HISIA ZANGU: Kuna hili la Fei Toto, halafu kuna lile la Aziz Ki

KUNA suala la Fei Toto. Tukasikia na kuambiwa kwamba Simba inamtaka. Sasa hivi yupo katika kambi ya Azam nchini Morocco. Niliongea na watu wa Azam wakaniambia kwamba hawana habari hiyo na dau la Fei Toto kwenda kwingineko linajulikana.

Nikaongea na mwandishi au tumuite mchambuzi mmoja ambaye alikuwa amelikazania jambo hilo na kwamba lipo akaniambia kwamba ameongea na Fei mwenyewe na Fei yupo tayari kwenda Simba. ningechagua lipi?

Nikatengeneza hisia. Kwanza huenda lilikuwa jambo ambalo liliandaliwa na watu kadhaa wa Simba kwa ajili ya kupoza machungu yaliyokuwa yanatarajiwa ya Clatous Chama. Viongozi walikuwa wana msimamo thabiti wa kuachana na Chama.

Dakika za mwisho kukawa na hofu kwamba jambo lenyewe lingewatibua mashabiki wa Simba. Ndio maana walijaribu kupambana dakika za mwisho. Na ndio maana pia labda jambo la Fei kwenda Simba nalo likawa linapenyezwa.

Akili ya kawaida inakwambia kwamba Azam wamepata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa wa Afrika baada ya miaka mingi. Wanawezaje kumuachia Fei katika nyakati hizi? Mchezaji wao bora wa msimu uliopita. Inawezekana vipi?

Akili nyingine inakwambia inawezekana. Simba na Azam hawana baya. Mzee Bakhresa aliwahi kuwa mweka hazina wa Simba. Vipi kuhusu watoto wake? Lakini pia Simba iliwahi kuwachukua kwa urahisi Shomari Kapombe, John Bocco, Aishi Manula na Erasto Nyoni. Kuna urafiki wa Simba na Azam na kuna uadui wa Yanga na Azam ambao unaendelea kuimarika.

Lakini huyu mwandishi aliyenihakikishia kwamba alikuwa anaongea na Fei mwenyewe hatuna sababu ya kumpuuza. Hawa wachezaji wetu wakienda kucheza Azam wanakosa sifa wanazozitaka. Huenda uvumi wenyewe pia ulikuwa unamfurahisha Fei. Na huenda kweli Fei alikuwa tayari.

Alikuwa na msimu bora uliopita. Alifunga mabao mengi akapika mengine. Unadhani angekuwa Simba au Yanga sifa zake zingekuaje? Lakini kwa sababu mabao amefunga Azam basi watu wamekaa kimya. Kibinadamu hata yeye mwenyewe sasa hivi anajua anachezea timu ya namna gani. Wakati mwingine pesa sio kila kitu.

Upande mwingine kuna jambo la Aziz Ki. Hatimaye amesaini mkataba mpya pale Yanga. Haijanishangaza sana. Nimesikia ameachana na dili kubwa ambazo angeweza kupata kwingineko na ameamua kusaini katika klabu hii ya Jangwani.

Hisia zangu zinaniambia Aziz aliamua kusaini Yanga muda mrefu uliopita. Na Ukweli ni kwamba alisaini mkataba mpya Yanga kabla hajaenda likizo nyumbani. Sina uhakika sana kama alipata ofa kubwa kuliko aliyowekewa mezani na Yanga.

Ninachofahamu ni kwamba Yanga hapa karibuni walitengeneza mazingira ya kujitekenya kisha kucheka wenyewe. Walitengeneza mazingira ya kibiashara katika saini ya Aziz Ki. Kumfanya ang’are na jina lake lichomoze zaidi katika harakati hizi za usajili aonekane kama vile ni mchezaji mpya aliyewasili nchini.

Wakatengeneza mazingira kwamba Aziz alikuwa hajasaini kwao wakati walijua wazi kwamba Aziz alikuwa amesaini mkataba mpya. Wakatengeneza mazingira kwamba walikuwa katika wakati mgumu wa kuipata saini ya Aziz wakati haikuwa kweli. Hata rais wao, Hersi Said aliwapiga chenga ya mwili waandishi wa Afrika Kusini kwa kuwaambia Aziz hajasaini Yanga halafu ndani ya saa 24 akatangazwa amesaini mkataba mpya.

Nilifahamu ugumu wa Aziz kuondoka nchini. Aziz analelewa kama mtoto na familia ya GSM pamoja na ile ya Hersi. Yeye, mama yake mzazi pamoja na dada yake wamekuwa familia ya Yanga. Klabu ambayo ilipaswa kumuondoa Aziz nchini ingepaswa kufanya kazi ya ziada.

Kuna tofauti ya dau la mshahara au malipo ya kusaini mkataba ambalo lingeweza kumuondoa Aziz nchini, lakini lilipaswa kuwa dau kubwa maradufu. Lilikuwa ni suala dogo tu kwa Aziz kusaini Yanga mkataba mpya tofauti na watu wengi walivyokuwa wanafikiria. Uamuzi wa Aziz kuondoka au kubaki Yanga unabakia zaidi kwa mama yake kuliko wakala wake.

Lakini ukiachana na hayo, kuna raha kubwa ya kuwa Aziz Ki katika Jiji la Dar es salaam na nchi ya Tanzania. Unaishi kwa raha mstarehe. Unaishi kama Cristiano Ronaldo au Lionel Messi. Kila unakopita, kila unalofanya.

Jambo hili linawasumbua wanasoka wengi waliopata ustaa nchini. Wawe wa kigeni au wazawa. Kwa upande wa wazawa hii inaashiria ndio maana hatuna wachezaji wengi wanaocheza nje. Wachache wanaokwenda huwa wanarudi. Hawana uvumilivu wa kujenga himaya mpya nje ya nchi yao.

Kwa wageni utagundua namna ambavyo wanaipenda Tanzania na utulivu wake, watu wake ni marafiki, chakula ni kizuri. Hawapati kasheshe. Wengine rafiki zangu kina Mukoko Tonombe waliamua kuoa hapa.

Nadhani hii ilimsumbua hata rafiki yetu Fiston Mayele wakati alipokwenda Misri. Akili yake alikuwa ameiacha Yanga na Tanzania kwa ujumla. Akachukua muda mwingine kuzungumzia mambo ya Yanga na Tanzania kuliko mambo ya Misri.

Mpaka sasa ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu Misri, lakini usidhani kama pale Misri anazungumzwa sana kama ambavyo angekuwa anazungumzwa Tanzania. Haishangazi kuona mara nyingi mastaa wetu wa kigeni hata wakiondoka baadaye wanarudi nchini.

Sasa hivi wapo tayari hata kurudi katika timu za kawaida tu kama Namungo au Singida ilimradi tu wawepo nchini. Sidhani kama Aziz angesaini kwingine kiurahisi na kuacha ufalme wake Tanzania huku akilelewa kama mtoto mdogo na Hersi. Huu ni mtego ambao wachezaji wetu wanajivalisha wakipata ustaa mkubwa katika klabu za Simba na Yanga.

Related Posts