Joto ni kubwa kwa walimu, wanafunzi na wazazi katika maandalizi ya mitihani ya kidato cha nne.
Katika maandalizi ya mitihani hii, ambayo kitaalamu tunaweza kuibatiza kama ‘tathmini tamati’, wazazi wanaosomesha watoto shule za binafsi huwa katika wakati mgumu, kwani michango mbalimbali kwa wamiliki wa shule huwa haimithiliki.
Katika kipindi hiki, ada rasmi hubaki pale pale lakini michango huibuka ya kila namna, ilimradi tu wanafunzi waweze kuandaliwa vyema na kufaulu vizuri.
Wazazi wengi wanalia na gharama zinazoongezeka kwa watahiniwa hawa.
Leo kuna michango ya wanafunzi kubadilisha mlo, mchango wa mitihani shindanishi na shule jirani, mchango wa kula kuku mwishoni mwa wiki, mchango wa kununua kahawa ili wanafunzi wasome zaidi pasipo kusinzia.
Mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne ina maana kubwa katika maisha ya wanafunzi wengi nchini Tanzania.
Ni hatua muhimu inayowaruhusu wanafunzi kutathminiwa kitaifa na kuamua hatua zao za baadaye kielimu.
Mitihani hii inatoa nafasi kwa wanafunzi kuingia vyuo vikuu, vyuo vya kati na vyuo vya ufundi stadi, hivyo kufungua milango ya fursa mbalimbali za kielimu na ajira.
Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne yanaweza kuwa na athari kubwa kwa maisha ya wanafunzi, ikiwemo kupata udhamini wa masomo na nafasi za kazi nzuri.
Hii ni hatua muhimu kwa wanafunzi na wazazi kwani inawakilisha mwisho wa safari ya elimu ya sekondari na mwanzo wa fursa mpya.
Kujiandaa kwa mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne kunahitaji nidhamu na bidii kubwa kutoka kwa wanafunzi.
Mchakato wa maandalizi unahusisha kusoma kwa kina na mara kwa mara, kufanya majaribio ya kujipima na kushiriki katika masomo ya ziada.
Wanafunzi wanahitaji kuweka mipango ya masomo na kudhibiti muda wao kwa ufanisi ili kuhakikisha wanakamilisha mtalaa wote na kuelewa masomo yote yanayohitajika.
Mbali na hayo, wanafunzi wanapaswa kujitunza kiafya kwa kula vizuri, kufanya mazoezi, na kupata usingizi wa kutosha ili wawe na afya bora na akili timamu wakati wa mitihani.
Ushirikiano mzuri na walimu na wazazi pia ni muhimu katika safari hii ya maandalizi, kwani wanatoa mwongozo, motisha, na msaada unaohitajika kwa wanafunzi kufaulu mitihani yao.
Lakini baadhi ya wazazi wanaosomesha watoto kwenye shule binafsi jijini Dar es Salaam wamelalamikia michango hiyo, huku wengine wakisema hawana namna.
“Nina binti yangu (shule imefichwa) kaambiwa alete fedha ya mlo maalumu ambao ni kwa ajili ya kidato cha nne.
‘‘Bado juzi kati hapa baada ya kumalizia likizo nimelipia fedha ya masomo ya ziada, tofauti na ada elekezi, ambayo kwa mwaka ni zaidi ya milioni tatu,” alieleza mzazi ambaye hakutaka kutajwa gazetini.
Katika taratibu za Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), ni vigumu kumhamisha mwanafunzi ambaye tayari alikwishasajiliwa na yuko kwenye kipindi kinachokaribia ratiba ya mitihani.
Hata hivyo, inaruhusiwa kwa mwanafunzi husika kufanya mitihani hiyo akitokea nje ya kituo, endapo kuna matatizo fulani hasa ya kiafya ama kinidhamu.
Pamoja na Serikali kuwa na utaratibu wa kutoa elimu bila malipo, fursa hii bado inakosa wateja wa kutosha kufuatia baadhi ya wazazi kutilia shaka ubora wa elimu hiyo kwa baadhi ya shule, hivyo kujikuta wakikutana na kadhia ya michango isiyomithilika kwenye shule za binafsi.
Miaka ya hivi karibuni, baadhi ya wabunge walipaza sauti juu ya utaratibu wa kupunguza michango na gharama kubwa shule binafsi na kuitaka Serikali ifikirie kuweka ada elekezi.
Mjadala huu unaonekana ulipata upinzani mkubwa kwani wabunge walio wengi wamewekeza katika biashara ya elimu, huku wamiliki wa taasisi hizi wakilalamikia kodi kubwa ambazo zinakadiriwa kuwa zaidi ya 15.
Kwa mtazamo huu, mzazi anayekataa kusomesha mtoto kwa utaratibu wa elimu bure, ni sharti akae mkao wa kuchangishwa mpaka hewa anayovuta mwanawe akiwa shuleni.
“Kimantiki haingii akilini nilazimike kulipia masomo ya ziada na chakula maalumu kwa mwanafunzi wa kidato cha nne ilhali nimekwishalipia ada. Shule inapaswa kuwa na bajeti yenye vipengele vyote hivyo kwa mujibu wa sheria,” alisema mzazi mmoja ambaye mtoto wake yuko shule ya bweni jijini Dar es Salaam.
Kuna michango ambayo haiepukiki kama vifaa vya maabara na masomo ya ziada au mitihani shindanishi ili kuwapima vijana kabla ya kuingia kwenye mtanange unaotarajiwa, lakini ni sharti gharama hizi ziwekewe ukomo na Serikali kupitia wathibiti ubora wa elimu.
Pamoja na umuhimu na ubora uliopo katika shule binafsi, baadhi ya taratibu zinakinzana kabisa na maisha halisi ya mzazi anayetafuta maisha.
Ndiyo maana baadhi ya wateja wanaposomesha watoto wao kidato cha nne, katu hawana hamu tena kuwapeleka vidato vinavyofuata katika shule hizo.
Kufuatia uamuzi huu, shule nyingi zenye kidato cha tano na sita zimejikuta zikikosa wanafunzi na wachache walipo hujikuta wanarundikiwa gharama kubwa za uendeshaji kama ilivyo kwa hawa wanaojiandaa na mitihani ya kidato cha nne.
Hatupaswi kama nchi kuwa na ubaguzi katika elimu. Nchi nyingi barani Afrika zina shule za umma ambazo zimekwishapiga hatua kiubora kiasi kwamba mzazi haoni sababu ya kumpeleka mtoto taasisi binafsi.
Nchini Rwanda shule nyingi za binafsi zimeingia ubia na shule za umma ili waweze kupata wanafunzi na kupunguza gharama za uendeshaji. Tanzania nasi tunaweza kuelekea katika mstari huu wa Rwanda.