TIC yalenga uwekezaji wa Sh26.6 trilioni

Dar es Salaam. Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeeleza kuwa, mwaka huu kinalenga kusajili uwekezaji wa Dola 10 bilioni za Marekani (Sh26.6 Trilioni).

Leo Jumatatu, Julai 15 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC Gilead Teri, amewaeleza waandishi wa habari kuwa lengo hilo limewekwa wakati nchi ikiendelea kuvutia uwekezaji mkubwa kutoka nje na ndani kwa kuwa na sheria nzuri za uwekezaji na motisha.

“TIC inalenga kusajili miradi 1,000 yenye mtaji wa nje wa dola bilioni 5, na mtaji wa ndani wa dola bilioni 3.5,” amesema Teri na kuongeza kuwa, mwenendo wa uwekezaji kwa miaka mitano iliyopita ulikuwa mzuri.

Teri amesema Serikali ilifunga mwaka wa fedha wa 2023/24 kwa kusajili miradi 707 yenye thamani ya Dola 6.56 bilioni za Marekani ikilinganishwa na miradi 369 iliyosajiliwa kipindi kama hicho mwaka jana ikiwa na thamani ya Dola 5.39 bilioni.

Hata hivyo, amesema ushiriki wa ndani pia umekuwa wa kuvutia huku asilimia 38.19 ya miradi iliyosajiliwa ikimilikiwa na Watanzania, wageni wakimiliki asilimia 42.86 na asilimia 19.38 ni ya ubia kati ya Watanzania na wageni.

“Miradi hii (ya mwaka 2023/24) inatarajiwa kuzalisha ajira 226,585 ikilinganishwa na ajira 53,871 katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/2023,” amesema.

Sekta iliyoongoza kuvutia uwekezaji mkubwa ilikuwa  ya viwanda ikiwa na miradi 313 yenye thamani ya Dola 2.462 bilioni, ikifuatiwa na sekta ya usafirishaji yenye miradi 128 ya thamani ya Dola 1.03 bilioni.

Sekta ya ujenzi wa majengo ya biashara ilikuwa ya tatu ikiwa na miradi 76 yenye thamani ya Dola 1.07 bilioni, wakati utalii ulisajili miradi 75 yenye thamani ya Dola 349.40 milioni, na kilimo, ikiwa na miradi 56 yenye thamani ya Dola 710.02 milioni.

Kulingana na takwimu zilizotolewa na TIC, Dola 6.56 bilioni zilizorekodiwa katika mwaka wa fedha uliopita zilikuwa za juu zaidi kuwahi kutokea katika miaka mitano iliyopita ya fedha.
Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa katika mwaka wa fedha 2021/22 miradi 274 yenye ya Dola 2.24 bilioni ilisajiliwa, wakati mwaka wa fedha 2020/21 miradi 234 ilisajiliwa yenye thamani ya Dola 3.34 bilioni na mwaka wa fedha 2019/20 TIC ilisajili miradi 220 yenye thamani ya Dola 1.73 bilioni.

Teri amesema kwa kiasi kikubwa sheria na kanuni za uwekezaji zimekuwa na nafasi kubwa katika kuweka mazingira rafiki ya biashara na kushawishi imani ya wawekezaji.
“Motisha hizi ni pamoja na misamaha ya kodi kwa wawekezaji wa kawaida na wa kimkakati, kupunguzwa kwa ushuru wa forodha na vivutio vingine vya kifedha vinavyofanya uwekezaji nchini kuvutia zaidi,” amesema.
Pia, Teri amesema uamuzi wa Serikali kupunguza kiwango cha mtaji hadi Dola 50,000 kwa wawekezaji wa ndani utavutia usajili zaidi kundi hilo.
Aidha ili kuboresha urahisi wa kuwekeza nchini Tanzania, Serikali ina mpango wa kuimarisha huduma za Kituo kimoja cha Huduma (One Stop Service Centre) kwa kuanzisha mfumo wa mtandao wa kusajili miradi ya uwekezaji.
“Mfumo huu unaruhusu wawekezaji kusajili miradi yao kutoka popote duniani ndani ya siku moja hadi tatu,” amesema Teri.
Amesema mwelekeo wa kimkakati wa kituo hicho ni katika sekta muhimu, huku asilimia 10 ya miradi hiyo ikiwa ni ile inayochangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Related Posts