Utalii wa matibabu kuipaisha Tanzania

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiendelea kuboresha sekta ya afya, wananchi kutoka mataifa mengine wamekuwa wakifunga safari kwa ajili ya utalii wa matibabu nchini, hususani ya moyo, figo na saratani.

Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zilizokusanywa kutoka Idara ya Uhamiaji zinaonyesha idadi ya watalii iliongezeka kwa asilimia 24.3 hadi kufikia 1,808,205 mwaka 2023 ikilinganishwa na 1,454,920 walioripotiwa mwaka 2022.

Ripoti hiyo inaonyesha katika watalii wote waliofika nchini mwaka 2023, asilimia 6.8 walitoka Zambia na kati yao Wazambia hao, asilimia nane walikuja kwa matibabu.

Kenya ilikuwa na asilimia 5.1 ya watalii wote waliofika nchini, na kati yao asilimia nne walifika kutibiwa.

Burundi ilikuwa na watalii asilimia 4.8 ya wote waliozuru nchini na kati ya waliokuja kwa matibabu ni asilimia 46.

Kwa upande wa Uganda, ilikuwa na watalii asilimia tatu walioingia nchini mwaka 2023 na kati ya hao, waliofika kutibiwa ni asilimia 2.6.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ilikuwa na asilimia 2.5 ya watalii wote na kati yao asilimia 10 waliingia nchini kwa matibabu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wageni kutoka mataifa mengine yakiwamo Marekani, Italia, na Ujerumani waliotembelea Tanzania walikuja kujivinjari na likizo.

Wapo waliotoka Kenya na Burundi waliokuja kutembelea marafiki na jamaa, kuhudhuria mikutano na makongamano.

Uwepo wa Bandari ya Dar es Salaam unatajwa kuwa moja ya sababu ya kuvutia wageni kutoka Zambia, Zimbabwe, na DRC kuja Tanzania kwa sababu za kibiashara.

Katika kukuza utalii wa matibabu, Wizara ya Afya katika hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 ina mpango wa kuuendeleza kwa kuzijengea uwezo Hospitali za Taifa, Maalumu na Kanda ili kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa wananchi na raia wa kigeni.

“Hadi kufikia Machi 2024 jumla ya raia wa kigeni 7,843 kutoka nchi mbalimbali walipata huduma hizo kupitia wataalamu wa ndani ikilinganishwa na raia wa kigeni 5,705 mwaka 2022/23,” inaelezwa na wizara katika hotuba ikiyowasilishwa bungeni na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu.

Wagonjwa wengi kwa mujibu wa taarifa wanatibiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Saratani Ocean Road, Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma na baadhi ya hospitali za kikanda nchini.

Mbali na hospitali za Serikali, pia zipo za binafsi zinazotoa matibabu kwa wageni kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Watoa Huduma za Afya Binafsi (APHFTA)), Dk Egina Makwabe, huku wakijipanga kuandaa kanzidata kuonyesha wengi wanatoka nchi gani na wanatibiwa nini.

Hilo litaenda sambamba na kutekeleza mkakati wao wa kuweka mnyororo mzuri wa utoaji wa huduma ili kujua hospitali gani inatoa huduma gani za kibingwa na wataalamu waliopo.

Hilo amesema litasaidia utoaji wa rufaa za wagonjwa badala ya kuwaandikia kwenda nje ya nchi, wataelekezwa hospitali zinazotoa huduma za kibingwa nchini.

“Pia, tunatarajia kuwa na mkutano wa mashirika yasiyokuwa ya Serikali utakaofanyika Agosti 30 na 31 mwaka huu jijini Dar es Salaam ukijumuisha wadau kutoka nchi za Afrika Mashariki, moja ya mada itakayozungumziwa ni utalii tiba, tutapata nafasi ya kuwaambia wenzetu tunafanya nini ili tuweze kupata wagonjwa zaidi,” alisema.

Hata hivyo, amesema suala la uwezeshaji utalii tiba linahitaji ushiriki wa pamoja kati ya Wizara ya Afya, Idara ya Uhamiaji Tanzania, na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Profesa Abel Kinyondo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amesema wakati dunia inaanza kuhama kwenda katika aina nyingine za utalii, tiba utalii ni moja ya hatua inayoweza kuanza kutumiwa na nchi kuendelea kujipatia fedha.

Ili utalii huo uzae matunda ameshauri kuhakikisha uzingatiwaji wa ubora wa huduma zinazotolewa ili kuifanya nchi kuwa miongoni mwa machaguo ya watu kama ilivyo kwa nchi kama vile India.

“Pia, upatikanaji wa vitanda ni moja ya kitu cha kuzingatia, si upatikanaji wa vitanda hospitalini tu hata katika hoteli kwa sababu wagonjwa wanaokuja wanaongozana na ndugu na jamaa, baadhi huongozana na wauguzi, hivyo ni lazima wawe na sehemu ya kulala,” amesema.

Amesema iwapo mgonjwa anatibiwa Hospitali ya Taifa  Muhimbili basi iwepo hoteli karibu ili kumuondolea msaidizi usumbufu wa kutembea kilomita nyingi kila anapotaka kumuona mgonjwa wake.

Pia, amesema upatikanaji wa visa ni moja ya jambo ambalo linapaswa kuangaliwa ili kuweka urahisi kwa wanaotaka kuja nchini kutibiwa.

Profesa Aurelia Kamuzora amesema tafiti zianze kufanyika hasa katika miti ya asili ambayo huweza kutibu magonjwa ili kuifanya nchi kuwa na kitu cha tofauti.

“Hii itatusaidia sana badala ya kusubiri watu kutoka nje watufanyie tafiti na watengeneze kitu wakati tunaishi nacho katika mazingira yetu, utofauti ndiyo utakaotubeba kwani baadhi ya nchi zinafanya hivi na zinafanya vizuri,” amesema.

Related Posts