Kashai Mtafanya Biashara Kidijitali: Waziri Nape

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Stephen Byabato wametinga katika Soko la Kashai mjini Bukoba jana usiku na kushiriki kikao cha wafanyabiashara wa soko hilo.

Wafanyabiashara wa soko hilo walikutana jana Julai 15, 2024 usiku kwa ajili kushiriki kikao kilichokuwa kikijadili namna ya kuboresha soko hilo ambalo linatakiwa kufanyiwa maboresho lililopo mjini Bukoba mkoani Kagera.

Mawaziri hao walifika sokoni hapo mida ya saa 2 usiku na kupata fursa ya kuzungumza nao kisha wakawapongeza wafanyabiashara hao kushiriki kikao hicho ambacho nao walikuwa wakitoa maoni yao ya kuboresha soko hilo baada ya kuona michoro ya awali kisha na wao kueleza nini kifanyiwe maboresho.

Nape amesema kushirikishwa kwa wafanyabiashara hao kutaondoa manung’uniko na lawama kwani kumekuwa na mtindo wa wafanyabiashara kutoshirikishwa kwenye baadhi ya miradi hivyo kupelekea misigano isiyokuwa na tija.

Waziri Nape ambaye alifika mkoani humo kwa ajili ya kuendelea na ziara yake mikoa ya Kanda ya Ziwa ya kukaguwa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano inayojengwa mikoa 26 ya Tanzania Bara ambapo anatembelea mikoa ya Kigoma, Kagera, Geita, Mwanza na Shinyanga.

Sambamba na hayo pia Waziri Nape ameahidi pindi soko hilo litakapokamilika watafungiwa intaneti ya bure (Free Wi-Fi) ili kuwawezesha kufanya biashara kidijitali.





Related Posts