Mwanza. Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imetoa ruhusa kwa wakili Steven Kitale kuwasilisha maombi ya mapitio ya kisheria dhidi ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kuhusu uhalali wa wajumbe wa kamati ya uchaguzi ya chama hicho.
Pia kuhusu TLS kupandisha ada za wanachama wake kuhudhuria Mkutano Mkuu wa mwaka (AGM) kutoka Sh118,000 hadi Sh200,000.
Hata hivyo, Mahakama imesita kutoa amri kuzuia AGM ya TLS mwaka huu na kusimamisha mchakato wa uchaguzi mkuu wa chama hicho unaojumuisha shughuli za Kamati ya Uchaguzi na Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi, badala yake imemtaka mleta maombi kuwasilisha maombi ya mapitio ya kisheria kwanza.
Shauri hilo lililotawaliwa na upinzani wa hoja kutoka pande zote, limesikilizwa leo Jumatatu Julai 15, 2024, mbele ya Jaji Athuman Matuma kuanzia saa saba mchana na uamuzi kutolewa saa 2:30 usiku.
Katika shauri hilo, mleta maombi Kitale anawakilishwa na jopo la mawakili zaidi ya 20 wakiwamo Steven Makwega, Godfrey Basasingohe, Erick Mutta, Ernest Mhagama, Godfrey Goyayi na Angelo James.
Upande wa wajibu maombi, ambao ni TLS, Mkurugenzi Mtendaji wa TLS, Baraza la Uongozi la TLS, na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) umewakilishwa na Wakili Mkuu, Lameck Merumba, mawakili Subira Mwandambo, David Shiratu, na Hekima Mwapusi.
Mbele ya Jaji Matuma, wajibu maombi wakiwakilishwa na wakili Mwapusi walileta pingamizi wakiwa na hoja tano kwenye shauri la msingi la maombi ya mapitio ya kisheria.
Akisoma hoja hizo, Mwapusi amedai maombi ya Kitale hayana mashiko kisheria kwa kuwa yamewasilishwa mapema kinyume cha sheria, hakuambatanisha uamuzi unaolalamikiwa, kukosa uwezo wa kisheria, kiapo cha mleta maombi ni batili, na maombi ni ya kipuuzi, ya kero na matumizi mabaya ya mchakato wa Mahakama.
“Maombi haya hayana msingi wa kisheria, bali ni hila na ghiliba za kisheria. Mleta maombi anazuia mkutano mkuu wa mwaka (AGM) kwa masilahi gani? Mkutano wa mwaka gani? ya tarehe gani? Hajaeleza anazuia mchakato upi wa uchaguzi. Kwa hiyo tunaiomba Mahakama yako kutupilia mbali maombi hayo,” amedai Mwapusi mbele ya mahakama.
Hoja hizo za pingamizi baada ya Mahakama kuzisikiliza imezitupa kwa gharama.
Jaji Matuma amesema Mahakama imejiridhisha pasi na shaka kwamba hoja za mleta maombi zina nguvu na msingi kisheria wa kusimama na kusikilizwa.
Baada ya kutupilia mbali pingamizi la wajibu maombi,
“Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, mawakili wa mleta maombi wamewasilisha hoja wakirejelea yaliyozungumzwa kwenye kiapo cha mleta maombi. Kwa mujibu wa nyaraka hizo, katika mkutano wa dharura wa 10 wa Baraza la Uongozi la TLS, liliainisha ada, lakini kwa namna ambayo haijawekwa bayana,” amesema Jaji Matuma.
“Ni wazi kwamba muombaji, ambaye ana masilahi mapana kwenye jambo hili kama mjumbe wa Baraza la Uongozi, ana jukumu la kusimamia wajibu na uwajibikaji. Aliomba nyaraka zinazoidhinisha uteuzi wa Kamati ya Uchaguzi na Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi, lakini alinyimwa nyaraka hizo,” amesema.
Akisoma uamuzi, Jaji Matuma amesema Mahakama inakubaliana kuwa Kamati ya Uchaguzi wa TLS na upandishaji wa ada za wanachama kuhudhuria AGM ya 2024, kutoka Sh118,000 hadi Sh200,000, hazikupata baraka za wajumbe wote wa Baraza la Uongozi, hivyo uamuzi huo unakiuka misingi ya kisheria.
“Muombaji anasema kunyimwa nyaraka hizo kunamfanya aone mchakato wa uchaguzi umegubikwa na mapungufu ya kisheria na amethibitisha kesi inayohitaji ufafanuzi wa kimahakama na kisheria. Pia, uchaguzi ni mchakato wa kisheria na wasimamizi wa uchaguzi husika lazima wapatikane kwa kuzingatia miongozo ya kisheria,” amesema Jaji Matuma.
Akizungumza kwa niaba ya mleta maombi (Kitale), Wakili Erick Mutta amesema mteja wake ameridhishwa na uamuzi uliotolewa na Mahakama, akiahidi kufungua shauri la maombi ya mapitio ya kimahakama na zuio la muda la mchakato wa uchaguzi mahakamani kesho Jumanne Julai 16, 2024.