MASTAA wa kikosi cha Simba wamesema wana kila sababu ya kufanya makubwa msimu ujao kutokana na viongozi, benchi la ufundi kufanya kile kinachowapa mwanga wa kuhakikisha wanakuwa bora.
Simba ipo nchini Misri kujiweka tayari kwaajili ya msimu mpya huku mastaa hao wakiweka wazi kuwa msingi ni nidhamu na ushirikiano ili kufikia malengo yao 2024/25.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema kazi yao ni kupambana na kuvuja jasho kwaajili ya Simba mpya baada ya kushindwa kufanya vizuri misimu mitatu nyuma wakikosa mataji, sasa wanataka kurudi upya kwa ushindani.
Nahodha msaidizi, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ amesema wanapokea vitu sahihi hasa kipindi hiki ya maandalizi, wanajengwa kimbinu licha ya siku chache za kukaa pamoja wanaona mwenendo mzuri.
“Benchi la ufundi limekamilika na linatupa vitu ambavyo ni sahihi kwa wakati huu, kocha pia amekuja na mfumo mzuri aina ya mazoezi anayotupa ni mazuri kadri siku zinavyozidi kwenda yanatujenga,” amesema.
“Kiukweli tumekuwa na mwanzo mzuri tunasiku chache lakini mwenendo tunaokwenda nao ni mzuri siku zinavyozidi kwenda tutakuwa bora kuhakikisha tunanza vyema msimu ujao.”
Beki wa kati wa Simba, Che Malone alisema licha ya usajili mkubwa ambao umefanywa na klabu hiyo anatarajia msimu mgumu lakini watapambana kuhakikisha wanafikia malengo.
“Maandalizi ni mazuri ni siku tano sasa tangu tumeanza mazoezi ya kina kila siku tuna mabadiliko na nimeshuhudia kila mtu anautayari wa kufanya kazi kwa ajili ya kufikia mafanikio,” amesema na kuongeza:
“Uongozi na benchi la ufundi upo hapa kutupa ushirikiano wametupa kila kitu tunachokitaka lengo ni kuona tunafikia malengo, msimu huu tuna mataji matano ya kuyawania kwa mazoezi ambayo tunayafanya kila kitu kitaenda vizuri.”
Mkongwe Shomari Kapombe amesema mazoezi yanakwenda vizuri kikubwa ambacho kocha amewapa wao kama wachezaji wanaendelea kujifunza taratibu ili msimu mpya utakapoanza waanze kwa ushindani.
“Vitu ambavyo amesisitiza zaidi ni nidhamu, timu kuwa na umoja hivyo tunaendelea kujifunza taratibu wote kwa ujumla kwani wenyeji na wageni tumeanza kufundishwa pamoja.
“Kuna misingi mingine ambayo anaendelea kuijenga ya kiuchezaji pia tunaendelea nayo. Anasisitiza kwenye aina ya mifumo yake sambamba na kuhakikisha tunakuwa na utimamu wa mwili,” amesema Kapombe na kuongeza kuwa kocha Davids Fadlu anafurahishwa na namna wanavyopokea kwa uharaka maelekezo yake.