Nakuru. Rais wa Kenya William Ruto ameishutumu Taasisi ya Ford Foundation ya Marekani kwa kudhamini maandamano ya Gen Z yaliyotokea mwezi uliopita nchini humo.
Ruto amesema hayo jana Jumatatu Julai 16, 2024 wakati akizungumza mjini Nakuru.
Amedai kuwa taasisi hiyo ililipa na kukodi waandamanaji waliosababisha ghasia.
“Nataka niulize watu wa Ford Foundation watuambie hiyo pesa wanatoa, wanatoa ifanye fujo ndio wapate faida gani?
“Tutawaita na tutawaambia kama hawapendi demokrasia nchini Kenya, kama watafadhili vurugu na machafuko tutawaita na tutawaambia wao pia kujirekebisha au waondoke,”amesema Rais Ruto.
Pia, tovuti ya BBC imeripoti kuwa Ruto amesema kuwa Serikali yake haitamwacha yeyote anayewapanga vijana wa Kenya ili kusababisha ghasia barabarani wakati wa maandamano ya amani.
Juni, 2024 Kenya ilikumbwa na mfululizo wa maandamano ya vijana walikuwa wakipinga muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2024 pamoja na kupinga hali ngumu ya maisha.