KIKOSI cha Simba kipo Misri kikijiandaa na msimu mpya wa 2024/25 bila kuwa na kipa namba moja kwa misimu takriban sita kabla ya ule uliopita, Aishi Manula.
Kipa huyo ameachwa nyumbani kwa kile kinachodaiwa kwamba hayupo katika mipango ya timu, lakini mwenyewe inadaiwa kwamba hajaambiwa kitu.
Manula anadaiwa kwamba anatamani kuondoka Msimbazi, lakini bado ana mkataba wa mwaka mmoja aliosaini Julai, 2022.
Aishi anadaiwa kwamba alishaona dalili za kutohitajika tangu msimu uliopita, hivyo ulipoisha tu msimu wa 2023/24 akaenda klabu aliyowahi kuichezea zamani, Azam FC kuulizia kama anaweza kupata ‘hifadhi’.
Azam FC wakamkubalia, lakini kwa masharti kwamba hawataki migogoro na Simba, hivyo akamalizane nao mwenyewe. Akaenda kuongea nao (Simba) wakamwambia kama amepata timu aiambie hiyo timu ipeleke ofa.
Akaenda kuwaambia Azam nao wakapeleka barua ya kumuomba kwa mkopo. Lakini barua haikujibiwa hadi Simba wakaenda Misri na inaelezwa hakuambiwa kama timu inakwenda.
Akarudi kuwauliza kwanini hawajibu barua au kama hawataki kumtoa kwa mkopo, basi wawajibu Azam ili hatua zaidi zichukuliwe ikiwemo ofa ya kumnunua, lakini Simba wako kimya.
Nia yao, inadaiwa kwamba akae bila kucheza msimu mzima kwa kile kinachodaiwa kwamba kama sehemu ya kisasi kwake.
Viongozi wa Simba wanadaiwa kuwa na hasira na Aishi kwa mambo mbalimbali yaliyotokea wakati wa maisha yao ya pamoja. Kupitia makala hii nitaelezea mambo matatu ya Simba na Aishi kuwa katika mtanziko.
Aishi alijiunga na Simba 2017 akitokea Azam. Akasaini mkataba wa miaka miwili hadi 2019. Ulipoisha huo hakutaka tena kusaini mkataba wa miaka miwili akataka mitatu.
Huu haukuwa utaratibu wa Simba, hivyo viongozi walipinga sana. Lakini yeye akasisitiza hataki miaka miwili anataka mitatu na kama hawampi miaka mitatu hasaini.
Simba wakawa hawana namna huwezi kukubali kumpoteza Aishi kwa sababu ya mwaka mmoja unaozidi kwenye mkataba, wakakubali. Akasaini miaka mitatu hadi 2022. Mkataba huo ulipoisha akataka tena mitatu, Simba wakaona huyu mtoto sasa anawapanda kichwani wakataka kukaza ili kumpima.
Naye akakaza, kwamba hasaini kama sio miaka mitatu.
Simba wakarukaruka mwisho wakakubali japo kwa shingo upande, akasaini.
Lakini safari hii wakaapa kwamba hawatakubali ‘kuchukuliwa tena mateka’ na Aishi, wakaanza kujiandaa na maisha bila yeye.
Katika mkataba mpya wa 2022, Aishi hakutaka tu miaka mitatu, bali na hela ya mafuta ya gari yenye thamani ya Sh300,000 kwa mwezi.
Lakini tangu asaini mkataba huo Julai 2022, Aishi hakuwahi kupewa hela hiyo hadi alipochukua hatua Aprili 2023.
Ilikuwa kuelekea mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Ihefu Aprili 7, 2023 kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Simba walikuwa wametoka Morocco kucheza mechi ya mwisho ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Raja Casablanca.
Walipofika nchini waliingia kambini moja kwa moja, na wachezaji wote kasoro Aishi. Yeye aligoma hadi apewe hela yake ya mafuta kama walivyokubaliana kwenye mkataba.
