa kwa dirisha la waombaji wa vyuo vikuu leo Jumatatu Julai 15, 2024 jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema waombaji wapo katika makundi matatu, ambayo ni pamoja na wenye sifa stahiki za kidato cha sita, wenye sifa stahilki za stashahada au sifa linganifu na wenye sifa stahiki za cheti cha awali cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) pamoja na stahahada.

Akizungumzia na Mwananchi leo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Paul Loisulie amesema kwa bahati mbaya nchi zinazoendelea watu hawana uhuru mkubwa wa kusoma wanachokipenda moyoni, badala yake huchagua kozi kulingana na upepo uliopo ama hamasa iliyopo katika jamii.

“Ninachoweza kushauri, kwanza kwa wale wanaoweza kuna aina sita za ajira ambazo hazijachuja duniani ya kwanza ni uhandisi wa kompyuta kwa ujumla wake, ikiwemo Tehama. Kuna mambo ya akili mnemba, mifumo ya Tehama ina soko sasa hivi duniani kote,” amesema.

Amesema kozi nyingine ambazo zina soko duniani ni data (takwimu), uhandisi, sanaa pamoja na ubunifu.

Aidha, amewataka wanafunzi wa vyuo kutojikita tu kwa kozi watayokwenda kusoma na badala yake kutafuta na taarifa nyingine zinazoweza kuwaongezea thamani ya kile atakachokisoma.

“Kwa ujumla mtu anaweza kusoma kozi yoyote, lakini kwa ujumla wake anaweza kujiongeza. Bila kujiongeza hata yule anayesoma kompyuta hawezi kutoboa. Wakijiongeza watapata vitu vingine ambavyo vimejificha,”amesema.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MENT), Ochola Wayoga amesema wanafunzi hao wanatakiwa kuomba udahili ambao kwao ni sehemu ya wito wao.

“Tuna vyuo vingi nchini, lakini sio vyote vina ubora. Kuna vyuo ambavyo kijana akienda ni sawa sawa tu na akifanya kitu kingine,” amesema.

Amesema kwa wale wenye ufaulu mzuri katika mitihani hiyo, wanatakiwa kuangalia fursa za ufadhili wa masomo nje ya nchi ambazo hutolewa kila mwaka na baadhi ya nchi.

Amesema kwa wazazi ambao ni wafanyabiashara, anashauri vijana hao kukaa nao kwa mwaka mzima kujifunza biashara inafanyikaje na kisha kwenda kuchagua kozi itakayomsaidia kuiboresha zaidi.

Amesema kwa kufanya hivyo, itasaidia mwanafunzi huyo kutohangaika na mikopo ya Serikali na badala yake kutumia mapato yanayotokana na biashara kujilipia ada.

Wayoga amesema ni muhimu pia kabla ya kukopeshwa mkopo wa elimu ya juu, wanafunzi wakapata elimu juu ya fedha hizo ambayo mara nyingi hawapati, jambo ambalo linafanya hata urejeshaji kuwa wa tabu.

“Kwa sababu wengi watakuwa wanaomba mkopo, wanatakiwa kujua angalau A, B, C, D ya mikopo hiyo ambayo wanapaswa kuilipa wakati wanapoanza kazi,” amesema.

Related Posts