Sintofahamu Manula akibaki Dar timu ikiwa Misri

SINTOFAHAMU inaendelea kwa kipa wa Simba, Aishi Manula aliyekuwa anadaiwa angejiunga na Azam FC iliyoweka kambi Morocco, lakini ajabu ni kwamba bado yupo jijini Dar es Salaam.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema haitaki kumtoa Manula kwenda Azam kwa mkopo isipokuwa inataka kumuuza, jambo linaloonekana ni gumu kufanyika.

Mmoja wa viongozi wa timu hiyo amesema Manula amebakiza mkataba wa mwaka mmoja, hivyo kumtoa kwa mkopo Azam wanaamini ni kuingia hasara na wanachotaka ni kumuuza ili kumalizana naye.

“Simba hakuna kitu itapata endapo Manula akienda kwa mkopo Azam maana amebakiza mwaka mmoja. Kinachotakiwa ni wao (Azam) wamnunue kwa dau walilowekewa mezani,” amesema kiongozi huyo.

“Manula bado ni mchezaji wa Simba kama walivyo wachezaji wengine, hayo mambo mengine ya kwenye mitandao hayahusiani na kitu chochote. Mchezaji mwenyewe anajua anajua mkataba wake unasemaje.”

Ingawa kiongozi huyo hakutaka kufunguka zaidi, ila Mwanaspoti linafahamu Simba ilitangulia kuhitaji huduma ya kiungo wa Azam, Feisal Salum ‘Fei Toto’, lakini iliwekewa dau kubwa na timu hiyo, jambo lililofanya na wao kumuuza Manula na siyo kumtoa kwa mkopo.

Msimu ulioisha haukuwa mzuri kwa Manula kutokana na kusumbuliwa na majeraha, ambapo Simba ilimsajili Ayoub Lakred ambaye aliisaidia timu hiyo kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Makipa waliopo Simba hadi sasa ni Lakred, Manula, Ally Salim, Hussein Abel na Ahmed Feruzi anayeweza kutolewa kwa mkopo.

Related Posts