Ziara hii ni juhudi za kuongeza ushirikiano wa Ujerumani na mataifa ya Afrika Magharibi, ili kuzuia kuenea kwa ukosefu wa usalama kunakoshuhudiwa kwa sasa katika mataifa ya ukanda wa Sahel.
Akizungumza mjini Dakar, Baerbock amesema usalama wa Afrika Magharibi na maendeleo ya siku zijazo ni mambo yanayohusiana kwa karibu na usalama na maendeleo ya Ulaya.
Baerbock ameongeza kusema kwamba na changamoto za kikanda,zinazoikabili Afrika magharibi kama ugaidi, uhamiaji, uhalifu na umaskini zinaathiri Ulaya moja kwa moja.
Soma pia: Annalena Baerbock
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani anatarajiwa pia kufanya ziara nchini Ivory Coast, ambayo pamoja na Senegal zinachukuliwa kama washirika wawili wakuu zaidi wa Ulaya, wakati ambapo mataifa mengi zaidi yanaigeukia Urusi kama mshirika.
Baada ya mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Senegal Yassine Fall jana Jumatatu, Baerbockamesema suala la ukosefu wa utulivu katika eneo la Saleh liko wazi.
“Kwa pamoja, hatuna dhana zozote kuhusu hali ya sintofahamu katika Sahel. Wapangaji wa mapinduzi wamezirudisha nyuma nchi zao, kiuchumi, kisiasa na pia katika uhusiano wao na Ujerumani.
“Hatuwezi kuendelea kana kwamba hakuna kilichotokea. Wakati huo huo, ni wazi pia kwamba Sahel iko katika ujirani wetu usio wa moja kwa moja. Matatizo na changamoto za kanda ya ugaidi, uhamiaji, uhalifu uliopangwa, umaskini – huathiri moja kwa moja, ikiwamo Ulaya. Ndio maana hatupuuzi hali hii, lakini tunachukua hatua katika mbinu sahihi zilizosalia.”
Mapinduzi ya kijeshi
Ziara ya Baerbock inajiri huku kukiwa na wimbi la ukosefu wa utulivu katika eneo la Sahel, ambao baadhi ya waangalizi wameuita Ukanda wa Mapinduzi, kufuatia mapinduzi ya kijeshi nchini Mali, Chad, Guinea, Sudan, Burkina Faso, Niger na Gabon tangu 2020.
Soma pia:Ugaidi na uhalifu uliopangwa wakithiri Sahel na kusambaa hadi pwani ya Afrika Magharibi
Viongozi wengi wa serikali mpya za kijeshi wameachana na uhusiano na Umoja wa Ulaya, wamejiondoa kutoka kwa Jumuiya ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS)na badala yake kugeukia usaidizi kutoka Vikosi vya Urusi. Hata hivyo Senegal na Ivory Coast wamedumisha mahusiano yao na nchi za Magharibi.
Akiwa nchini Senegal, Baerbock pia amefanya mazungumzo na Rais mpya Bassirou Diomaye Faye.
Haya yanajiri wakati waziri wa Maendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze anaandaa mkutano wa Muungano wa Sahel mjini Berlin, ambao unaratibu ushirikiano wa kimataifa wa maendeleo kwa Mauritania, Mali, Burkina Faso, Niger na Chad.