Tabora. Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Deusdedit Katwale ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama wilayani humo kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wanaotuhumiwa na mauaji ya mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Kalunde, Salma Mussa (15).
Salma ameuawa Julai 8, 2024 wakati akielekea shuleni na inadaiwa kuwa licha ya kuuawa, alichomwa moto na watu wasiofahamika.
Akieleza tukio hilo leo matatu Julai 15, 2024 mjini Tabora, baba mzazi wa Salma, Mussa Athuman amesema mtoto wake alipotea tangu Julai 8, 2024 hadi alipoonekana akiwa amefariki na mwili wake kuchomwa moto.
“Mtoto wangu alipotea alipokwenda shule Julai 8, 2024 na hakurudi. Tukaanza kumtafuta kwa makundi, hadi Julai 11 tulipompata akiwa porini na ameuawa.
Akizungumza wakati wa mazishi ya Salma Mussa (15), Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Deusdedit Katwale amesema Serikali imesikitishwa na kitendo na tayari vyombo vya ulinzi vimeanza kuwasaka watuhumiwa.
“Tangu nifike hapa Tabora hili ni tukio la kwanza, kama Serikali hatutakubali matukio kama haya yakitokea kwenye wilaya yetu, tangu tulipopata taarifa za tukio hili tumeanza kuchukua hatua, lakini sitaweza kuzitaja kwa sasa.
“Natoa agizo kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwenye wilaya yetu, kuchukua hatua ili waliohusika wakamatwe na hatua kali zichukuliwe,” amesema.
Amewatoa hofu wananchi, akisema Serikali ina mkono mrefu na waliofanya ukatili huo watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Mwenyekiti wa kijiji cha Tumbi Manispaa ya Tabora, Rajab Hamsini amesema “Jukumu la ulinzi na usalama ni la wananchi wote, baada ya tukio hili tunawaomba wananchi wote tushirikiane kutoa taarifa sahihi kwa Serikali, ili washukiwa watiwe nguvuni kwa lengo la kukomesha matukio hayo.”
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Alhaji Ibrahim Mavumbi Sheikh amesema wanalaani tukio hilo alilosema linalotia doa mkoa.
“Kwanza kitendo hiki ni kitendo cha kinyama kumtendea mwanadamu mwenzako hata kama alikuwa na matatizo, zipo njia nyingi za kutatua matatizo kabla ya kuuana. Matukio haya ni ajabu kufanyika kwenye maeneo yetu, tunalaani kwa kiasi kikubwa,” amesema Mavumbi.