ALAT yapewa mbinu kuleta mabadiliko kwa jamii

Unguja. Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) imetakiwa kujipambanua kwa kutetea masilahi ya umma ili kuleta mabadiliko ya kweli kwenye jamii, jambo ambalo limetajwa kuwa litaifanya iweze kuheshimika.

Hayo yameelezwa leo Aprili 24, 2024 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Masoud Ali Mohammed alipofunga mkutano wa 38 wa ALAT, uliofanyika kwa siku mbili mjini Unguja.

Kinyume chake, Masoud amesema ALAT wasipokuwa wakweli na kuendelea kuoneana aibu, hawataweza kuleta mabadiliko yanayotegemewa na wananchi.

“ALAT ni chombo muhimu ambacho kinatakiwa kusimamia uadilifu, kupambana na ubadhirifu wa mali za umma, kutetea masilahi ya chombo na wananchi, hasa wanyonge na kukemea rushwa, hii ikawe kaulimbiu yenu katika jumuiya hii,” amesema Masoud.

Amewataka wajumbe wa ALAT wajitahidi kujenga serikali za mitaa zenye uwajibikaji, uwazi na zenye kusikiliza sauti za wananchi kwa kusimamia rasilimali.

Kwa mujibu wa Masoud, changamoto nyingi zinazotokea kwa wananchi ALAT ndiyo wa kwanza kuzitafutia ufumbuzi kabla ya kufika Serikali Kuu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa ALAT, Murshid Hashim Ngeze amesema ni vyema mikutano ya ALAT ifanyike kabla ya vikao vya Bunge na Baraza la Wawakilishi ili hoja zitakazoibuliwa ziweze kujadiliwa katika vikao hivyo.

“Hii itasaidia kwa wajumbe waliopo katika vikao hivyo kutoa mawazo yao na kuchukuliwa kufanyiwa kazi katika kipindi cha bajeti bungeni.

Katika mkutano huo, baadhi ya wajumbe walizungumzia maagizo yaliyotolewa jana Aprili 23, 2024 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Mohamed Mchengerwa wakati akifungua mkutano huo, kuhusu kuondoa migongano baina yao, kutatua kero na kusimamia ukusanyaji wa mapato kwenye halmashauri zao.

Katika mchango wake, Meya wa Jiji la Mbeya, Dormohamed Rahmat amesema hawana budi kuyafanyia kazi maagizo hayo kwa kuwa mapato ndiyo msingi wa maendeleo katika maeneo yao na yanapunguza mzigo kwa Serikali Kuu.

“Mimi katika halmashauri yangu tumejiandaa kukuza vyanzo vya mapato bila kuwaumiza wananchi,” amesema Rahmat.

Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ally amesema katika mabaraza yanayojielewa kuanzisha vyanzo vya mapato ni lazima iwe ajenga yao katika kujiimarisha na kuwa zinafikiria hilo kila wakati.

Amesema kuna baadhi ya halmashauri zinazima mashine katika kufanya kazi zao, lakini katika halmashauri yake hilo halipo kwa sababu kipo kitengo maalumu kinachohusika na masuala ya Tehama kudhibiti ubadhirifu.

“Watu wanaohusika na kitengo hicho ukizima mashine unapaswa kutoa taarifa kwa nini umeizima ili kujiridhisha na tunahakikisha mashine ya mapato haiingii bila kusajiliwa,” amesema Ally.

Akifungua mkutano huo, Waziri Mchengerwa alisema licha ya kuwapo halmashauri ambazo zimefanya vizuri katika makusanyo, baadhi zinatumia mashine hewa kufanya manunuzi.

Alisema taratibu zote za manunuzi ya kikodi zinapaswa kuzingatia mifumo ya kielektroniki ili kupunguza mianya ya rushwa na udaganyifu katika maeneo yao.

Related Posts