Dar es Salaam. Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Harun Nyagori amesema takribani asilimia 70 hadi 80 ya dawa za maumivu zina chumvi.
Hali hiyo amesema huweza kumfanya mtu anayezitumia dawa hizo mara kwa mara kupata athari sawa na yule anayekula chumvi nyingi.
Profesa Nyagori amesema hayo leo Jumatatu Julai 15, 2024, wakati akichangia mada katika Mwananchi Space iliyoandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL), ikiwa na mada isemayo ‘matumizi holela ya chumvi na sukari yanavyochangia magonjwa yasiyoambukiza nini kifanyike.’
“Hivyo hii inaweza kumfanya mtu anayetumia dawa hizi kila wakati kuwa sawa na mlaji chumvi kwa kiasi kikubwa. Kuna matumizi ambayo si ya moja kwa moja, lakini wananchi wanashindwa kujua na wanajikuta wanatumia chumvi bila wao kujua,” amesema.
Licha ya kutakiwa kupunguza matumizi ya chimvi, amesema yapo mazingira ambayo mtu huweza kulazimishwa kuitumia, akieleza kuna baadhi ya wagonjwa huenda hospitali wakiwa na matatizo ya kukosa chumvi.
“Hivyo tunamlazimisha kwa sababu kuna muda ambao moyo ili ufanye kazi unahitaji chumvi,” amesema.
Kuhusu sukari, ameshauri ni vyema watu wakachagua kula tunda mojamoja badala ya kunywa glasi ya juisi ya matunda, ili kutoupa mwili kazi ya kushughulika na sukari nyingi inayoingia kwa wakati mmoja.
“Watu wengine wanadhani unywaji juisi huweza kuwafanya kuwa salama, lakini falsafa ni ileile ya kupunguza matumizi ya sukari,” amesema.
Kwa mujibu wa daktari wa binadamu, Zainab Abdallah ameshauri kuchagua kunywa maji ya kutosha, maji yenye ladha ya matunda na chai inayotokana na mimea, ili kuepuka matumizi ya vinywaji vyenye sukari nyingi.
Amesema matumizi ya vinywaji hivyo yanaweza kuwa mbadala wa soda na juisi.
“Kitu kingine kinachotuathiri ni kutotumia njia bora na nzuri ya kuzuia miili, tunakula vyakula hovyo vinayoweza kufanya miili kuongezeka. Hii inasababisha matatizo kama vile magonjwa ya shinikizo la damu. Hivyo ni vyema kula milo kamili na kupunguza matumizi ya chumvi na sukari,” amesema.
Dk Zainab amesema ni muhimu kula vyakula vyenye virutubisho vya kutosha, ambavyo havihitaji kuongeza chumvi na sukari.
“Pia matumizi ya viungo vya asili kama vile vitunguu na tangawizi vinaweza kusaidia kupunguza matumizi ya chumvi kwa wingi,” amesema.
Mkuu wa Tathimini na Usajili wa Bidhaa za Chakula Zanzibar (ZFDA), Khadija Sheha amesema watu wengi hawazingatii usomaji wa maelekezo kwenye vifungashio vya bidhaa, bali huangalia tarehe ya kutengenezwa na ya mwisho wa matumizi.
Amesema vifungashio vyote huonyesha kilichomo ndani ya bidhaa, kwamba ina virutubisho gani na mtu anatakiwa kula kwa namna gani.
“Kwa bahati mbaya watu wengi hatuna desturi ya kusoma vifungashio, mimi nikinunua krispi paketi moja naona imendikwa gramu 300 lakini natakiwa nile kwa kiasi gani, ili nisile chumvi kupitiliza au sukari kupitiliza? lLakini hatuna kawaida kama walaji kusoma maandishi yaliyopo,” amesema Dk Khadija.
Amesema maandishi hayo hutoa taarifa, lakini walaji wanaangalia zaidi mwanzo wa matumizi na mwisho wake na taarifa kama chakula kina chumvi nyingi kiasi gani hawakumbuki.
Kutokana na hali hiyo, Dk Khadija amesema elimu zaidi inaendelea kutolewa kwa wananchi, ili wasome maelekezo hayo kuepuka kutumia sukari kupitiliza, hivyo kujiepusha na magonjwa yanayoweza kujitokeza.
