RPC Mkama ataka wananchi kutunza miondombinu reli SGR

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama amekaa kikao na Polisi Kata wanao zihudumia Kata zilizopitiwa na mradi wa treni ya mwendokasi (SGR) na kupanga Mikakati ya Ulinzi wa miundombinu ya reli hiyo.

Akiongea na Polisi Kata hao wenye vyeo vya Wakaguzi na Wakaguzi Wasaidizi ,Rpc Mkama amesema, Morogoro imepitiwa kwa kiasi kikubwa na reli ya mwendokasi hivyo ni jukumu la kila askari kulinda miundombinu hiyo hususani Polisi Kata wanaofanya kazi kwenye Kata zilizopitiwa na mradi.

Kamanda Mkama amewataka Polisi Kata hao kuongeza kasi ya kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa reli hiyo ili wawe wanatoa taarifa kwao za uhalifu katika maeneo yao.

Aidha, Kamanda Mkama ameelekeza Polisi Kata kuwashirikisha viongozi wa Serikali wa Kata na mitaa au Vijiji pamoja na watu maarufu ili iwe rahisi kukubalika kwenye jamii na kupewa ushirikiano.

Reli ya mwendokasi inafanya safari zake kutoka Mkoa wa Dar es salaam hadi Morogoro na hivi karibuni itaanza safari za Dodoma na kufanya Wilaya kadhaa kupitiwa na treni hizo ikiwemo, Morogoro Mjini, Vijijini pamoja na Kilosa.

Boazi Akida Mkazi wa Morogoro ambaye anaishi jirani na Reli hiyo amesema watatoa ushirikiano kwa polisi Ili kuwabaini na kuwafichua watu wanaofanya uharibifu miondombinu hiyo.

Related Posts