Nswanzurimo out, Kitambi in Singida BS

UONGOZI wa Singida Black Stars, umefanya mabadiliko katika benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na Patrick Aussems raia wa Ubelgiji kwa kumuongeza Denis Kitambi.

Awali benchi hilo lilikuwa na Aussems ambaye ni kocha mkuu akisaidiwa na Ramadhan Nswanzurimo raia wa Burundi ambaye ameondolewa na nafasi yake imezibwa na Kitambi.

Taarifa kutoka ndani ya Klabu ya Singida Black Stars, zimelithibitishia Mwanaspoti kuwa Kitambi amepewa mkataba wa mwaka mmoja kusaidiana na Aussems ambapo wawili hao wameshawahi kufanya kazi pamoja katika nafasi hizo ndani ya kikosi cha Simba msimu wa 2018-2019 na 2019-2020 kabla ya Aussems kufungashiwa virago Novemba 2019.

Mwanaspoti linafahamu kwamba Nswanzurimo mwenyewe ameamua kuondoka kikosini hapo na leo hakukaa katika benchi wakati timu hiyo ilipocheza mechi ya mwisho ya Kagame dhidi ya El Merriekh Bentiu ya Sudan Kusini na kushinda 3-1.

Mtoa taarifa wetu amebainisha kwamba, sababu za Nswanzurimo kuondoka kikosini hapo ni kutoelewana na Kocha Aussems.

“Muda wowote kuanzia sasa taarifa itatoka kwamba Nswanzurimo si kocha tena wa Singida Black Stars, nafasi yake inachukuliwa na Denis Kitambi.

“Mabadiliko hayo yanakuja mapema kutokana na Nswanzurimo mwenyewe kuamua kuondoka baada ya kutoelewana na Kocha Mkuu Aussems.

“Tayari Nswanzurimo ameaga katika group la WhatsApp na ame-left tangu jana akisisitiza kwamba hayupo tena katika timu ndio maana leo hajakaa katika benchi katika mchezo wa mwisho wa Kagame,” kilisema chanzo hicho.

Ikumbukwe kwamba, Juni 12 mwaka huu Nswanzurimo alitambulishwa kuwa kocha msaidizi na mchambuzi wa video wa timu hiyo ambapo amedumu kwa takribani siku 33.

Kitambi anaibukia Singida Black Stars baada ya msimu uliopita 2023-2024 kuishusha daraja Geita Gold kutoka Ligi Kuu Bara ambapo alikuwa kocha mkuu wa kikosi hicho.

Related Posts