Imeshauriwa ziwepo kampeni za utoaji taarifa sahihi ya nini kifanyike na kipi , ili kubadili mtindo wa maisha wa kila siku wa mtu.
Ushauri huo umetolewa na Ofisa Afya ya Uzazi na Lishe kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Edwin Swai, aliyesema shirika hilo hutoa mapendekezo, lakini wanazungumzia kwa mapana zaidi katika mabadiliko ya mifumo ya sheria ambayo inalinda walaji na wanaotengeneza.
Amesema ni vyema kuhakikisha sehemu kama vile shule, hospitali na migahawa, matumizi sahihi ya chumvi yanazingatiwa.
Dk Swai amesema hata wanaoingiza bidhaa hiyo wajue ni kwa kiwango gani na ikizidi haitaingizwa.
“Ni vyema kiwango cha chumvi kiandikwe kwenye bidhaa, ili mtu akitaka kununua ajue ina chumvi kiasi gani,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Swai, uwepo wa taarifa sahihi ni muhimu hasa kwa bidhaa zinazohamasisha ufanyaji wa mazoezi yanayosaidia kupunguza uwepo wa magonjwa yasiyoambukiza.
Madini joto katika chumvi
Mhariri wa Afya wa Gazeti la Mwananchi, Herrieth Makwetta, amesema utafiti wa chumvi uliofanyika nchini mwaka 2019 umebaini Tanzania ina uwezo wa kuzalisha takribani tani 330,712 za bidhaa hiyo kwa mwaka.
Makwetta amesema kati ya chumvi inayozalishwa, asilimia 57 hurutubishwa kwa madini , lakini asilimia 43 haina madini hayo kabisa.
Utafiti huo amesema umebaini chumvi isiyo na madini joto inazalishwa na wazalishaji wadogo-wadogo ambao wako zaidi ya 7,000 kwa wale wanaozalisha chini ya tani 50 kwa mwaka.
Amesema wazalishaji hao wanatumia teknolojia duni na wametawanyika katika maeneo kadhaa ambayo hayafikiki kwa urahisi, ili kuwapatia utaalamu elekezi wa uzalishaji bora wa chumvi.
“Tafiti zaidi zinaonyesha Tanzania inaendelea kukabiliwa na tishio la magonjwa yasiyoambukiza, huku waathirika wakuu wakiwa ni watu wenye zaidi ya miaka 50, ambao hata hivyo waishio vijijini hufariki dunia bila hata kupatiwa vipimo wala matibabu,” amesema.
Utafiti uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Kutetea Masilahi ya Wazee la HelpAge, umeonyesha watu wenye umri zaidi ya miaka hiyo hawana uhakika wa vipimo wala matibabu.
Makwetta amesema katika hilo, wataalamu wameonya upungufu wa madini yanayopatikana kwenye chumvi yanaweza kusababisha magonjwa yakiwamo goita au madhara kwa watoto wachanga, lakini madini hayo yakizidi mwilini husababisha magonjwa yasiyoambukiza.
Amesema uwekaji wa chumvi ambayo haijapikwa kwenye chakula hutoa asilimia 90 ya madini ya sodiamu ambayo humweka mtu hatarini kupata shinikizo la juu la damu, kifafa cha mimba, saratani ya tumbo, magonjwa ya figo, moyo na mishipa.
“Ikumbukwe chumvi ndiyo kiungo kikuu cha sodiamu katika lishe ya binadamu. Mwili unahitaji sodiamu kwa kazi nyingi, kazi yake kuu ni utendaji sahihi wa seli na udhibiti wa maji, nguvu na shinikizo la damu,” amesema.
Kiwango kinachopendekezwa ni kula chini ya gramu tano za chumvi kwa siku, ambayo ni sawa na takriban kijiko kimoja cha chai.
Chumvi husaidia kuweka hali ya msawazo ya kimiminika kinachopatikana kwenye mwili wa binadamu ambao umetawaliwa na maji.
Kuhusu sukari amesema upo utafiti ambao umebaini asilimia 92.8 ya wazee vijijini hawakuwahi kupimwa kisukari, asilimia 68.8 ya waishio mijini hawakuwahi kupimwa kabisa magonjwa hayo.