Viongozi wakamuacha wakiamini mechi iliyopo mbele dhidi ya Ihefu sio kitisho, hivyo kipa namba mbili wakati huo, Beno Kakolanya angeweza kuimudu.
Baada ya mechi ndio wangekaa na Aishi kuzungumzia madai yake na kuyamaliza. Lakini siku moja kabla ya huo mchezo viongozi wakapata taarifa kwamba Kakolanya amesaini kuitumikia Singida Big Stars msimu utakaokuja.
Viongozi wakapata ‘ubaridi’ baada ya kuunganisha nukta za mmiliki wa Singida Big Stars na uhusiano wake na watani wao wa jadi, yaani Yanga. Wakahofia kwamba kutokana na ukaribu huo yawezekana Kakolanya akatumika kuwahujumu ili watolewe, hivyo asicheze mchezo huo.
Ukimtoa Kakolanya kipa aliyebaki alikuwa Ally Salim ambaye viongozi hawakuwa na imani naye kutokana na uchanga wake, hivyo wakampigia magoti Aishi aje acheze mechi hiyo.
Kitendo cha kumpigia magoti kiliwakera sana viongozi hao wakajiona wamekuwa wanyonge mbele ya mchezaji wao.
Wakakumbuka alivyowasumbua kwenye kusaini mkataba na bado anawanyanyasa hadi wampigie magoti, wakadhamiria kumfundisha adabu wakati sahihi ukifika.
Aishi akaja kucheza mechi ya mashindano bila kufanya mazoezi, huku akili yake ikiwa imewekwa kwenye hali ya kugoma.
Mpira wa miguu unachezwa kichwani kupitia akili, miguu ni vifaa tu vya kuchezea. Kwa hiyo akili ikiwa kwenye mgomo, mwili nao unakuwa hukohuk, ukilazimisha ndipo majeraha huja kama matokeo.
Na ndicho kilichotokea kwa Manula, akaumia katika mchezo huo na kukaa nje kwa miezi takriban sita.
Msimu wa 2022/23 ukaisha na Aishi hajapona, Simba ikabidi watafute kipa mwingine ndipo akaja Ayoub Lakred. Viongozi wanadaiwa kwamba wakaona sasa wakati sahihi umefika.
Lakini Ayoub naye hakuanza vizuri, hivyo Aishi akaendelea kusubiriwa kwa hamu na gamu. Mungu bariki, ikaja mechi ya watani wa jadi, Novemba 5, 2023. Hadi hapo Ayoub ameshaharibu sana, watu wakawa na hofu naye wakampa Aishi jukumu la kulinda heshima.
Bahati mbaya sana kwake akachezea lile kono la nyani (5-1). Hapo sasa inadaiwa kwamba wakawa wameshampata. Hapo ndipo Aishi alipoanza kupoteza umuhimu ndani ya Simba.
Na viongozi wakapata uhalali. Na bahati mbaya zaidi kwake, nyota ya Ayoub ikaanza kung’ara kwa kufanya uokoaji mzuri kila mechi. Kabla watu hawajapona donda la 5-1 ikaja mechi ya Tanzania Prisons pale Morogoro.
Aishi akiwa na siku mbaya kazini, Simba ikafungwa 2-1 kwa mabao ya Samson Mbangula. Baada ya hapo inadaiwa kwamba wakawa wameshinda vita sasa kilichobaki ni uamuzi tu juu yake.
Hachezi na haondoki hadi mkataba wake uishe. Na ndicho kinachoendelea…hawamuuzi, hawamtoi kwa mkopo na wala hawamchezeshi.
Taarifa za ndani ni kwamba atakwenda Misri kuungana na timu kwa sababu sheria za Fifa zinalazimisha timu kumpa mchezaji haki ya kufanya mazoezi.
Lakini msimu wa 2024/25 unaweza ukawa wa kuchoma mahindi kwa Aishi kama hakutakuwa na namna nyingine, na iwapo makipa wenzake watawaka kuliko yeye.