Dar es Salaam. Mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji, Najit Joginda ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kumpangia tarehe ambayo ataenda mahakamani hapo kwa ajili ya kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo na sio kwa ajili ya kesi yake kutajwa.
Joginda, maarufu Kipaya, ametoa maelezo hayo leo Jumatatu, Julai 15, 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga, wakati kesi hiyo ya mauaji namba 37224/2023 ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Mshtakiwa huyo ambaye ni mpanda farasi, alitoa maelezo hayo muda mfupi baada ya wakili wa Serikali, Pancrasia Protas kuieleza Mahakama hiyo kuwa wanakamilisha kuandaa nyaraka muhimu kwa ajili ya kuzipeleka Mahakama Kuu.
“Mheshimiwa hakimu, upande wa mashitaka tunakamilisha kuandaa vijalada (taarifa muhimu) kwa ajili ya kuzipeleka Mahakama Kuu, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa” amedai wakili Protas.
Upande wa mashitaka baada ya kueleza hayo, hakimu Mwankuga alikubaliana na ombi la kuahirisha kesi hiyo hadi Julai 29, 2024.
Hakimu Mwankuga baada ya kueleza hayo ndipo mshitakiwa Joginda alipouliza iwapo tarehe ijayo watasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo.
Kipaya ambaye kesi yake ilisikilizwa kwa njia ya video huku mshitakiwa akiwa rumande na sehemu ya maelezo yake ilikuwa kama ifuatavyo.
Mshtakiwa: Mheshimiwa hakimu siku hiyo kesi yetu itasomwa Commital Proceedings ( maelezo ya mashahidi na vielelezo)?
Mshtakiwa: Sasa nitaitwa lini? Maana hii kesi kila ikipangwa inatajwa tu.
Hakimu: Kesi ni process (mchakato).
Mshtakiwa: Kesi hii ni ya muda mrefu, tangu Februari 2023 ilipofutwa na kufunguliwa nyingine na upande wa mashitaka kila kesi inapotajwa wanakuja na majibu hayohayo.
Mshtakiwa: Mheshimiwa hakimu sisi tunaona msituite mahakamani hapa tarehe ijayo, tusubiri mpaka siku tutakapoitwa hapa kwa ajili ya kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo.
Hakimu: Tumepanga tarehe hiyo kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama upande wa mashitaka wameshasajili nyaraka hizo Mahakama Kuu.
Hakimu: Taarifa ya Mahakama ni siku 14 na kwa kesi ambazo hazina dhamana, zinatakiwa zitajwe kila baada ya siku 14, hivyo hata nyie kesi yenu itaitwa mahakamani tarehe hiyo.
Mbali na Kipanya, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ni Abibu Kilenge.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Januari 18, 2021 eneo la Kidole lililopo Chanika, walimuua Salehe Makule.