Crispin Ngushi apewa mmoja jeshini

ALIYEKUWA mshambuliaji wa Yanga, Crispin Ngushi amejiunga na kikosi cha Maafande wa Mashujaa ya Kigoma kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Ngushi aliyewahi kuichezea Mbeya City, amejiunga na Mashujaa akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na Yanga kumalizika huku Coastal Union iliyokuwa inamtumia kwa mkopo msimu uliopita, ikishindwa kukubaliana naye maslahi binafsi ya kubaki naye.

Mwenyekiti wa Mashuja, Meja Abdul Tika alisema, wao kama viongozi wanaendelea kuimarisha kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao, huku akiweka wazi malengo yao makubwa ni kuleta ushindani tofauti na walivyofanya msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara.

“Msimu ujao tunataka kufanya vizuri zaidi ndio maana tumeanza maandalizi mapema ya kuimarisha kikosi, wachezaji ambao tutakubaliana nao tutawatangazia kama ambavyo tumefanya kwa wengine, hivyo mashabiki wawe na subra ya hilo,” amesema.

Akizungumzia maandalizi ya msimu ujao kwa ujumla, Meneja wa timu hiyo, Athumani Amiri amesema wanaendelea na kambi yao jijini Dar es Salaam katika fukwe za Bahari ya Hindi na kuanzia wiki ijayo wataanza safari ya kwenda visiwani Zanzibar.

Mastaa wengine wapya waliosajiliwa na Mashujaa ni Ally Nassoro ‘Ufudu’ (Kagera Sugar), Yusuph Dunia (Geita Gold), Robert Mackidala (KenGold), Ismail Mgunda (Singida Black Stars), Mathew Michael (Mbeya City) na Seif Karihe aliyetokea Mtibwa Sugar.

Related Posts